29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

DANGOTE KUONGOZA UUZAJI MCHELE DUNIANI

Na MWANDISHI WETU


KAMPUNI ya Dangote Group ya Nigeria, inayomiliki Dangote Cement nchini ya kule Mtwara, inategemewa kuwa msafirishaji mchele nje kinara duniani, pale atakapokamilisha miradi yake ya mpunga nchini mwake Nigeria.

Dangote ataifanya kwa mara ya kwanza Nigeria kujitegemea kwa chakula na hasa mchele ambao watu wengi hupenda kula nchini humo.

Dangote Group imepanga kuwekeza kiasi cha dola za marekani bilioni moja kwenye kilimo cha mpunga katika majimbo matatu nchini Nigeria na hivyo kutegemea kupata zaidi ya tani milioni tatu za mpunga na mchele tani milioni mbili.

Hali hiyo inatokana na sera nzuri za uwekezaji zinazotolewa na Serikali ya Nigeria kwa usafirishaji nje wa bidhaa ambazo zimefanya Dangote avutike nazo na kuamua kubadili mwelekeo wa biashara yake kutoka mwingizaji bidhaa toka nje (importer) na kuwa mpelekaji bidhaa nje (exporter) na hivyo kubadili mwenendo na modeli ya biashara  ya Aliko Dangote.

Hayo yalisemwa na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfdB), Akinwumi Adesina, kule Morocco kwenye mkutano wa Mo Ibrahim Forum kuwa ifikapo 2021 Dangote atakuwa muuzaji mkubwa nje wa mchele.

Mabadiliko hayo ya mtazamo wa Aliko Dangote yana tija kwake, nchi ya Nigeria na bara zima la Afrika na ni mfano wa kuigwa kwa maendeleo ya kweli ya uchumi wa bara hili.

Akizungumza kwenye jukwaa la Mo Ibrahim mjini Lagos wiki iliyopita, Adesina alidai kuwa Afrika lazima iweke kipaumbele kuhusu suala la kilimo na upatikanaji wa chakula, kwani usalama wake ni muhimu kwa maendeleo ya watu, kwani hukuza uchumi na kutoa ajira nyingi kwa watu.

Bara la Afrika alisisitiza lisonge mbele kwa mwenendo mzima wa kufanya kazi.

“Unapoagiza bidhaa kutoka nje maana yake unapeleka nje ajira ya watu wako na unapotengeneza bidhaa ndani ya nchi unaongeza thamani na hivyo kunufaisha nchi kwa kupata ongezeko la thamani kwenye mnyororo wa bei stahiki.

Dangote alianza kwa kuweka dola milioni 300 na baadaye kuziongeza hadi kufikia bilioni moja na hivyo kuleta mapinduzi yake ya kijani kwa kupanda mpunga, kuukoboa kiwandani na kuuza nje.

“Nilifurahia suala hilo kwa sababu kilimo cha mpunga na chakula kwa ujumla ni kitu bora kufanya na kina faida kwa wadau wote na hutoa ajira na kwa yote huwa kina faida kubwa kwa wanaoshughulika nacho na mazao yake siku zote yana soko,” alisema Adesina.

Mwaka 2013 Adesina alitajwa na Forbes Fortune kama ni Mtu wa Forbes wa Mwaka toka Afrika (Forbes Africa Person of the Year 2013) na Dangote alifuatia kupata  utambuzi huo kwa mwaka uliofuata, katika mwaka 2014.
Dangote Rice Limited imefanya mkataba wa pande tatu wa kutoa ajira 16,000 kwa wakulima wa nje wa mpunga (rice out growers) na Serikali ya Jimbo la Sokoto na kuanzisha skimu ya zao hili kule Sokoto. 

Mwenyekiti wa Dangote Rice Limited, Aliko Dangote, anasema aliamua kulima mpunga na kufanya biashara yake baada ya kutambua nia thabiti ya Serikali ya Shirikisho la Nigeria katika kufufua kilimo na kuwa uti wa mgongo wa uchumi na kupunguza uagizaji wa chakula kutoka nchi za nje kwa vile kinavyoweza kulimwa nchini humo.

Alisema kuwa Nigeria inakula tani za metriki milioni 6.5 ambazo hugharimu taifa hilo dola za Marekani bilioni mbili kila mwaka na inafurahisha sasa kuona serikali ina mwelekeo kisera ambao hutia moyo sekta binafsi kushiriki kwenye kilimo.

Alifichua kuwa, katika miaka mitatu ijayo watafikia tani milioni moja kutoka hekta 150,000 zitakazopandwa mpunga na baada ya hapo haitakuwapo  tena haja kuingiza mchele kutoka nje.

Skimu ya Dangote Rice Outgrowers imejizatiti kuzalisha ajira nyingi, kuongeza kipato cha wakulima wadogo na kuhakikisha usalama wa chakula katika nchi na kutoa mbegu bora za mpunga, mbolea na madawa ya kilimo na vilevile msaada wa kitaalamu  bora kwa wakulima wadogo.  Skimu hiyo itasaidia kubadilisha mwenendo wa uchumi, kupunguza umasikini  na kupunguza  kiasi cha fedha za kuagiza chakula nje na kuwa kituo kimoja cha kushughulika masuala yote ya ongezeko la thamani kuhusu mpunga na mchele.

Wakati huohuo, Dangote Flour Mills imeanza kupata  faida na kuonesha  kwenye hesabu zake kupata faida ya  Naira bilioni 11.82 kabla  ya kodi kutokana na taarifa zilizotolewa na Nigerian Stock Exchange  (NSE) kwa mwaka unaoishia Desemba 31, 2016, baada ya miaka minne ya kupata hasara.

Dangote Flour Mills inahusu viwanda vya Dangote Flour, Dangote Pasta na Dangote Noodles, ambayo iliuzwa kwa Tiger Branded Consumer Goods, halafu ikarudishwa tena kwenye himaya ya Dangote na kuwekewa mikakati mipya ya muundo na mwenendo na hivyo kuanza kupata faida nono. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles