28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

ASALI YA TANZANIA NI BORA, UZALISHAJI MDOGO

NA HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM


WAFUGAJI nyuki nchini wametakiwa kuhakikisha wanatumia mizinga ya kisasa ili kupata asali yenye ubora utakaokidhi vigezo vya soko la kimataifa.

Tamko hilo limekuja baada ya wadau kuona kuwa, wapo baadhi ya watengenezaji mizinga ya kienyeji ambayo haina ubora, jambo ambalo linapunguza soko na ubora wa asali.

“Iwapo mizinga itatengenezwa bila kufuata vipimo sahihi vinavyotakiwa, kwa kawaida nyuki wengi huwa hawavutiwi na aina hiyo ya mizinga na badala yake mfugaji anaishia kuvuna asali kidogo sana na isiyo na ubora,” alisema Mdau  wa Misitu na nyuki, Stephen Msemwa.

Akaongeza kuwa, ipo haja kwa elimu zaidi kutolewa kwa wafugaji nyuki na watengenezaji mizinga juu ya jinsi gani mfugaji anaweza kuzalisha asali kwa wingi na yenye ubora sokoni.

“Kawaida nyuki huvutiwa kuweka makazi yao katika mizinga yenye  nafasi ya kutosha ambapo wanaweza kuruka kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kama itatokea mzinga una umbo dogo nyuki hao hukimbia mzinga huo,” alisema.

Akasema kupitita Wakala wa Misitu  (TFS) na nyuki nchini, wananchi wamekuwa wakipatiwa mafunzo kutoka kwa wataalalmu wa ufugaji nyuki  na pia kuwasambazia mizinga yenye ubora ambapo hadi tangu taasisi hiyo ianzishwe na  hadi kufikia mwaka 2015, jumla ya mizinga 14,076 ilisambazwa kwa wafugaji.

“Zoezi hili la usambazaji mizinga limesaidia siyo tu katika sekta ya ufugaji nyuki, bali hata katika uhifadhi wa misitu na hivyo kusaidia kuhifadhi mazingira,” alisema.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, alisikika akisema asali ya Tanzania ina ubora mzuri kulingana na tafiti zinazofanyika kila mwaka, hali ambayo imekuwa ikifanya ipate soko zuri kimataifa.

Alisema hayo wakati Bodi ya TFS na baadhi ya watendaji walipotembelea Kituo cha Ufugaji nyuki Ukimbu, kilichopo Manyoni, mkoani Singida.

Alisema utafiti unaofanyika ni pamoja na kuangalia ubora wa mazao ya nyuki na tafiti za masoko.

“Wataalamu wamegundua nyuki wa Tanzania hawana magonjwa, tumekuwa tukifanya utafiti kila mwaka na tunatoa sampuli 60 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kupeleka kwenye maabara nchini Ujerumani, lengo ni kuona kama zina kemikali zenye madhara kwa binadamu, lakini inaonesha asali ya Tanzania ni nzuri,” alisema.

Alisema kuna mashamba ya nyuki 92 yanayosimamiwa na TFS, ambayo ina mizinga inayokaribia 8,500, ambapo hutumika kwa ajili ya kuzalisha mazao ya nyuki, kufundishia na tafiti.

Alisema asali ya Tanzania ina soko zuri la kimataifa katika nchi za Ulaya, Amerika na Asia na wataendelea kuboresha soko la asali na la mazao mengine ya nyuki.

Akaongeza kuwa, pamoja na tafiti zinazoendelea, bado kuna mahitaji makubwa ya asali nje ya nchi, jambo la msingi ni kuangalia namna bora ya kuvuna mazao ya nyuki na  teknolojia bora ya uhifadhi.

Aliwataka wataalamu katika mashamba ya nyuki nchini, kuongeza nguvu katika ufugaji nyuki na kutafuta masoko na kuwafundisha wananchi namna bora ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Nta hutumika zaidi katika kutengeneza vipodozi, mishumaa, kutengenezea mizinga, kutengeneza dawa na pia kutengeneza dawa za kung’arisha mbao.

Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaonyesha kuwa, kati ya mwaka 1996 na 1997, Tanzania ilisafirisha jumla ya tani 395 za nta na tani milioni 2.46 za asali zilizokuwa na thamani ya Dola za Kimarekani 1,019,020 na Dola milioni 2.058 kwa pamoja.

Nchini Tanzania zipo ekari milioni 33.5 za misitu na uoto wa asili ambao una mazingira rafiki ya ufugaji nyuki.

Kwa kutambua umuhimu wa ufugaji nyuki kitaifa, kwa kujenga na kukuza uchumi, kuondoa umasikini katika jamii, kulinda na kutunza mazingira, taifa lilitayarisha na kupitisha sera ya ufugaji nyuki ya mwaka 1998, ambayo ndiyo inayotumika mpaka sasa.

Inakadiriwa hapa nchini kuna himaya za nyuki zipatazo milioni 10, ambazo zina uwezo wa kuzalisha tani za asali 140,000, yenye thamani ya dola za Marekani milioni 140, na kupatikana nta tani 10,000 zenye thamani ya dola za Marekani milioni 19.

Mahitaji ya sasa ya asali na nta yanazidi kupanuka kwa kasi kubwa, kutokana na wawekezaji wa viwanda kuhitaji asali kwa wingi, hasa wenye kutengeneza bidhaa za vyakula na madawa.

Takribani asilimia 50 ya asali inayozalishwa, inatumiwa hapa nchini katika kutengeneza pombe za kienyeji na mvinyo. Aidha, asilimia 10 inatumika katika viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu na pia kwenye viwanda vyenye tanuru za kuoka mikate na biskuti. Kiasi kidogo kinachobaki huuzwa nchi za jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Wanunuzi wakubwa wa nta ni Japan, Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya. Pamoja na kwamba asali na nta ya Tanzania vinatajwa kuwa na soko la uhakika na la kudumu, lakini uzalishaji wake ambao ni kwa asilimia 6.5 bado ni wa kiwango kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa eneo la nchi. Idadi ya mizinga na idadi ya wadau milioni mbili wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki, bado ni ndogo sana.

Wengine ni nchi za Umoja wa Ulaya na hasa Uingereza, Ujerumani na Uholanzi, wakifuatiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu – Emirate na Oman.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles