Na KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
ANAYEDAIWA kuwa Kiongozi wa Taasisi ya Kusambaza Dawa za Kulevya nchini, Ally Haji, maarufu Shikuba na wenzake wawili, wamesafirishwa kimya kimya kwenda nchini Marekani usiku wa kuamkia jana.
Pamoja na rufaa iliyokatwa Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga uamuzi huo, Serikali imewaondoa bila kutoa taarifa kwa mawakili wala ndugu wa watuhumiwa hao.
Taarifa za kupelekwa Marekani Shikuba na wenzake; Iddy Mfuru na Tiko Adam, zilipatikana jana kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika, akiwamo mke wa mfanyabiashara huyo na mawakili wao.
Aprili 12, mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, ilikubali maombi ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe ya kutaka Watanzania hao washikiliwe na kusafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka ya kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya yanayowakabili nchini humo.
Baada ya uamuzi huo, Aprili 13, mwaka huu, mawakili wa Shikuba na wenzake; Hudson Ndusyepo, Majura Magafu na Adinani Chitale, waliwasilisha katika mahakama hiyo nia ya kukata rufaa na tayari waliwasilisha sababu za kukata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania kama sheria inavyowataka endapo hawakuridhika.
Akizungumza na MTANZANIA, mtoa taarifa mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina lake, alisema watuhumiwa hao wameshasafirishwa kuelekea Marekani tangu juzi saa sita usiku.
Mke wa Shikuba, Munira Ally, alipoulizwa kwa simu, alikiri kwamba mumewe alishasafirishwa na hawakupewa taarifa kuhusu kuondoka kwao.
“Waliondoka jana (juzi) saa tano na dakika kumi na ndege ya KLM kuelekea Marekani, sisi tumepata taarifa wakiwa wameshaondoka, hatuna jinsi walishaondoka.
“Baba mkwe hali yake ni mbaya baada ya kupata taarifa hizi, pale nyumbani watu wanajua wanazungumza anasikia… huwa anasumbuliwa na ugonjwa wa sukari na shinikizo la damu.
“Tunataka tukutane na mawakili tuzungumze nini cha kufanya, gerezani atakuwa kaacha vitu vyake, napanga utaratibu niende Gereza la Ukonga kufuata vitu mbalimbali zikiwemo nyaraka za rufaa,” alisema Munira.
Wakili Ndusyepo, akizungumzia hilo, alisema amesikia wateja wao wameondoka nchini juzi usiku, huku Serikali ikijua kwamba kuna rufaa Mahakama Kuu.
“Serikali inajua kuna rufaa imekatwa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, inaacha kuheshimu, sheria inadharauliwa, Katiba haifuatwi, leo wamefanyiwa hawa kesho watafanyiwa wengine, kuna haja ya kupiga kelele,” alisema.
Wakili Magafu alipotakiwa kuzungumzia suala hilo, alisema alipata taarifa ya kuondoka kwao kutoka kwa Ndusyepo.
Awali Aprili 10, mwaka huu, Serikali iliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pamoja na vielelezo mbalimbali, ikiomba watuhumiwa wazuiliwe na kusafirishwa kwenda Marekani kujibu tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Mahakama ilisikiliza maombi hayo Aprili 11, mwaka huu na kutoa uamuzi Aprili 12, ikibariki watuhumiwa hao kwenda nchini humo baada ya kujiridhisha kwa ushahidi uliotolewa mahakamani.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha aliposoma uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, alisema mahakama kabla ya kuamua ilijiuliza maswali kadhaa, ikiwamo kama mashtaka wanayohusishwa nayo wajibu maombi yako katika utaratibu wa kubadilisha wahalifu.
Pia mahakama ilijiuliza na kubaini kuwa kuna makubaliano ya kubadilishana wahalifu kati ya nchi hizo mbili.
Hakimu Mkeha alisema kama wajibu maombi watakuwa wanapingana na uamuzi huo, mahakama inawapa nafasi ya kukata rufaa ndani ya siku 15 na walifanya hivyo.
Mwakyembe aliwasilisha maombi Februari 15, mwaka huu, akiomba mahakama hiyo kuamuru Shikuba, Mfuru na Adam washikiliwe wakati wakisubiri kibali cha kuwasafirisha kwenda Marekani kujibu tuhuma za kula njama, kusafirisha na kusambaza dawa za kulevya nchini humo.
Jamhuri ikiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki, katika kuiridhisha mahakama iliwasilisha maombi na ushahidi dhidi ya wajibu maombi, kuonyesha kujihusisha kwao katika matukio hayo.
Ushahidi ulionyesha kwamba Marekani iliwachunguza wajibu maombi kwa miaka minne na walitumia Dola 10,000 kununua dawa hizo kutoka kwa taasisi yao ili kubaini ukweli.
Wajibu maombi ilibainika walikuwa wakisafirisha heroin na cocaine kwa kutumia magari, na wakifikisha dawa hizo Marekani huwatumia watu kusambaza kwa kutumia ndege binafsi na Shikuba ndio kiongozi wa taasisi hiyo.
Kakolaki alidai maombi yaliambatana na kiapo kilichoapwa na Richard Magnes ambaye anadai wajibu maombi wanatuhumiwa kuingiza dawa za kulevya zaidi ya kilo 1.78 Marekani.
Shikuba, ambaye amekuwa akihusishwa na biashara kubwa ya usafirishaji dawa za kulevya kati ya Afrika Mashariki, Asia, Ulaya na Marekani, alikamatwa mwaka 2014 nchini, akihusishwa na shehena ya kilo 210 za heroin zilizokamatwa mkoani Lindi mwaka 2012.
Serikali ya Marekani iliamua kutaifisha mali za mfanyabiashara huyo na kupiga marufuku kampuni za nchi hiyo kujihusisha na biashara zake.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Udhibiti wa Mali za Nje cha Wizara ya Fedha ya Marekani, ilieleza kuwa Shikuba ametambuliwa kama kinara wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi wa Vinara wa Dawa za Kulevya wa Nje ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, sheria hiyo imekuwa ikitumiwa na Marekani kufuatilia wahalifu kadhaa wanaojihusisha na biashara hiyo duniani na kwamba Shikuba amekuwa akijaribu mara kadhaa kurubuni viongozi wa Serikali za Afrika kuepuka kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana na biashara zake haramu.
Imeelezwa kuwa tangu mwaka 2006, Shikuba amekuwa akiongoza wanachama wa mtandao wake kutuma shehena za dawa za kulevya kwenda sehemu kadhaa duniani kama China, Ulaya na Marekani.