Na KOKU DAVID
KODI ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni kodi ya mlaji inayotozwa kwenye bidhaa na huduma zinazozalishwa hapa nchini na pia kwenye bidhaa au huduma zinazoingia Tanzania Bara kutoka nje ya nchi.
Kodi hii hutozwa kuanzia ngazi ya uzalishaji wa bidhaa, uuzaji wa jumla, reja reja hadi bidhaa inapomfikia mlaji wa mwisho.
Kwa mujibu wa sheria za kodi, mlipaji wa kodi hii ni mlaji, mtumiaji wa bidhaa au huduma, kwa maana ya yule mtu anayeitumia bidhaa au huduma akiwa wa mwisho.
Mfanyabiashara anatakiwa kujisajili na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ikiwa ni pamoja na kupata cheti cha usajili anapokuwa amefikia kiwango cha mauzo ya Sh milioni 100 ya bidhaa zinazotozwa VAT kwa mwaka na kwamba kiwango cha asilimia 18 ndicho kinachotumika kwa sasa.
Kwa upande wa Kodi ya Mapato, hii inalipwa kulingana na mapato anayopata mtu kutoka kwenye biashara yake.
Kulingana na sheria ya kodi, viwango vya kodi ya mapato kwa wafanyabiashara vimegawanyika katika sehemu tatu, ambapo sehemu ya kwanza ni viwango vinavyowahusu wafanyabiashara binafsi na wadogo ambao mauzo yao hayazidi Sh milioni 20 kwa mwaka.
Kiwango cha pili cha kodi kinawahusisha wafanyabiashara binafsi ambao viwango vya kodi hutegemea faida inayopatikana kulingana na kumbukumbu za biashara na hesabu za mizania zilizokaguliwa.
Katika kiwango cha tatu cha kodi hii ya mapato kinayahusisha makampuni, mashirika, vilabu, ushirika na taasisi nyingine ambazo kiwango maalumu hutozwa kwenye faida.
Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali za kijamii na kiuchumi, Tanzania haina utaratibu wa kutoza VAT kwenye kila kitu.
Kuna baadhi ya bidhaa hutozwa VAT kwa kiwango cha asilimia sifuri na nyingine zimesamehewa kabisa ambazo ni vyakula ambavyo havijasindikwa.
Huduma nyingine zilizosamehewa kulipia VAT ni mayai, dawa za binadamu zilizotajwa na Wizara ya Afya, magazeti, majarida na vitabu, mbolea na dawa za kilimo, huduma za tiba kama meno na magonjwa mbalimbali, usafirishaji wa abiria kwa kutumia basi, treni, ndege, meli na vyombo vingine vya usafiri.
Lakini kwa upande wa biashara ya teksi, gari za kukodi, boti na ndege za kukodi, huduma za elimu zinazotolewa na taasisi yoyote iliyosajiliwa na serikali, uuzaji au upangishaji wa nyumba za kuishi au ardhi ikiwa ni pamoja na huduma za mazishi hazina msamaha.
Hivyo, kutokana na hali hiyo, kwa mtu au kampuni inayotaka kuanza biashara, ni lazima ajue taratibu au sheria za kodi ili ziweze kuzingatiwa na kufuatwa.
Kwa wale wanaotaka kuanzisha biashara binafsi, hatua ya kwanza ni ya usajili kwa ajili ya kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).
Katika usajili wa biashara ya makampuni, ni lazima waanzishaji wapate cheti cha usajili kutoka kwa Msajili wa Makampuni (BRELA).
Ikumbukwe kuwa, katika harakati za kutaka kufungua kampuni au biashara, ni muhimu mlipakodi kukumbuka namba yake ya utambulisho kila anapokwenda katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa shughuli mbalimbali za ukadiriaji na kulipa kodi, pia namba hiyo inarahisisha kupatikana kwa jalada lake la kodi.
Baada ya kupata TIN, mfanyabiashara (binafsi au kampuni) atatakiwa kufuata taratibu zote za maombi ya leseni ambayo inapatikana katika ofisi ya biashara ya jiji, manispaa, mji au ofisi ya halimashauri ya wilaya au Wizara ya Viwanda na Biashara.
Meneja wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Gabriel Mwangosi, anasema baada ya taratibu za uanzishaji wa biashara au kampuni kukamilika, sheria zote za kodi zinawataka wafanyabiashara kuhakikisha wanazingatia suala la utunzaji wa kumbukumbu sahihi za biashara kupitia mfumo wa utoaji wa risiti kwa kutumia mashine za kodi za kielektroniki (EFDs).
Anasema pamoja na kwamba ni matakwa ya sheria, pia utunzaji wa kumbukumbu kwa njia hiyo una faida mbalimbali kwa mfanyabiashara, ikiwa ni pamoja na kuwezesha kufanya makadirio ya kodi ambayo ni sahihi.