25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KILAINI: HATA SISI TUNAHOFIA KUTEKWA

Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini

Na EVANS MAGEGE,

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini, amesema mwenendo wa matukio ya kuteka na kutesa watu yaliyoripotiwa kutokea hivi karibuni  yanawatia hofu viongozi wa dini.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili katikati ya wiki hii alipoombwa kutoa mtazamo wake juu ya tukio la kutekwa kwa Msanii wa Bongo Fleva, Roma Mkatoliki na wenzake waliotekwa hivi karibuni katika Studio za Tongwe Records zilizopo Masaki, Dar es Salaam na kupelekwa kusikojulikana kwa muda wa siku mbili, Kilaini, alisema hofu hiyo inatokana na mazingira ya utekaji isiyoonyesha sababu ya watu kutekwa na kuteswa.

Kilaini alisema hali ya kutokufahamika kwa sababu za watu kutekwa kunawafanya hata viongozi wa dini kupatwa na wasiwasi wa kukumbwa na matukio hayo.

“Hali hii ikiendelea hivi hata sisi viongozi wa dini tunaweza kutekwa kwa sababu hatujajua kwanini watu wanatekwa, tunapata wasiwasi mkubwa,” alisema.

Kilaini alisema Tanzania ni nchi ambayo watu hutembea kwa uhuru lakini kwa sasa maisha yamekuwa ya hofu ya kutekwa.

“Hapa nchini tunatembea kwa uhuru kabisa, lakini kwa sasa hivi imekuwa ni shida, naona watu wameanza kuogopa, wasanii na hata nyinyi watu wa habari, kuanzia hapo itaenda kwa kuteka mara huyu au yule na hiyo hali si nzuri,” alisema na kuongeza:

“Kwa kweli nina wasiwasi, naona hata waandishi nyinyi mko hatarini, mnapotea hivi hivi hata mkirudi mnaogopa namna ya kuongea.

“Sisi tunaomba hatua kubwa ichukuliwe kwa maana ya polisi kufanya kazi yake kwa sababu kwa mara ya kwanza Tanzania tulikuwa hatujapata vitu kama hivi. Ilikuwa inatokea mara chache na inaeleweka ni wezi na walionekana wanaiba lakini kwa matukio haya ya sasa inatia wasiwasi.”

Alisema hali hiyo ikiachwa ni hatari kwa sababu inazua hofu kwa wananchi na watu wakifanya kazi kwa woga mambo hayatakwenda.

“Tunaomba Mungu atusaidie litoke kabisa. Wanaochunguza walishughulikie hadi kwenye mizizi yake, waichimbue hadi mizizi waing’oe la sivyo nchi haiwezi kukalika. Jambo la kutafuta ni iko wapi mizizi ya utekaji la sivyo nchi haitakalika kwa sababu mtu hawezi kutembea hata njiani,” alisema.

Mtazamo huo wa Kilaini umekuja wakati kukiwa na mjadala mkubwa wa hofu ya utekaji ulioibuka wiki hii ndani ya Bunge.

Katika sehemu ya mjadala huo, Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alidai kupewa taarifa na baadhi ya mawaziri kuwa yeye na wabunge wenzake 10 wako katika hatari ya kuuawa na kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo vya utekaji.

Hoja ya Bashe iligusa na wabunge wengi na iliibua sakata la kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ben Saanane, aliyepotea kusikojulikana tangu Novemba, mwaka jana.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), ameelezea hofu ya utekaji nyara kwa kusema ni vyema sasa ikaundwa kamati teule ya kuchunguza vitendo vya utekaji.

“Mtanzania aliyepotea, Ben Saanane ni suala linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito wa juu, si suala linalopaswa kuchukuliwa kisiasa,” alisema.

Akikazia hoja yake, Zitto, alikwenda mbali kwa kukumbusha tukio la aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, aliyeteswa na kuumizwa na watu wasiojulikana hadi leo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Serikali inafanyia kazi vitendo vya utekaji watu na itatoa taarifa baada ya kufanyika uchunguzi.

 “Wabunge wamezungumzia suala la usalama. Ninaomba niwahakikishieni kwamba Serikali inalifanyia kazi na baadaye tutatoa taarifa kwenu. Tuache vyombo vyetu vifanye kazi ya uchunguzi.

“Kwamba ni nani anayefanya haya na je, matukio haya yanakubalika? Tunajua ni matukio yasiyokubalika,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles