29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KUACHILIWA HURU HOSNI MUBARAK KUMEACHA SOMO GANI KWA TAIFA LETU?

NA YAHYA MSANGI, LOME-TOGO

HOSNI Mubarak alipinduliwa mwaka 2011 na alikuwa rais wa kwanza kushtakiwa katika kile kimbunga cha Kiarabu (Arab Spring). Sasa Mubarak yupo huru baada ya kuachiliwa na Mahakama ambayo imemwondolea makosa ya kuwaua waandamanaji mwaka 2011.

Kuna visa na mikasa katika kesi hii ya Hosni Mubarak inapaswa tujifunze baadhi ya mambo! Hasa wanasiasa wanaotumia nguvu ya umma. Kuna masomo anuwai na ingekuwa vyema katika timu zao wakae chini na kuchambua hii kesi ya mafarao.

Kisa cha kwanza

Hosni Mubarak alikaa 'kizuizini' kwa takribani miaka 6. Ni kizuizi cha ajabu, maana alikuwa chini ya askari wake! Siku zote Mubarak alikuwa anajulikana ni 'mgonjwa' na akifikishwa mahakamani ndani ya machela.

Ila baada tu ya kuachiwa huru, Mubarak ameweza kusimama na kupungia watu mikono kupitia dirisha la kasri lake lililopo eneo la Heliopolis. Mgonjwa kapona kwa furaha.

Je, walioendesha mpambano walijua au hawakujua kuwa ile ilikuwa picha la Kichina? Kama hawakujua si mapungufu makubwa? Hivi Mubarak hawezi kurudi madarakani tena? Si mahakama ya rufaa imeshamsafisha?

Kisa cha pili

Licha ya kukaa madarakani miaka 30, Rais Mubarak 'aliondoka'  Ikulu bila kupenda baada ya maandamano ya siku 18 tu. Ilikuwaje rais wa mkono wa chuma vile hakujiandaa kiasi kile?

Je, waliowezesha tukio lile la ajabu walipotea njia? Zilikuwa nguvu za soda dhidi ya Mubarak? Lazima kuna kitu walikosea si bure!

Kisa cha tatu

Kuachiliwa kwa Mubarak kumekuja kwa kificho! Watu wamekuja kujua kuwa yuko huru siku moja baadaye.  Si wapinzani wala wala jumuiya ya kimataifa ilikuwa na taarifa kuwa Mubarak ataachiwa huru! Naamini hapa kuna somo la kujifunza pia!

Kisa cha nne

Kila Mubarak alipokuwa akifikishwa mahakamani kulikuwa na waandamanaji kibao wanaompinga na wakishinikiza apewe kifungo cha maisha au anyongwe. Lakini hata baada ya watu kujua ametoka jela wiki hii na wahamasishaji kuanza kushawishi vijana wajimwage barabarani kupinga uamuzi wa Mahakama ya rufaa, lakini vijana wamekataa kuingia barabarani.

Kuna dalili zote za kuchoka kwa kundi hilo la vijana. Ndugu zetu hawa wanasiasa ni vyema wakaelewa kuwa, mpambano ukidumu muda mrefu bila mafanikio huleta mchoko wa mwili na akili.

Kisa cha tano

Kwa kipindi alichokuwa 'kizuizini' ulifanyika uchaguzi ambao kiongozi kutoka chama cha Muslim Brotherhood, Mohamed Mursi, alishinda na kutawala kiduchu kabla ya kupinduliwa na maofisa wa jeshi ambao walilelewa na Hosni Mubarak.

Mapinduzi haya, kama yale ya kuwaondoa Al Shaabab waliposhinda kura Somalia, hayakulaaniwa na ambao huwa wanaamini kwamba viongozi wapatikane kwa kura. Kwa Misri na Somalia kura ikaonekana si demokrasia.

Kuna ndugu zetu wanadhani watu wa nje wanajali sana kura! Hili ni somo zuri kwao. Wenzetu wana maslahi yao ndiyo wametanguliza mbele. Nchini Misri na Somalia wameunga mkono kukataa matokeo ya sanduku la kura.

Kisa cha sita

Vijana wengi wa Misri sasa wanaamini vyombo vya dola chini ya Hosni Mubarak vilikuwa afadhali kuliko sasa chini ya Jenerali El Sisi. Yaani jana afadhali kuliko leo! Mbona hii tabia ya kudai bora ya aliyetoka inashika kasi sana barani Afrika?

Hivi karibuni nimesikia hapa vijana pale mjini Banjul nchini Gambia wakidai bora ya Yaya Jammeh kuliko Adam Barrow! Inasemekana mkuu mpya analindwa na vikosi vya nje ambavyo vinawasumbua wananchi! Inasemekana pia Barrow kaweka watu wake nao wameanza kula nchi!

Kisa cha saba

Uchumi wa Misri umeporomoka mno. Uchumi wake unategemea sana biashara ya utalii. Ukifika Misri ile ya wakati ule hutasita kuona vivutio vyao vya utalii vilivyokuwa na mvuto.

Kuanzia kijito alichookotewa kitoto Musa, usukani wa kusukuma maji wa Jakobo, makaburi ya Mafarao 'Pyramids', sehemu Maria alipokimbilia na kitoto chake kupata hifadhi, kichaka Mungu alipotaka kumwonyesha Musa kuwa mimi ndio mwanzo na mwisho, Sphinx, jumba la Malkia Cleopatra lililozama baharini, kijiji cha kumbukumbu za maisha enzi za mafarao 'Pherionic village', jumba la makumbusho ambapo pamehifadhiwa hadi miili ya mafarao na mali zao na kadhalika.

Vyote hivi vimeparaganyika kwa maandamano ambayo hatimaye yamewatumbukia nyongo! Je, kuendesha mpambano bila kujali kama mpambano huo unaharibu au kujenga uchumi wa nchi ni jambo la busara?

Ni jinsi gani watu waendeshe harakati bila kuhujumu uchumi wa nchi yao? Hivi pale Misri sasa nani ndio kaumia kati ya Mubarak na watu wake au wanasiasa na vijana?

Haya ndiyo maajabu saba kwa Misiri na Hosni Mubarak. Je, wapinzani na watawala wetu kuna lolote la kujifunza? Je, wananchi wa Tanzania tuna la kujifunza katika varangati hilo la wananchi na wanasiasa wa Misri ?

Tuko tayari kupitia hii njia waliyopitia wananchi wa Misri? Ina faida au hasara tupu kwa Tanzania yetu? Tunapaswa tujiulize sana maana wamisri wa kawaida wameambulia maumivu ya kutosha.

Rais Mursi naye bado yuko jela anapigania asinyongwe au kufungwa maisha. Si ishara nzuri kwa wanaoendesha mpambano bila maandalizi ya kutosha na namna nzuri ya kutohujumu vitega uchumi vya nchi.

Wasalaam!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles