Na BAKARI KIMWANGA
UKUAJI wa uchumi Tanzania unaelezwa kuwa mzuri kuliko nchi nyingine zilizopo katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki kama vile Kenya, Rwanda na Burundi.
Mchumi kutoka Kurugenzi ya Sera za Uchumi na Utafiti wa Benki Kuu ya Tanzania, Lusajo Mwankemwa, anasema takwimu za ukuaji wa Pato la Taifa zinaonesha kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kukua vizuri.
Anasema ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni mzuri ukilinganisha na nchi nyingine zilizopo Afrika Mashariki, huku ikiwa miongoni mwa nchi za bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa.
Ikiwa na ukuaji wa uchumi wa asilimia 7.0 mwaka 2015/16, Mwankemwa anaeleza Tanzania ipo mbele ya nchi jirani kama Burundi ambayo kwa mwaka jana, uchumi wake ulikua na kufikia asilimia 4.0, huku matarajio yao ilikuwa ni kufika asilimia 5.0. Tanzania pia ipo mbele ya Kenya ambayo ukuaji wake ni asilimia 5.6, huku malengo ikiwa ni kufikia 6.0, Rwanda 6.9 na matarajio kwa mwaka 2016 ilifikia 6.0.
Mchumi huyo ansema katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka jana, kiwango halisi cha ukuaji wa Pato la Taifa kiliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 6.5, ikilinganishwa na kiwango cha ukuaji cha asilimia 6.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2015, huku akifafanua kuwa sekta nyingi zilikua kwa kasi isipokuwa sekta chache.
“Sekta zilizokuwa na viwango vikubwa vya ukuaji katika kipindi hicho ni pamoja na shughuli za uchimbaji madini na mawe (asilimia 15.8); shughuli za usafirishaji na uhifadhi wa mizigo (asilimia 15.5); habari na mawasiliano (asilimia 13.4); na huduma za fedha (asilimia 11.5).
“Maoteo ya ukuaji wa Pato la Taifa kwa mwaka 2016 (Januari-Desemba) yalitarajiwa kuwa asilimia 7.2. Hata hivyo, ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2016 ulifikia asilimia 7.0, chini ya matarajio, hali ambayo ilitokana na mwenendo wa uchumi katika miezi tisa ya mwanzo ambapo sekta zinazoajiri watu wengi na zenye mchango mkubwa katika uchumi hazikukua
katika kasi iliyotarajiwa ikiwemo sekta ya kilimo ambayo ilikua kwa wastani wa asilimia 2.1 (matarajio ya mwaka ni asilimia 2.6).
“Biashara ilikua kwa wastani wa asilimia 5.6 (matarajio ya mwaka ni asilimia 7.6). Aidha, kuzorota kwa uchumi kwa nchi za Jumuiya ya Ulaya na China ambao ni wabia wetu wakubwa wa biashara na uwekezaji ndio kumechangia kupunguza matarajio ya awali ya kasi ya ukuaji wa uchumi nchini. Kasi ya ukuaji wa uchumi wa China inakadiriwa kupungua kutoka asilimia 6.9 mwaka 2015 hadi asilimia 6.6 mwaka 2016,” anasema Lusajo.
Mfumuko wa bei
Anasema mfumuko wa bei ulipungua kutoka asilimia 6.5 Januari mwaka jana hadi asilimia 5.5 Juni mwaka jana na kupungua zaidi hadi asilimia 4.5 Septemba 2016 na baadaye kupanda kidogo Desemba na kufikia asilimia 5.0.
Aidha, anasema mfumuko wa bei kwa mwaka mzima wa 2016, ulipungua na kufikia wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 5.6 mwaka 2015.
“Maana yake ni kuwa bei za bidhaa na huduma ziliongezeka kwa kasi ndogo zaidi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma. Mwenendo huu wa kushuka mfumuko wa bei ulichangiwa na kasi ndogo ya ongezeko la bei za chakula nchini, kushuka kwa wastani wa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia, utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti na fedha na
utulivu wa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani,” anasema.
Kutokana na hali hiyo, Lusajo anasema mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kubakia katika viwango vya tarakimu moja katika siku zijazo na kubakia ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5.0.
Kwa mujibu wa mchumi huyo, matarajio hayo yatategemea kuendelea kutulia kwa bei ya nishati nchini kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa umeme, mwendelezo wa sera thabiti ya fedha na kibajeti, kutobadilika sana kwa bei za mafuta katika soko la dunia pamoja na kuendelea kuwepo kwa utulivu wa thamani ya Shilingi.
Hata hivyo, anasema vipo viashiria vinavyoonesha uwezekano wa kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutokana na hali ya ukame iliyojitokeza hapa Tanzania na kwa baadhi ya nchi za ukanda wa Afrika Mashariki pamoja na uwezekano wa kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Thamani ya Shilingi
Anasema katika kipindi cha Julai – Desemba mwaka jana, Serikali iliendelea na utekelezaji wa sera za fedha na bajeti, hatua zilizowezesha kuimarika kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani. Katika kipindi hicho, thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani ilipungua kwa kasi ndogo kutoka wastani wa Shilingi 2,144.27 kwa dola moja Desemba 2015 hadi Sh 2,170.44 kwa dola moja Desemba mwaka jana.
Kuimarika kwa thamani ya Shilingi kulitokana na hatua mbalimbali za sera ya fedha zilizochukuliwa na Benki Kuu katika kusimamia hali ya ukwasi kwenye uchumi pamoja na kuimarika kwa urari wa bidhaa na huduma katika sekta ya nje.
“Thamani ya Shilingi kwa Dola ya Marekani ilishuka (kwa takriban asilimia 2.15 katika kipindi cha 12 kufikia Januari 19, mwaka huu), kufuatia kuimarika kwa Dola ya Marekani.
“Kuimarika kwa Dola ya Marekani kuliathiri pia sarafu nyingine zikiwemo Yuan ya China (iliyoshuka thamani kwa asilimia 3.55 katika kipindi cha miezi 12 kufikia Januari 19, mwaka huu), Shilingi ya Uganda (asilimia 3.7), Faranga ya Rwanda (asilimia 8.55)
na Pauni ya Uingereza (iliyoshuka thamani kwa asilimia 13.04),” anasema.
Akizungumzia juu ya kuimarika kwa Dola ya Marekani, kulitokana zaidi na kupanda kwa riba ya sera ya fedha (policy rate/Fed Fund rate) Desemba mwaka jana, hali iliyosababisha wawekezaji kuongeza mahitaji yao ya Dola ya Marekani kwa ajili ya kuwekeza.
Na kwa upande wa Tanzania, Januari ni msimu wa mapato madogo ya fedha za kigeni zitokanazo na mauzo ya mazao ya biashara, hali ambayo imechangia pia kuwa na dola pungufu kwenye soko la fedha.
Sekta ya nje na akiba ya fedha za kigeni
Lusajo anasema mwaka jana, nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje (current account deficit) ilipungua kwa asilimia 48.8 na kufikia nakisi ya Dola za Marekani milioni 2,054.8, kutoka nakisi ya Dola za Marekani
milioni 4,011.6 kwa mwaka 2015.
Kupungua huko kulitokana zaidi na ongezeko la thamani ya madini hususan dhahabu, bidhaa asilia, mapato yatokanayo na utalii pamoja na kupungua kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususan bidhaa za kukuza mitaji na bidhaa za matumizi ya kawaida.
“Katika kipindi hicho, thamani ya bidhaa na huduma zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 5.2 na kufikia Dola za Marekani milioni 9,381.6 wakati thamani ya bidhaa na huduma toka nje zilipungua kwa asilimia 13.7 na kufikia Dola za Marekani milioni 10,797.4.
“Hadi Desemba mwaka jana, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola za Marekani milioni 4,325.6 ambazo zinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takriban miezi 4.2.
“Rasilimali za fedha za kigeni za mabenki ya biashara zilifikia Dola ya Marekani milioni 768.2, wakati amana za fedha za kigeni zilizohifadhiwa na wakazi katika benki za biashara zilifikia Dola za Marekani milioni 2,870.8. Hivyo, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kuwa ya kuridhisha,” anasema Lusajo.
Mikopo kwa sekta binafsi
Anasema mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 7.2 katika kipindi cha mwaka ulioishia Desemba 2016 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 24.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Kupungua kwa kiwango cha ukuaji kulitokana na tahadhari iliyochukuliwa na mabenki kufuatia kuongezeka kwa mikopo chechefu kutoka asilimia 6.4 Desemba, 2015 hadi asilimia 9.5 Desemba, 2016.
“Ni vema pia ieleweke kuwa kupungua kwa kasi ya kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi katika miezi ya hivi karibuni, si kwa Tanzania pekee. Kwa mfano, kiwango cha ukuaji wa mikopo kwenda sekta binafsi katika nchi jirani ya Kenya kilipungua kutoka asilimia 19.7 kati ya Julai na Oktoba 2015 hadi kufikia asilimia 4.1 katika kipindi kama
hicho mwaka jana.
“Aidha, nchini Uganda mikopo kwa sekta binafsi ilipungua kutoka asilimia 25.2 Septemba mwaka 2015 hadi asilimia -1 Septemba 2016. Pia mwenendo usioridhisha ulijitokeza katika mikopo chechefu katika nchi hizo jirani na kusababisha baadhi ya mabenki hususan Benki ya Crane ya Uganda kuwekwa chini ya uangalizi. Hali ni mbaya zaidi kwa nchi kama Nigeria na Ghana zinazouza mafuta.