Na JUDITH NYANGE – MWANZA
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Samweli Masumbuko (32), Mkazi wa Kata ya Mahina wilayani Nyamagana, kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 10.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, mtuhumiwa huyo alikamatwa Aprili 1, mwaka huu saa 11:00 jioni katika Mtaa wa Mwembeni, Kata ya Mahina.
Kamanda Msangi alisema mtuhumiwa anadaiwa kuwa alimbaka mwanafunzi huyo Machi 25, mwaka huu saa 11:00 jioni, lakini kwa kipindi chote hicho hakuweza kusema kwa mtu yeyote hadi Aprili 1, mwaka huu mama yake alipogundua mwanawe kufanyiwa ukatili huo.
“Mama wa mtoto huyo aligundua tukio la kubakwa kwa mwanawe wakati akimwogesha, kisha akatoa taarifa polisi ambao walifanya ufuatiliaji wa haraka kwa kushirikiana na wananchi na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa.
“Samweli Masumbuko anakabiliwa na tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Mahina na kumsababishia maumivu makali sehemu zake za siri,” alisema Kamanda Msangi.
Alisema upelelezi dhidi ya watu waliohusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha au kushawishi ukatili huo bado unaendelea na kwamba mtuhumiwa anahojiwa na Jeshi la Polisi na pindi uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Hata hivyo, Kamanda Msangi amewashauri wazazi au walezi kuwa na utaratibu wa kuwakagua watoto wao mara kwa mara ili kuweza kubaini mapema kama wana tatizo.