23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI IKIMALIZA HUKO IWAFIKIE PIA WALIONUNUA VYETI VYA DIGRII

KWA takribani wiki nzima sasa habari kubwa na ambayo imetawala katika si tu vyombo vya habari, bali katika midomo ya watu, ni uamuzi wa Serikali kuwaweka pembeni watumishi wake zaidi ya 9,932 wanaodaiwa kuwa na vyeti vya kughushi.

Miongoni mwa watumishi hao wamo wauguzi, madereva, walimu na watu wenye taaluma mbalimbali, ambao baadhi yao wamefanya kazi kwa muda mrefu.

Orodha ambayo imekwishatangazwa imeainisha wazi kwamba watu hao ni wale ambao ama cheti kimoja kimetumiwa na zaidi ya mtu mmoja, au wameghushi kwa maana rekodi zao kutoonekana Baraza la Mitihani nchini.

Tunaamini orodha hiyo pengine ni sehemu tu ya idadi kubwa ya watumishi ambao wana vyeti feki, haijalishi wanatumia majina yao au ambayo si yao, ambao bado wamebaki katika mifumo ya utumishi serikalini.

Tunasema hivyo kwa sababu tunafahamu kwamba vipo baadhi ya vyuo si tu vya hapa nchini, bali na nje ya nchi, ambavyo vimekuwa vikitoa vyeti vya digrii kwa fedha.

Kwa sababu hiyo, tunaamini lipo kundi la watumishi wenye vyeti feki vya shahada mbalimbali ambalo halijaguswa, hili ni lile ambalo limenunua vyeti halisi, hasa vile vya elimu ya juu kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali, vikiwamo vikubwa na vyenye sifa.

Tunaamini watu hawa pamoja na kwamba vyeti vyao vinaonekana kuwa ni halali kwa sababu vimetolewa na vyuo hivyo, lakini yaliyomo katika vichwa vyao hayaendani na vyeti vyao, kwa sababu walivipata kwa njia ambazo si halali.

Utendaji duni katika sekta mbalimbali, ukosefu wa maarifa katika kudhibiti rasilimali za Taifa, kushindwa kuandaa mikataba bora, maamuzi ya kukurupuka na ya kufuata upepo tunaamini chanzo chake ni kundi hili.

Pamoja na kwamba tunaunga mkono uamuzi wa Serikali wa kuwaondoa katika mfumo  wake wa ajira watu wote wenye vyeti feki, pengine sasa ni wakati muafaka wa kulitazama na kundi hili ambalo limejificha nyuma ya mgongo wa makaratasi ya vyeti halali vya digrii ilhali darasa hawalijui.

Ukitaka kufahamu kwamba jambo hili ni kubwa kiasi gani, nchini Marekani tunaelezwa kuwa idadi ya watu wanaopata Shahada ya Udaktari (PhD) kila mwaka ni kati ya 40,000 na 45,000.  Idadi ya watu wanaopata PhD feki ikiwa ni pamoja na kuanzia stashahada (diploma) kila mwaka inazidi 50,000. Kwa maneno mengine, inaelezwa kuwa zaidi ya nusu ya watu wote wanaodai kuwa na PhD wana digrii feki.

Tunatambua kwamba jambo hili ni gumu, linaitesa si tu Tanzania, bali dunia nzima, lakini tunadhani ni vyema sasa Serikali iongeze udhibiti, hasa katika vyeti vinavyotolewa na vyuo mbalimbali, ikiwamo vyuo vikuu nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles