27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

BOSI WA FREEMASON ACHOMWA MOTO DAR

Waombolezaji wakiwa wamebeba mwili wa aliyekuwa Kiongozi wa Freemasons Tanzania, Sir Andy Chande, wakielekea kuuchoma moto katika eneo la mazishi hayo lililopo Kijitonyama, Dar es Salaam jana.Kijitonyama, Dar es Salaam jana.

Na TUNU NASSOR – DAR ES SALAAM

MWILI wa aliyekuwa Kiongozi wa Jumuiya  ya Freemason Tanzania na Afrika Mashariki, Sir Jayantilal Keshavji Chande (89) ‘Andy’ Chande umefanyiwa mazishi kwa kufuata mila za dini yake kwa  kuchomwa moto.

Mwili huo uliondolewa nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam jana saa nne asubuhi na kuelekea katika makaburi ya dhehebu la Hindu yaliyoko Kijitonyama.

Akizungumzia utamaduni wa kuchoma moto maiti, Mwenyekiti Mstaafu wa dhehebu hilo, Dk. Ramesh Shah,  alisema katika imani yao wanaamini kuwa mtu anapofariki roho yake hubaki karibu na mwili huo.

Alisema iwapo mwili huo hautateketezwa basi roho yake  haindoki itaendelea kusubiri katika eneo uliopo mwili huo.

“Tunapoteketeza mwili uliokufa hutoa fursa kwa roho kuondoka na kwenda kuzaliwa katika mwili mwingine,” alisema Dk. Shah.

Akimzungumzia marehemu Dk. Shah alisema Sir Chande alikuwa ni maarufu kutokana na kujitoa kwake katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

“Katika harakati za maazimio ya Arusha biashara ya familia yake, kiwanda cha Chande Industries Limited kilitaifishwa kwa Serikali Februari 7, 1967.

“Marehemu Sir Chande alikubali kunyang’anywa kiwanda chake cha kusaga nafaka na kukubali kufanyakazi kama mwajiriwa katika kiwanda hicho ambapo Hayati Mwalimu Nyerere, alimwalika Chande kusaidia kuanzishwa kwa Shirikisho la viwanda vya kusaga na kuchakata (NMC),” alisema Dk. Shah.

Alisema Chande alikubali kwa uaminifu kuwa Mkurungezi Mkuu wa National Milling Corporation kwa kipindi cha miaka mitano, baada ya kustaafu alitumika kama mshauri wa bodi ya shirika hilo.

Kwa upande wake Balozi Juma Mwapachu, alisema Sir Andy Chande  alitoa mchango mkubwa ndani ya nchi na  katika Nyanja za kimataifa.

Alisema baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kwanza mwaka 1977 , Sir Chande alikuwa mwasisi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC).

“Alichangia kwa kiasi kikubwa kuundwa kwa taratibu za uendeshaji wa shirika hilo akiwa kama mwenyekiti wake,” alisema Balozi Mwapachu.   

Naye mmoja wa watoto wa marehemu, Anuj Chande alisema watamkumbua baba yao kutokana na kuwa na upendo na kushirikiana na jamii ya Tanzania na kimataifa katika masuala mbalimbali.

“Baba alikuwa akiwasaidia zaidi ya wanafunzi 100 katika masomo yao na pia alianzisha mashirika yasio ya kiserikali ya kuisaidia jamii kama shule ya viziwi Buguruni, shirika la  msalaba mwekundu na ushirikiano wa Tanzania na Ujerumani,” alisema Anuj.

Sir Andy Chande alifariki Aprili 6, mwaka huu jijini Nairobi baada ya kuugua tumbo kwa kipindi cha wiki moja wakati ugonjwa wake mkubwa uliokuwa ukimsumbua ulidaiwa kuwa presha.

Malkia Elizabeth wa Pili  wa Uingereza alimtunuku medali ya heshima ya kuwa  Commander of  the Civil Division of the Most Excellent Order of the British Empire (KBE),”ilieleza taarifa hiyo.

Katika miaka kabla ya uhuru wa Tanzania,  Sir Chande ametumikia katika nafasi ya mwanachama wa Legislative Council (LEGICO ) mwaka 1958 hadi 1961.

Mwaka 1959, alipata nafasi ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Katibu Kuu wa serikali ya Uingereza Ian McLeod kuhusiana na mapendekezo ya Uingereza kutoa uhuru wa kujitawala kwa Tanganyika.

Baada ya uhuru, Chande alishiriki katika shughuli mbalimbali nchini hasa za kijamii na kiuchumi.

Kwa nyakati tofauti aliwahi kuwa mwenyekiti au kama mwanachama wa bodi ya wakurugenzi wa makampuni kadhaa ya umma na binafsi ikiwa ni pamoja na Benki ya Barclays Tanzania na Uganda na pia  mashirika mbalimbali ya Serikali , ikiwa ni pamoja na Shirika la Reli la Afrika Mashirika na East African Harbours Corporation.

Baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, Sir Chande aliteuliwa kuwa  mwanzilishi na Mwenyekiti wa Shirika la Ndege Tanzania  (ATC) na baadaye Mwenyekiti wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na wa Tanzania Railways Corporation (TRC).

Chande alikuwa anajishughulisha na masuala ya  kisiasa na kidiplomasia na wakati mmoja aliwahi kuwa mshauri wa Wizara ya Kamati ya Umoja wa Afrika ambayo inashughulikia masuala ya migogoro ya mafuta nchi za waraabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles