24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

CONSOLATHA NA MARIA: MAPACHA WALIOUNGANA WENYE NDOTO YA KUWA WATAALAMU WA KOMPYUTA

*Ulemavu ulisababisha wafichwe

*Hupata alama sawa darasani bila kuigiziana

*Wana hisia tofauti, mmoja akila samaki hudhurika


NA FRANCIS GODWIN-IRINGA

MUNGU ana maajabu yake. Mungu ana makusudi yake. Ndivyo unavyoweza kusema ukitafakari uumbaji wa Mungu kwa viumbe vyake wakiwamo binadamu.

Makusudi hayo yanajidhihirisha katika muujiza wa watoto mapacha Consolata na Maria Mwakikuti (26), waliozaliwa wakiwa wameungana kiwiliwili, ambao sasa wana ndoto ya kujiunga chuo kikuu.
 

Mapacha wengi wanaozaliwa wakiwa wameungana huripotiwa kufariki muda mfupi baada ya kuzaliwa au kufanyiwa upasuaji ili kuwatenganisha japo wapo wengine ambao huishi.

Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia, kukua kwa mitandao ya kijamii kuzaliwa kwao kungekuwa gumzo katika vyombo vya habari.

Lakini kwao haikuwa hivyo kutokana na ukweli kwamba teknolojia haikuwa kwa kiwango cha leo lakini pia vyombo ya habari yaani magazeti, televisheni na radio havikunasa tukio la kuzaliwa kwao katika Hospitali ya Misheni ya Ikonda mwaka 1996.

Ulemavu wao ulisababisha wafichwe na kwa wakati huo habari za kuzaliwa kwao hazikuenea sana.

Walianza kujulikana wakati walipojiunga na elimu ya msingi wakati wamisheni walipolazimika kuwahamishia watoto hao kwa mama mlezi wao na kwa wakati huo, walitafutwa walezi wawili.

Wakiwa na miaka mitatu, baba yao Alfred Mwakikuti alifariki dunia na walipofikia darasa la pili mwaka 2002, mama yao pia alifariki dunia hivyo kuwaacha wakiwa yatima.

Mama yao mlezi anasema licha ya kuwa analipwa kiasi kidogo cha mshahara kutoka misheni kwa ajili ya kuwalea, bado maisha yao ni magumu sana na analazimika kulima ili aweze kukidhi mahitaji yao.

Mapacha hao Consolata na Maria wanaoishi Ikonda wilayani Makete, Mkoa wa Njombe, si tu Mungu ameruhusu waendelee kuishi bali pia kuwabariki kuonyesha maajabu yake kwa kuwapa mafanikio na kufanya vizuri kwenye masomo yao.
 

Mapacha hao walipata elimu yao ya msingi kijijini hapo na kufanikiwa kufaulu vizuri kabla ya mwaka 2011 kuchukuliwa kwa malezi na wamisionari na kupelekwa wilayani Kilolo kwa ajili ya kuwalea zaidi. 

Mapacha hao kwa sasa wamehitimu  kidato cha  sita mwaka huu katika Shule ya Sekondari ya Udzungwa na wanalelewa na kituo cha Nyota ya Asubuhi Kidabaga, wilayani Kilolo Mkoa wa  Iringa.

Wanasema ndoto yao kubwa  pindi watakapomaliza chuo ni kuwa  wataalamu wa kompyuta.

Awali, baada ya kumaliza elimu ya msingi walijiunga na Shule ya Sekondari Nyota ya Asubuhi  baada ya walezi wao kukataa wasijiunge na shule ya sekondari ya Jangwani walikokuwa wamepangiwa baada ya matokeo yao kutoka.


“Siku tuliposikia tumefaulu hatukulala kwa furaha, tuliruka na kumshukuru Mungu kwani hatukuamini kama tungeweza kufaulu kutokana na kusomea katika mazingira magumu.

“Hatukuwa na kiti cha kukalia darasani, siku zote tulikalia kibaiskeli ambacho hakitutoshi na kadri siku zilivyokuwa zikisogea ndivyo kilivyokuwa kikituumiza kwa kuwa ni kidogo na sisi tunakua,” anasema Consolata.

Mabinti hao wanasema wakiwa wanasoma, kila siku asubuhi rafiki zao waliwapitia ili kuwapa msaada wa kusukuma baiskeli yao hadi shuleni. Muda wa mapumziko waliwarejesha nyumbani kwao kwa ajili ya kujisaidia.

Wanasema utaratibu huo ulidumu muda wote wakiwa shuleni ambapo hawasiti kuwashukuru wenzao kwa upendo huo.

Mapacha hao walipata alama zinazolingana kwenye mtihani wao wao mwisho, kila mmoja akipata alama 151, lakini kinachothibitisha kuwa hawakutazamiana wala kusaidiana kwenye mtihani ni tofauti ya alama walizopata kwenye baadhi ya masomo.

Katika somo la maarifa ya jamii, Consolata alipata alama 29 na Maria alipata alama 25, wakati kwenye somo la sayansi Maria amemzidi Consolata kwa kupata alama 31 dhidi ya 29 na hali ni kama hiyo kwenye somo la Kiingereza ambalo Maria amepata alama 36 na kumzidi Consolata aliyepata alama 34.
 

Consolata na Maria ambao kwa  sasa wamehitimu kidacho cha sita wana shauku ndoto ya kutimiza ndoto zao kielimu kwa kuendelea na masomo ya  chuo kikuu.

Wanasema hawajawahi kufeli masomo na wamekuwa wakipishana  iwapo mmoja atashika namba moja basi mwingine hushika atakuwa wa pili  ambapo pia wamekuwa wakishindana hivyo  hadi wanahitimu kidato cha sita.
 

Japo wameungana, lakini kila mmoja ana hisia zake. Juhudi zao zinazolingana katika masomo na tabia zao hazikuwafanya watu wa aina moja licha ya kuungana tumbo Kila mmoja ana hisia zake na ana vitu anavyopendelea mfano  Maria ni mcheshi zaidi ya Consolata hachagui chakula lakini Maria akila samaki anasumbuliwa na tumbo.

Lakini kama mmoja akijisikia kwenda kulala, basi mwenzake pia atalazimika kulala kwa kuwa wameungana tumboni. Maumbile yao yanawalazimu mapacha hawa wapendane na kusaidiana.
 

“Maria akiumwa inanibidi niwe mpole, nitulie kwa sababu nikimfanyia fujo nitamuumiza, akitaka kulala tunaenda wote na kama litamuuma tumbo la kuharisha basi tutaenda wote uani, hatujawahi kugombana, tunapendana sana,” anasema Consolata.

Kwa upande wake Maria anasema maisha yao ya shule yalikuwa mazuri kutokana na ukweli kwamba, watu wengi waliwapenda hivyo hawakujiona tofauti.
 

“Tunahitaji shule ambayo itaweza kutusaidia, kama kuna uwezekano wa kupewa nyumba tutashukuru kwani hali yetu ilivyo ni tofauti na wenzetu,” ansema.

Walimu wao wanashauri, ikiwa Serikali itaamua kuwasomesha, basi ihakikishe kuwa mama yao mlezi anakuwa nao karibu baada ya kuwawezesha kufikia hapo walipo sasa.
 

Katika maisha yao ya kusoma, kila mmoja alikuwa na madaftari yake na wakati wa kufanya mazoezi au kuandika kazi wanazopewa, mmoja huanza kuandika, akimaliza na mwingine huandika.
 

“Wala hatupati shida tumezoea, kila mmoja anafanya kazi yake, mimi naandika kwa mkono wa kushoto na Maria anaandika kwa mkono wa kulia,” anasema Consolata, ambaye anaonekana kuwa mchangamfu zaidi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilolo,  Asia Abdalah na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Rita Kabati ni miongoni wa viongozi  waliopata kuwatembelea kwa  nyakati tofauti  watoto  hao.

Mkuu huyo wa Wilaya anasema serikali inawathamini na inaendelea kuwapenda hivyo kama mkuu wa wilaya ataendelea kufika kuwasalimia na kuwasaidia. 

“Nimefurahi sana kuwaona mkiwa na furaha kubwa na mnafanya vema katika msomo yenu kwa kufanya vizuri katika masomo yenu ya kidato cha nne na sasa kidato cha sita, hakika mnaonyesha matumaini makubwa ya kwenda chuo kikuu kutokana na jitihada zenu darasani kwa kuwa mnafanya vizuri katika masomo yenu ya kidato cha sita sasa,” anasema Asia. 

Hata hivyo, mapacha hao wanaomba serikali kuendelea kufanya kazi nzuri kwa wananchi wake kwa kasi hiyo laikini pia wanapenda kuona serikali ikiendelea kuboresha elimu mashuleni kwa kutatua changamoto ya vitabu vya sayansi ili kuzalisha wasomi zaidi wa masomo ya Sayansi nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles