23.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

BAKHRESA AWEKEZA HOTELI KIFAHARI Z’BAR

*Ni ya Mtoni Marine, kuwa kubwa EAC


Na BAKARI KIMWANGA-ALIYEKUWA ZANZIBAR

SEKTA ya Utalii ni moja ya nguzo muhimu kwa uchumi wa Visiwa vya  Zanzibar na kutokana na hali hiyo zimekuwa zikichukualia hatua mbalimbali ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa ambao utachochea uchumi wa visiwa hivyo.

Kutokana na hali hiyo, utalii Zanzibar umekuwa ukipewa nafasi kubwa katika mipango ya Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Jamii, ambapo imefanikiwa kuchangia kati ya asilimia 25 hadi 27 ya Pato la Taifa.

Sekta hiyo imekuwa ikichangia asilimia 70 ya mapato ya fedha za kigeni ambapo hiyo ni dalili ya ukuaji wa uchumi, ambao ulikuwa wa wastani wa chini ya asilimia 15.

Hatua hiyo inamfanya mfanyabiashara bilionea nchini, Said Salim Bakhresa, kuamua kujikita kwa undani na kubadili mandhari na mwonekano wa Kisiwa cha Unguja kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa hoteli kubwa ya kisasa yenye hadhi ya nyota tano visiwani humo.

Bakhresa kwa kuona fursa hiyo, ameamua kuwekeza katika miundombinu kwa ajili ya shughuli za utalii kwa kujenga miradi miwili mikubwa ya miundombinu ambayo sasa ipo mbioni kufikia ukingoni.

Mradi huo mkubwa ni wa kimataifa wa ujenzi wa kisiwa cha Kitalii ambacho kitatengenezwa kwa mfumo wa ufukiaji Bahari katika eneo la Hoteli ya Utalii iliyopo Mtoni Marine, kaskazini Magharibi ya Mji wa Zanzibar. Mradi huo utahamisha ekari 30 za bahari kujenga kisiwa cha kisasa mfano wa kile kilichonyika Dubai.

Hata hivyo, gharama kamili za mradi huo bado kujulikana, lakini zitakuwa ni zaidi ya dola milioni 500 hadi kukamilika kwake mapema mwaka huu.

Mradi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Bakhresa Group, utahusisha ujenzi wa hoteli ya kimataifa ya ghorofa tano, ambapo pia unahusisha utengenezaji wa eneo la wazi la mapumziko (Public Beach) pamoja na kutengeneza Kisiwa cha Mji mpya.

Hivi karibuni MTANZANIA ilikuwa ni moja ya ujumbe wa wanahabari waliotembelea mradi wa ujenzi wa hoteli ya kisasa inayotarajiwa kuwa katika ukanda wa Afrika Mashariki wa Mtoni- Marine Kisiwani Unguja.

Hoteli hiyo kubwa ya kitalii itakayokuwa ya aina yake inatarajiwa kuwa na eneo la kupumzikia, michezo kwa watoto, pamoja na sehemu maalumu kwa ajili ya familia kwa mapumziko ya siku au hata kulala hotelini hapo.

Akizungumzia mradi wa Mtoni Marine, Meneja mradi Karama Awadh, anasema: “Mradi umegawanyika katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni ujenzi wa vyumba vya kulala wageni (hoteli), huku sehemu ya pili ni uhamishaji maji ya bahari, (Land reclamation),” anasema.

Awadh anasema upande wa mradi wa hoteli hiyo itakuwa na vyumba 106 vinavyojengwa, ambapo sita kati yao vitakuwa na hadhi ya makazi ya Rais (Presidential Suites).

Alizungumzia upande wa uhamishaji maji kwenye bahari kwenye eneo lenye urefu wa mita 450 na upana wa mita 250 kama njia ya kuongeza ardhi kwa ajili ya mradi huo wa kisasa ambayo utavifanya visiwani  vya Zanzibar kuwa na mwonekano wa nchi za Ulaya.

Uwekezaji huo wa kimataifa wa kisiwa cha utalii, kinatengenezwa kwa mfumo wa ufukiaji bahari, eneo la Mtoni Kaskazini Magharibi mwa mji wa Unguja.

Anasema wazo hilo lilitokana na mwenyewe Mwenyekiti wa Kampuni ya SSB, Said Salim Bakhresa, ambaye alianza kutaka kulibadili eneo hili.

“Eneo hilo ni hilo lililojazwa mchanga, ni kwa ajili ya watu kupumzika, patakuwepo na michezo ya maji (water park), watu wa kila aina wakiwa na familia zao wapatao 3,500 watahudumiwa kila siku kwa wakati mmoja, sehemu ya Marine itakuwa na huduma za kuegesha boti 30 zenye urefu wa mita 10,” anasema Awadh.

Anasema hoteli hiyo itakuwa na barabara za juu (Flyover) kwenda katika eneo la mapokezi.

Kauli ya Bakhresa

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bakhresa Group, Said Salim Bakhresa, anasema kwamba ujenzi wa mradi huo ni muhimu kwa uchumi wa nchi na utasaidia mapato ya Taifa pamoja na kutoa ajira kubwa kwa vijana Wazalendo Zanzibar.

“Mfumo wa ufukiaji Bahari kwa ajili ya kuanzisha miradi ya kiuchumi ni mfumo unaotumiwa na mataifa mbalimbali duniani, ambapo kwa Afrika mradi kama  huu tayari umeanza kutumiwa katika Kisiwa cha Seychelles,” anasema.

Anasema eneo hilo la kuhamisha bahari litakuwa na sehemu ya kupaki boti ambapo pia kutakuwa na barabara maalumu za lami pamoja na ufukwe, ambapo watu wataogelea.

Ujenzi ulivyo

Mhandisi wa Mradi huo, Ahmed Shamsi, anasema kuwa, chombo maalumu kinachotumika kwa kazi ya uchimbaji wa mchanga baharini kina uwezo wa kunyonya na kusafirisha mchanga kutoka ndani ya bahari sambamba na kukata majabali.

Kazi hii inafanyika kwa saa 12 kila siku ambapo takwimu zinaonyesha wazi kwamba uchimbaji huo wa mchanga unaokwenda zaidi ya mita 15 chini ya bahari unafikia tani 600 za mchanga kwa saa moja, ambapo kazi hiyo ilianza Novemba mwaka jana na sasa ipo katika hatua za mwisho kukamilika kwa mradi huo.

Kauli ya Serikali

Akizungumzia mradi huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,  Balozi Seif Ali Iddi, ameupongeza uongozi wa Bakhresa Group kwa uamuzi iliochukua wa kuanzisha mradi huo mkubwa wa kimataifa.

Balozi Seif anasema kukamilika kwa mradi huo mkubwa ambao nchi za Afrika zilizoea kuona kwenye mataifa makubwa, sasa utasaidia kuitangaza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kama chemchemi ya utalii kimataifa.

“Ninapenda kuhakikishia uongozi wa Bakhresa Group kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila msaada unaohitajika katika kuona mradi huo unafikia malengo uliojipangia kwa masilahi ya nchi yetu na watu wake,” anasema Balozi Seif.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,293FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles