27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

VYETI FEKI VYAZUA KIZAAZAA

Na Waandishi Wetu-DAR/MIKOANI


NI kizaazaaa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya watumishi wa Serikali wanaodaiwa kughushi vyeti vya elimu, kuanza kufurika katika ofisi za wakurugenzi wa halmashauri kujua hatima yao.

 Watumishi hao wameanza kuchukua hatua hiyo jana baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki kuikabidhi orodha hiyo kwa Rais Dk. John Magufuli wiki iliyopita, ambaye aliagiza waliobainika kuondoka wenyewe katika nafasi zao kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA, umebaini kuwa baadhi ya huduma katika sekta ya afya na elimu zimeathiriwa kutokana na baadhi ya watumishi kuwamo katika orodha hiyo.

Mathalani katika mikoa ya Mbeya na Mtwara baadhi ya viongozi wa juu wamejikuta katika wakati mgumu kutokana na kukosa madereva wa kuwaendesha.

Pia baadhi ya watumishi waliotajwa kuwamo katika orodha hiyo, jana waliripoti kazini huku wengine wakionekana kuchanganyikiwa wasijue la kufanya.

 

MANISPAA YA ILALA

Orodha ya watumishi wenye vyeti feki iliyotolewa wiki iliyopita, inaonyesha katika Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam kuna watumishi 330 na ndiyo inatajwa kuongoza kwa kuwa na watumishi wengi.

MTANZANIA lilitembelea katika idara mbalimbali za manispaa hiyo, ikiwamo ya elimu na kushuhudia kundi kubwa la walimu wakiwa wanarandaranda katika ofisi ya Ofisa Elimu Msingi wakisubiri kumwona.

Wakati MTANZANIA linafika katika ofisi hizo, kulikuwa na zaidi ya walimu 20 waliokuwa ndani ya ofisi na wengine wakiwa nje wakisoma ubao wa matangazo.

Mmoja wa maofisa wa manispaa hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, alisema katika orodha hiyo wamo watumishi ambao tayari wamestaafu.

“Sasa sijui hawakuangalia payroll (orodha ya mishahara ya watumishi wa Serikali) wakati wanafanya uhakiki, kwa sababu wengine walioorodheshwa tayari walishastaafu,” alisema ofisa huyo.

 

TANGAZO LA NECTA

Tangazo lililotolewa na Baraza la Mitihani (Necta) lilionekana kuwapa ahueni baadhi ya walimu ambao walionekana wakihaha kuandika barua za malalamiko.

Baadhi ya walimu pia walionekana wakipiga picha tangazo hilo lililokuwa limebandikwa katika ubao wa matangazo nje ya ofisi ya ofisa elimu msingi, huku wengine wakiwa kwenye makundi wakitafakari.

“Ngoja tuandike tu barua tukatulie nyumbani tusubiri labda tutakuja kuitwa, kama kutakuwa na lolote mwalimu mkuu si yupo atatuambia,” alisikika mwalimu mmoja akimweleza mwenzake.

Tangazo hilo lilikuwa linawaelekeza watumishi wa umma wenye malalamiko kuhusu matokeo ya uhakiki wa vyeti vyao wawasilishe malalamiko yao kwa Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kupitia kwa waajiri wao.

“Barua za malalamiko ziambatanishwe na nakala za vyeti husika,” ilisema sehemu ya tangazo hilo.

 

HOSPITALI YA TEMEKE

Katika Manispaa ya Temeke, orodha inaonyesha kuna watumishi 270 wanaodaiwa kuwa na vyeti feki.

Miongoni mwa watumishi hao, wamo wa kada ya afya kama vile wauguzi, wataalamu wa maabara, wahudumu na wengine.  

Hospitali ya Rufaa ya Temeke pia imekumbwa na sakata hilo kwa baadhi ya watumishi wake kuwamo katika orodha hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Temeke, Dk. Amani Malima, alikiri baadhi ya watumishi wa hospitali hiyo kukumbwa na sakata hilo.  

Hata hivyo, Dk. Malima hakuwa tayari kutaja idara zilizoathiriwa.

“Tumeathirika, lakini tupo tunapambana na huduma zinaendelea kama kawaida,” alisema Dk. Malima.

 

MBEYA

Sakata la vyeti feki limezitikisa pia baadhi ya idara za Serikali mkoani Mbeya, ambako asilimia kubwa ya waathirika wanatajwa kuwa wanatoka idara za usafirishaji, afya na makatibu muhtasi.

Habari za kuaminika zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, zinaeleza kwamba ofisi hiyo imekumbwa na sakata hilo hasa kwa upande wa idara ya usafirishaji, wakiwamo madereva waliokuwa wakiwaendesha viongozi.

“Dereva aliyekuwa akimwendesha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya na hata Katibu Tawala wa Mkoa, wote wameguswa na sakata la vyeti feki.

“Hapa ninapoongea na wewe hawapo na tayari viongozi hao wamekabidhiwa madereva wengine,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho, kiliendelea kufafanua kuwa Halmashauri ya Jiji la Mbeya nayo imeguswa na sakata hilo, ambako dereva aliyekuwa akimwendesha Meya ameondolewa kazini baada ya jina lake kuonekana kwenye orodha ya watajwa wanaotumia vyeti feki.

Aidha, idara nyingine ambazo zinaonekana kuwa na idadi kubwa ya watumiaji wa vyeti feki ni ya afya, hasa katika halmashauri za Kyela, Mbarali, Rungwe na Busokelo na wengi ni wauguzi.

Gazeti hili lilimtafuta Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja, ambaye alisema yupo nje ya kituo cha kazi na kukabidhi jukumu hilo kwa Ofisa Utumishi wa Mkoa, Marko Masaya.

Alipoulizwa, Masaya alisema suala hilo bado halijafika rasmi ofisini hapo na kwamba kama litawasilishwa basi taarifa itatolewa, lakini hadi sasa nao wanaliona na kulisikia kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, taarifa rasmi kutoka ndani ya ofisi hiyo, zinaeleza kwamba baadhi ya wahusika ambao wametajwa kwenye sakata hilo, wameanza kuwasilisha taarifa za kupinga kwa madai kuwa vyeti vyao ni halali.

 

MTWARA

Madereva waliokuwa wakiwaendesha vigogo mkoani hapa, akiwamo Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara na Mkuu wa Wilaya ya Masasi, nao wamekumbwa na sakata hilo, hivyo kufanya hali kuwa tete.

Hali hiyo imesababisha viongozi hao kubadilishiwa madereva.

Taarifa za ndani kutoka katika ofisi ya katibu tawala wa mkoa, zinazonyesha kada zilizopata pigo ni pamoja na wauguzi, makatibu mahususi, madereva na walimu ambao ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu wamefikia 35.

Awali taarifa hizo zilidai kuwa watumishi wengi wilayani Nanyumbu waliposikia sekeseke la vyeti feki walikimbia wenyewe bila kusubiri uhakiki na baada ya uhakiki walibainika kuwa na vyeti feki.

 

PWANI

Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo iliyoko mkoani Pwani, nayo imekumbwa na sakata hilo baada ya baadhi ya watumishi kuwamo katika orodha hiyo.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa huduma za upasuaji katika hospitali hiyo zimesimama kutokana na mmoja wa wataalamu wa dawa ya usingizi kuwamo katika orodha hiyo.

 

KATIBU MKUU UTUMISHI

Gazeti hili lilipomtafuta Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Damas Ndumbaro, ili kuzungumza hali hiyo, hakupatikana ingawa hivi karibuni alitoa ufafanuzi na kusema kuwa majina yaliyotolewa ni ya awamu ya kwanza na siku chache zijazo itatangzwa orodha za awamu ya pili na tatu.

Alisema majina ya awamu ya kwanza yalihusisha watendaji wa Serikali za Mitaa, huku awamu ya pili ikihusisha taasisi, wakala wa Serikali na mashirika ya umma na awamu ya tatu itahusisha wizara na baadhi ya taasisi za Serikali.

“Majina yaliyotolewa hivi karibuni yalihusisha watendaji wa Serikali za Mitaa, lakini awamu ya pili na tatu ambayo inatarajiwa kutolewa wiki chache zijazo, itahusisha wizara, taasisi, wakala wa Serikali na mashirika ya umma, hivyo basi zoezi la kuwaondoa watendaji wenye vyeti feki bado linaendelea,” alisema Dk . Ndumbaro.

Hata hivyo, sakata hilo limeonekana kuwavuruga watendaji wa halmashauri mbalimbali nchini, ikiwamo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambako Katibu  Tawala wa Mkoa huo (RAS), Theresia Mmbando, aliitisha kikao cha dharura cha watendaji wa halmashauri zote za jiji hilo kujadili suala hilo.

Katika kikao hicho kilichoanza jana saa sita mchana, taarifa za ndani zinaeleza kuwa viongozi hao walikuwa wakijipanga kwa kuweka utaratibu mzuri wa namna ya kushughulikia malalamiko ya watumishi waliokumbwa na sakata hilo.

 

KATIBU NECTA

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk. Charles Msonde, amesema kuwa baraza hilo limewataka watumishi wenye malalamiko juu ya orodha ya wenye vyeti feki iliyotolewa na Serikali, kuyawasilisha kwa waajiri wao ili yaweze kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi Umma na Utawala Bora.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Dk. Msonde alisema kuwa watumishi hao wanapaswa kuwasilisha nakala halisi za vyeti vyao kwa waajiri wao ambao ni Utumishi.

“Tumetoa nafasi kwa wale wenye malalamiko, kweli tumetoa agizo hilo kwa waajiri kwamba yeyote mwenye malalamiko ayawasilishe kwao, tena na nakala halisi ya vyeti vyake na si vivuli ‘photocopy’ kama wengi wanavyodhani.

“Waajiri baada ya kupokea malalamiko hayo wayawasilishe kwa Katibu Mkuu Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili yashughulikiwe, maana ndiyo ngazi husika,” alisema Dk. Msonde.

Katika hatua nyingine, Dk. Msonde alisema kuwa hakuna watahiniwa wa kidato cha sita ambao wameshindwa kufanya mitihani jana.

Alisema taarifa zinazosambaa za kuwepo kwa watahiniwa hao si za kweli na kwamba zinapaswa kupuuzwa kwa sababu wanafunzi wote wamefanya mitihani.

“Mitihani imeanza leo (jana) na si kweli kwamba kuna watahiniwa wameshindwa kufanya mtihani, kila kitu kinakwenda sawa sawa kama kilivyopangwa na tunashukuru hakuna vitendo vya udanganyifu vilivyoripotiwa,” alisema.

 

MATOKEO YA UHAKIKI

Ripoti ya uhakiki wa watumishi wa umma nchini ilikabidhiwa wiki iliyopita na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki kwa Rais Dk. John Magufuli.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa watumishi 9,732 wamebainika kuwa na vyeti feki.

Rais Magufuli aliagiza watumishi hao wakatwe mshahara wa mwezi uliopita na pia wafukuzwe kazi na watakaoendelea kubaki kazini hadi Mei 5 wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwamo kufungwa jela miaka saba.

 

Habari hii imeandaliwa na Nora Damian, Patricia Kimelemeta, Christina Gauluhanga (Dar), Pendo Fundisha (Mbeya) na Florence Sanawa (Mtwara).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles