29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

EMMANUEL MACRON: MGOMBEA URAIS UFARANSA ALIYEPITWA MIAKA 25 NA MKEWE

Na Markus Mpangala


UCHAGUZI wa Ufaransa raundi ya pili utafanyika Mei 7, mwaka huu. Washindani wakubwa watakuwa Emmanuel Macron na Marie Le Pen. Jina la Macron ndilo limevutia zaidi vichwa vya habari vya Ufaransa na Ulaya kwa ujumla.

Dunia nzima sasa inamfahamu mwanasiasa huyo kuwa ndiye anatarajiwa kushinda uchaguzi mkuu wa urais ifikapo Mei 7 kutokana na takwimu kuonyesha anayo nafasi ya kumshinda Marine Le Pen.

Hata hivyo, lipo jambo linalohusu maisha binafsi ya Emmanuel Macron, nalo ni suala la ndoa yake. Mke wake ana miaka 64, huku Macron akiwa na miaka 39.

Wanandoa hao wana tofauti ya miaka 25 ya kuzaliwa kwao, lakini haikuwa kigezo cha kushindwa kuoana.

Hii ni ndoa inayosisimua na kushangaza watu mbalimbali kwa sababu inamhusisha mwanafunzi na mwalimu wake.

Kitaalumu Brigitte Trogneux yaani mke wa Emmanuel Macron ni mwalimu. Mwanamama huyo anabainisha kuwa alishuhudia kijana Emmanuel Macron akimpa ahadi ya kuoana wakati akiwa na miaka 17.

Alishangaa kuona kijana mwenye umri wa miaka 17 anataka kumuoa mwalimu wake, ambaye amemzidi miaka mingi ya kuzaliwa.

Kwa sasa Brigitte Trogneux, ana umri wa miaka 64, ni mwalimu wa tamthilia aliyemfundisha Emmanuel Macron akiwa shuleni.

Lakini sasa Macron na Brigitte ni wanandoa ambao wametabiriwa kuingia ikulu ifikapo Mei 7 mwaka huu, ikiwa na maana Emmanuel anatarajiwa kuwa rais wa Ufaransa, huku Brigitte kuwa ‘First Lady’.

Brigitte ameshuhudia mumewe akiongoza kwenye duru la kwanza la kinyang’anyiro cha urais wa Ufaransa dhidi ya kiongozi wa chama cha National Front, Marine Le Pen.

Macron alipata asilimia 23.75, ambapo mpinzani wake Marine Le Pen alipata asilimia 21.53. yote hayo yamekuwa gumzo jepesi kuliko lile linalohusu maisha ya Macron.

Ikulu ya Elysee inawasubiri Macron na mkewe Trogneux, ambapo Macron atakuwa Rais kijana kuliko wote katika historia ya Ufaransa.

ILIVYOKUWA

Macron akiwa na miaka 15 tangu azaliwe ndipo alikutana na Brigitte kama mwalimu wake. Baadaye Macron alimpa ahadi Brigitte kuwa atamuoa mwalimu huyo.

“Akiwa na umri wa miaka 17, Emmanuel aliniambia, chochote unachofanya, nakuahidi nitakuoa wewe Brigitte,” alisema Trogneux alipozungumza na jarida la Paris Match.

Uhusiano wa kimapenzi kati ya wawili hao ulianza pale Emmanuel Macron alipopewa jaribio la kuigiza tamthilia fupi iliyoandaliwa na mwalimu wake Brigitte Trogneux. Kipindi hicho Emmanuel alikuwa na miaka 18 tu na mwanafunzi wa Shule ya Shirika la Jesuit iliyopo Amiens, kaskazini mwa Ufaransa.

Mwalimu huyo ndiye alikuwa msimamizi wa jaribio la kuigiza tamthilia hiyo kwenye ukumbi wa shule.

Aidha, inaelezwa kuwa Macron alipendelea mno fasihi ambapo alitaka kuwa mwandishi wa riwaya na vitabu.

Baadaye Macron alihama kutoka Amiens kwenda jijini Paris katika mwaka wake wa mwisho wa kuhitimu sekondari.

“Kwa kipindi hicho tulipigiana sana simu. Tuliongea mengi kwa muda mrefu, tulitumia muda mwingi kuzungumza kwa simu, yaani masaa mengi tulipoteza kwenye simu,” alisema Brigitte.

Mwalimu huyo aliongeza kwa kusema, “Kidogo kidogo, alifuzu vikwazo nilivyomwekea hata sikuamini. Tena kwa utulivu na uvumilivu. Hakuwa mtoto tena. Alikuwa na mahusiano ya kimapenzi kama mtu mzima yeyote,”

Baadaye Brigitte alihamia Paris kuungana na Emmanuel Macron. Uamuzi wa kuhamia Paris uliambatana na kuachana na mumewe. Hii ina maana Brigitte alilazimika kuvunja ndoa yake ili aolewe na mwanafunzi wake.

Macron na Brigitte walifunga ndoa mwaka 2007, ingawaje hakutumia jina la mumewe badala yake alichagua kubaki na lake.

“Siwezi kumficha kitu. Yuko hapa, yeye ni maisha yangu. Daima yuko nami kwa hilo,” alisema Emmanuel Macron alipohojiwa wiki hii na French TV.

Katika hotuba yake mwezi uliopita, wanandoa hao walibusiana hadharani wakiwa ukumbini, ndipo Macron aliwaambia wafuasi wake, “Ninamhusudu kupindukia Brigitte, kwasababu amenifanya niwe mtu mwenye hadhi na heshima ninavyoonekana leo,”

Kisha alimgeukia mkewe na kumwambia, “Usikae nyuma yangu. Tukichaguliwa, hakuna kubaki nyuma. Tukichaguliwa, atakuwa na majukumu kuitumikia Ufaransa,”

Aidha, baadaye Macron alisoma masuala ya falsafa katika Chuo Kikuu cha Paris Nanterre.

Amewahi kuwa mshauri wa masuala ya uchumi wa Rais Francois Hollande, na baadaye waziri wa uchumi kwa miaka miwili.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika mbali ya  habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles