Na MWANDISHI WETU
RAPA ambaye wimbo wake wa ‘Wapo’ unazungumzwa zaidi kwa sasa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari, Emmanuel Elibariki (Nay wa Mitego), amesema kwa sasa anajipanga ajue cha kuzungumza na Rais Magufuli kama atapata nafasi ya kukutana naye kama alivyomuagiza.
Ney alisema alipotoa wimbo wake huo alijua hautafurahiwa na watu wote, lakini kwa sasa anashukuru kuwa huru, na sasa anafikiria cha kuzungumza na Rais kama atapata bahati ya kukutana naye.
“Kwa sasa nafikiria mwaliko wa Rais wa kukutana naye, lakini pia kama nitakutana naye nitamweleza kuhusiana na malengo ya wimbo wangu na namna wananchi wanavyomzungumzia huku mitaani,’’ alisema Ney.
Baadhi ya nyimbo za msanii huyo zilizowahi kufungiwa kutokana na madai mbalimbali, ikiwamo ya kukiuka maadili ni ‘Shika Adabu Yako’ aliowaimba baadhi ya wasanii wenzake, ‘Pale Kati’ uliodaiwa kuwadhalilisha wanawake. Pia wimbo wa ‘Itafahamika’ alioimba baadhi ya wasanii wenzake uliwahi kumletea matatizo na baadhi ya wasanii wenzake waliomwelewa tofauti na malengo yake alipotoa wimbo huo.