NAIROBI, KENYA
MUUNGANO wa upinzani nchini hapa, NASA umetangaza kuwa utaanzisha kituo cha kujumuisha kura na kutangaza matokeo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8.
Vinara wa muungano huo walisema dhima ya kuanzishwa kwa kituo hicho ni kuzuia kile walichotaja kama njama za chama cha Jubilee za kuiba kura, hasa zile za urais.
"Wakati huu, tutabuni kituo chetu cha kujumuisha kura za urais. Tutaweka mitambo ya kielektroniki," alisema kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka.
"Wajibu wa kujumuisha kura si wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pekee. Sisi pia tunaweza kuwa na kituo chetu," aliongeza Musyoka wakati akiwahutubnia maelfu ya wafuasi wao kwenye Uwanja wa Masinde Muliro, Jimbo la Kibunge la Mathare lililopo Kaunti ya Nairobi.
Naye Kiongozi wa Chama cha ANC, Musalia Mudavadi alidai IEBC inapanga kutumia mfumo wa zamani badala ya eletroniki kwa lengo la kuiba kura.
"Tunawaonya wasithubutu kufanya hivyo kwani wakati huu tutakuwa macho zaidi," alisema.
Kalonzo pia aliisuta serikali kwa kile alichodai usimamizi mbaya wa uchumi hali, ambayo imepelekea kupanda kwa gharama ya maisha kwa Mkenya wa kawaida.