KIGALI, RWANDA
BINTI wa mfanyabiashara maarufu ambaye aliwahi kukiwezesha kifedha Chama tawala cha Rwandan Patriotic Front (RPF), ametangaza kuchuana na Rais Paul Kagame katika uchaguzi wa urais Agosti 4 mwaka huu.
"Kila mtu anaogopa kujieleza kwa sababu wanakiogopa chama tawala,” alisema binti huyo, Diane Rwigara, akiahidi kuondoa umasikini, ukosefu wa haki na usalama.
Rwigara (35), ambaye atawania urais kama mgombea binafsi, alijiondoa kutoka RPF baada ya kifo cha baba yake, Assinapol Rwigara mwaka 2015.
Anasema kifo hicho kilitokana na kuuawa, lakini polisi wanakataa tuhuma hizo wakisema alikufa kutokana na ajali ya barabarani.
Akiwa mfanyabiashara mwenye ushawishi mkubwa, baba yake alitengeneza utajiri kupitia mali zisizohamishika na alishiriki kikamilifu kuikuza RPF kifedha kabla na baada ya kuingia madarakani katika miaka ya 1990.
“Siko hapa kuzungumza kuhusu kifo cha baba yangu,” alisema Rwigara katika mkutano na wanahabari mjini japa juzi, lakini pia akikiri kuwa kifo hicho chenye utata kuwa moja ya sababu iliyomfanya ajitose kuwania urais.
“Sote tunajua hapa, watu hutokomea kitatanishi au kuuawa,” alisema akirejea ripoti za mashirika ya haki za binadamu.
“Watu pekee wanaopewa sauti ni wale wanaousifu utawala huu kandamizi," aliongeza.
Mwaka 2014, Shirika la Haki za Binadamu (HRW) lilieleza uwapo wa wimbi kubwa la watu kutoweka kitatanishi nchini Rwanda, ripoti, ambazo zilikataliwa na mamlaka.
Walipopigiwa simu na Shirika la Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), maofisa wa RPF na Jeshi la Polisi la Rwanda walikataa kueleza lolote kuhusu tuhuma alizotoa binti huyo.
Rwigara anakuwa mtu wa nne kujitokeza kujitosa katika mchuano huo akiungana na mgombea binafsi Philippe Mpayimana, mkuu wa chama cha upinzani cha Democratic Green, Frank Habineza na Rais Kagame.
Rwanda imekuwa ikisifiwa mara kwa mara kwa utulivu na ukuaji wa uchumi lakini inakosolewa vikali kwa ukosefu wa uhuru wa kisiasa na demokrasia.