29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 21, 2021

ALI KIBA, DIAMOND PLATNUMZ MAJUKUMU YAWAWEKA MBALI NA UZALENDO

NA CHRISTOPHER MSEKENA

“Kiba na Diamond wameshindwa kuonesha uzalendo kwa Serengeti Boys, wamegoma kuimba wimbo wa hamasa licha kuwepo kamati ya hamasa. Inasikitisha

Hayo ni maneno ya mtangazaji mahiri wa michezo kutoka kituo cha utangazaji E Fm, Maulid Kitenge (Mshambuliaji) aliyoyatoa siku ya Alhamisi wiki hii kupitia ukurasa wake wa Twitter akionyesha kusikitishwa na mrejesho hasi wa wakali wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz na Ali Kiba katika kuisapoti timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys.

Mahasimu hao waliteuliwa na aliyekuwa waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye katika orodha ya watu kumi ili kuleta hamasa na kuisapoti timu hiyo ya vijana kwenye safari yao kuelekea fainali za AFCON nchini Gabon mpaka kombe la dunia nchini Gabon.

Kamati hiyo iliyojaa watu wenye ushawishi mkubwa kutoka sekta mbalimbali, upande wa burudani walichanguliwa Diamond Platnumz na Ali Kiba, lengo likiwa ni kutumia ushawishi walionao kusogeza mafanikio ya timu hiyo pekee Tanzania inayofanya vyema kwenye soka.

Bila shaka kila mmoja alitaka kufahamu mtindo gani watakaoutumia wawili hawa kufanya kazi ndani ya kamati moja na zaidi macho na masikio ya wengi yalitamani kuona na kusikia kolabo ya Diamond na Ali Kiba wakiwa wenyewe (man to man).

Tujikumbushe hii

Diamond na Ali Kiba wamewahi kukutana kwenye nyimbo mbili ambazo ni ule uliotoka mwaka 2011 kwa ajili ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika pamoja na ule uliotoka mwaka 2014 uliohusu Muungano wa Tanganyika.

Baada ya hapo kuna wimbo wa kuchangia matibabu ya msanii wa filamu marehemu Sajuki ambapo Ali Kiba alikuwepo ila Diamond hakuwepo.

Pia katika kolabo nyingine ile iliyowakutanisha wasanii wa mkoa wa Kigoma, Diamond Platnumz alikuwepo ila Ali Kiba hakuwepo kitu kilichoongeza shauku ya mashabiki wanaotaka kuwasikia wawili hawa katika wimbo mmoja.

Ubize wayeyusha uzalendo

Baada ya kuwekwa kwenye kamati hiyo, Diamond Platnumz na Ali Kiba wamekuwa na michakato mbalimbali kwa ajili ya kusimamisha biashara yao ya muziki, majukumu yaliyowaweka kando na uzalendo wa kuhamasisha watu kuishabikia na kuchangia timu yao ya Taifa.

Ali Kiba na ziara ndefu..

Kwa muda mrefu sasa amekuwa akifanya ziara yake kwenye mataifa mbalimbali Duniani. Alianza Afrika Kusini mwezi Februari mwaka huu ambapo alitumbuiza kwenye majiji kadhaa ya nchi hiyo.

Hakuishia hapo kwani Machi mwaka huu alitua Marekani na takribani mwezi mzima alikuwa akitmbuiza kwenye miji kadhaa ya nchi hiyo na mwezi huu wa nne mpaka Mei atakuwa Uingereza akiendelea na ziara yake ndefu ya kimuziki.

Yupo bize kiasi kwamba ni ngumu kufanya kazi ya kizalendo ya kuhamasisha kupitia uimbaji ili timu hiyo ya Taifa ifanye vyema kwenye safari yake hiyo.

Diamond Platnumz na wasafi.com, manukato

Huyu jamaa hana shoo nyingi kivile ila biashara zake za muziki zinaamfanya asipate wasaa wa kufanya kile kilichokusudiwa na kamati ya uhamasishaji.

Utakumbuka mwezi Machi mwaka huu mkali huyu wa Bongo Fleva aliweka rekodi ya kuzindua tovuti ya wasafi.com kwa ajili ya kuuza nyimbo za wasanii mbalimbali.

Hali kadharika wiki iliyopita alitambulisha manukato yake, Chibu Perfume na bidhaa zake zote hizo yaani unyunyu na wasafi.com zilihitaji uwepo wake wa karibu uli uweze kwenda vizuri.

Kwa hiyo unaweza kuona mbali na uhasimu wa Ali Kiba na Diamond Platnumz, majukumu waliyonayo yamewafanya wakae mbali na uzalendo wa uhamasishaji wa timu ya Taifa.

Kikubwa ni kila mmoja kutambua kuwa ushindi wa Serengeti Boys ni wetu sote kwa hiyo tuichangie timu kama tunavyoelekezwa kwenye matangazo mbalimbali ila upande wa uhamasishaji upande wa muziki tusubiri tuone mwisho wake ni nini kama wawili hawa watafanya chochote kitu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,682FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles