MOGADISHU, SOMALIA
WAZIRI mwenye umri mdogo zaidi nchini Somalia, Abas Abdullahi Sheikh Siraji, ameuawa kwa kupigwa risasi mjini hapa baada ya msafara wake kushambuliwa karibu na Ikulu.
Waziri huyo wa Ujenzi wa Umma alipata umaarufu mkubwa baada ya kushinda kiti cha ubunge kuliwakilisha Jimbo la Jubbaland licha ya ugeni katika siasa.
Sheikh Siraji (31), ambaye alikuwa kipenzi cha wengi nchini hapa aliwahi kuishi katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyopo nchi jirani ya Kenya akiwa mtoto na kisha kurejea hapa mwaka jana kushiriki uchaguzi mkuu.
Watu wengi walimtaja kama mtu machachari miongoni mwa mawaziri na saa chache kabla ya kuuawa kwake alizindua mradi wa ujenzi wa jengo kwa ajili ya watumishi wa umma.
Wizara ya Habari ya Somalia imetoa taarifa ikisema washukiwa wa mauaji hayo tayari wamekamatwa.
Taifa hili la Pembe ya Afrika lililoathirika na machafuko liliendesha uchaguzi wake Februari mwaka huu ambapo Mohamed Abdullahi ‘Farmajo’ alichaguliwa kuwa rais mpya.