Na RAMADHANI MASENGA
BONGO Muvi imekwisha sasa. Hakuna anayeshtuka kusikia Ray ama Riyama katoa Muvi mpya. Bongo Muvi ipo ipo tu. imebaki kuwa kama Panadol. Haimalizi tatizo bali inatuliza tu. Mtu akitaka kuangalia muvi za nyumbani anaangalia ila anakuwa hajamalizwa kiu yake.
Hakuna ubunifu wala viwango. Hakuna vipaji halisi wala kitu cha kushawishi kuangalia. Juzi wameandamana. Kabla ya kufanya hivyo walimfuata mkuu wa mkoa na kumlilia shida yao.
Eti walisema adui yao namba moja ni muvi za Kikorea na Kifilipino. Kichekesho hiki. Mkuu wa mkoa akawasikiliza. Huenda hana ufahamu wa kutosha kuhusiana na muvi za Kibongo na Kikorea.
Huenda aliwasikiliza kwa sababu za kisiasa pia. Ila ukweli ni kwamba hawakuwa na hoja ya msingi. Bongo Muvi imepauka sio kwa ujio wa muvi za Kikorea.
Ukurupukaji wao pamoja na kujaa mamluki katika sanaa yao ndiyo kumeua Bongo Muvi. Zamani Bongo Muvi ilipokuwa juu kila mtu maarufu alijidai msanii. Tulimuona Jokate, Lisa Jensen mpaka waimba Injili waliigiza.
Leo kiko wapi? Nina hakika Lisa Jensen hata hataki kusikia habari za Bongo Muvi. Hawa hasa ndiyo walioua soko la filamu.
Hawakuwa wakiigiza kwa kufuata miiko na desturi za maigizo badala yake walileta ubishoo. Kama kulikuwa kuna haja sana ya kuandamana, basi walifaa kuandamana kwenda kwa akina Ray na Wema.
Ray alileta wazugaji katika muvi na Wema alikuwa mzugaji katika filamu. Hawa kwa kiasi kikubwa ndiyo waliochimba kaburi la Bongo Muvi na wala sio muvi za Kikorea.
Maigizo yalipoteza thamani na heshima. Kila mmoja akawa muigizaji na muongozaji. Kina Sultani Tamba wakasahauliwa, kina marehemu George Tyson hawakuthaminiwa.
Sasa kwanini Bongo Muvi iendelee wakati ilijaa wapiga dili kibao? Bongo Muvi isingeweza kuendelea kama hata Aunt Ezekiel alikuwa muongozaji na mtunzi wa stori.
Anti ni hatari kwa kuigiza nakubali. Ila hana kitu katika kutunga stori. Kichwa ambacho kila siku kiko katika kumbi za starehe hakiwezi kuwa na utulivu wa kutosha wa kuandika stori kali kama zitungwazo na kina Sultani Tamba au mzee Kasim Twalibu ‘Teacher’.
Kina Aunt na Hemed ndiyo walioua Bongo Muvi. Kama Hemed aliweza kuhojiwa na kusema mafanikio yake makubwa katika kuigiza ni kuwa na mademu wengi. Wewe unategemea Bongo Muvi ingekuwa kwa muujiza gani?
Ilibidi tu Bongo Muvi ifikie mahali iwe vichekesho kama mastaa wake ni kina Wema na Anti Lulu. Kitu chochote kinapokuwa na watu ambao hawajui thamani yake ni lazima kiparaganyike.
Bongo Muvi imenajisiwa na hatimaye kupoteza thamani yake na hawa wasanii mvuto na skendo. Na baada ya kuona wameiharibu wote wameikimbia na kuwaachia kina Omary Clyton na Selemani Masenga wapambane upya.
Badala ya kujificha katika kivuli cha muvi za Kikorea na Kifilipino, Bongo Muvi inabidi wakubli ukweli. Ukweli wa kuwa wao ndio waliochoma sindano ya sumu katika mwili wa Bongo Muvi baada ya kuanza kuwaingiza mamisi na wanamitindio kwa fujo.
Watu ambao kwao sanaa ilimaanisha kutafuta umaarufu na kuwa na wingi wa skendo. Hakuna kinachoweza kuirudisha Bongo Muvi katika hadhi yake kama wenyewe wataacha kujitafakari na kujua walipokosea.
Kuandamana na kupinga uwepo wa muvi za Kikorea ni kujipa majibu mepesi katika maswali magumu. Wanatakiwa kukabiliana na ukweli halisi kuwa sanaa yao imefubaa kwa kuwa haina tena ubunifu na umakini watu wanaouhitaji.