23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA ABAINI MADUDU BODI YA WETCU

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa

 

Na Mwandishi Wetu,

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema timu aliyoiunda ichunguze tuhuma za ubadhirifu kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Tumbaku (WETCU), imekamilisha kazi yake na imebaini madudu mengi zaidi.

Machi 16, 2017, Waziri Mkuu aliivunja Bodi ya WETCU pamoja na Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) kwa sababu ya kushindwa kusimamia zao hilo pamoja na matumizi mabaya ya fedha za umma. Alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora awakamate viongozi wanne pamoja na kufunga ofisi za chama hicho hadi uchunguzi wa fedha za chama hicho utakapokamilika.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana, Majaliwa ambaye alifanya ziara ya siku moja mkoani Tabora jana, alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wajumbe zaidi ya 300 wa mkutano wa wadau wa zao la tumbaku katika Ukumbi wa Kiyungi Mwana Isike, mjini Tabora.

“Nilikuja Tabora mara ya kwanza ili kuchukua hatua za dharura na leo nimekuja kuendelea na mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuwezesha kilimo cha tumbaku kiwe na tija kwa wakulima na ndiyo maana niliomba wakulima, wanunuzi wa tumbaku, vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS) na viongozi wa Serikali wawepo kwenye mkutano huu,” alisema.

Akitoa mrejesho juu ya uchunguzi uliofanywa na timu aliyoiunda, Waziri Mkuu alisema WETCU haikuwa na kitengo cha ununuzi kwa zabuni.

“Waliunda kampuni inayoitwa FDTU (Flu and Dark Tobacco Union) ambayo ni Umoja wa Wenyeviti wa Union zote za Tumbaku nchini ambayo ilipewa kazi zote za ununuzi wa pembejeo na hela walikuwa wanagawana,” amesema.

“Tumefanya ufuatiliaji hadi katika benki lakini kwenye akaunti lakini hakuna hela mpaka sasa. Tumeangalia chanzo cha fedha za union zenu na kubaini hakuna fedha zinazotoka FDTU kwenda WETCU,” aliongeza.

Akifafanua kuhusu kashfa ya ununuzi wa gari aina ya shangingi lenye namba za usajili T181 DEN ambao ulifanywa kinyume na maazimio ya mkutano mkuu, Waziri Mkuu amesema viongozi wa WETCU walitumia zaidi ya Sh milioni 220 kuzidi kiwango kilichoidhinishwa na Mkutano Mkuu cha kununua gari lenye thamani ya Sh milioni 40.

“Gari walilolinunua ni la mwaka 2008 na si la mwaka 2015 kama taarifa zinavyoonesha. Lilikwishatumika kwa kilomita zaidi ya 95,000

lakini likarekebishwa hadi kubakiza kilomita 16,000 ili lionekane ni jipya, maana yake wamekula fedha nyingi sana na ni lazima tuwachukulie hatua za kisheria kwa sababu wamekula fedha, wamenunua gari lililotumika na si maamuzi ya mkutano mkuu.” 

Waziri Mkuu ameagiza Mkurugenzi wa Kampuni ya 4×4 Tanzania Limited, Faraz Yaseen, naye akamatwe na kuhojiwa ni kwanini alihusika na kuuza gari la mwaka 2008 lakini akabadilisha nyaraka ili lionekane ni la mwaka 2015. 

Akitoa ufafanuzi kuhusu uuzaji wa hisa za WETCU, Waziri Mkuu amesema chama hicho kilikuwa na hisa milioni 36 ambapo kilitoa milioni sita ili ziuzwe na zikapatikana Sh bilioni 2.520 na ndiko huko walitoa fedha za kununulia gari na vifaa vya ofisi kwa Sh milioni 49.

“Walichukua hisa 100,000 na kuziuza na wakapata Sh milioni 250 lakini fedha hizo hazikuwekwa kwenye akaunti ya chama. Hisa zilizobakia ambazo ni milioni 30, walishaanza mchakato wa kuuza hisa milioni 28.

“Je, mlishatoa kibali, wamempatia cheti halisi cha hisa hizo wakala Zani Security ili auze hisa hizo bila kuomba kibali cha mkutano mkuu,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles