27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SALAMU KWA RAIS WANGU MAGUFULI

Baadhi ya waandishi wa habari

NA MARKUS MPANGALA

RAIS wangu John Magufuli, ninakutii kwa akili, moyo, nguvu na kutoa heshima zangu zote kwako na mamlaka uliyonayo. Nafanya hivyo nikitambua kuwa, wewe ni kama mzazi kwangu na kiongozi wa Watanzania wote.

Utii huu haina maana unaninyima nafasi ya kujisaili binafsi au wewe kwa mamlaka uliyonayo nchini. Kwamba katika kipindi chako cha utawala kwenye nchi yetu usitarajie kuwa vyombo vya habari vitakuwa na habari za kukupendeza na kukuburudisha tu.

Vyombo vya habari vinaadabisha, vinaelimisha, vinaonya na kukemea, vinaburudisha na kusisimua, vinatangaza mazuri na mabaya, vinapenda amani, ndiyo maana hadi leo nchi yetu haijawahi kuwa na machafuko kama ya Rwanda na Burundi ambako vyombo vyao vilikuwa mstari wa mbele kuchochea uhasama baina ya makundi ya kijamii na kikabila. Sitarajii hayo kutokea katika uhai wa nchi hii.

Aidha, vyombo vya habari nchini vinaongozwa na Watanzania ambao hawana mahali pa kukimbilia. Tanzania ni nchi yao na wanaipenda mno kuliko kawaida, kama ambavyo baadhi yao wamekuwa mstari wa mbele kukuunga mkono inapobidi, kukukumbusha na kusisitiza pia.

Haitawezekana na hakuna chombo cha habari kinachoweza kufanya utani huo wa kukufurahisha kila siku Rais wangu. Leo hii vyombo vya habari vikikuuliza juu ya mradi wa zahanati za kata, shule za sekondari kwa kila kata, VETA kila wilaya, vituo vya tiba za kansa kila wilaya, na kero kedekede zilizojaa ndani ya jamii zetu utawajibu kweli?

Haitawezekana hata siku moja chombo cha habari kikaandika tatizo ambalo halipo humu nchini. Kama matatizo hayo yapo ni serikali yenyewe imesababisha, imechangia, imelea na kuendekeza mambo hayo. Waandishi wa habari ni sehemu ya wananchi wanaokumbana na kero au furaha iwapo Serikali inatekeleza huduma zake.

Leo hii ninavyoandika makala haya kuna mitambo ya kuzalisha umeme ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco) imezuiliwa katika Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa madai ya kutolipiwa Sh bilioni 4.

Tunafahamu kuwa, kadhia hii inahusisha mitambo hiyo na jenereta kutoka nje ya nchi, jambo ambalo linarudisha nyuma uzalishaji wa umeme nchini. Mfano huu ni kwamba hilo lipo kwenye taasisi za Serikali unayoiongoza, si kwenye vyombo vya habari.

Desemba 2016 na Februari 2017 nimeshuhudia ubovu wa barabara inayoanzia njia panda ya Kitai (makutano ya Wilaya ya Songea, Mbinga na Nyasa) kuelekea Lituhi, hali ambayo inawakwaza kampuni ya uchimbaji wa makaa ya mawe ya TANCOAL.

Nafahamu kuwa tayari Bandari ndogo ya Kijiji cha Ndumbi (Wilaya ya Nyasa) imejengewa Gati, ili ufike hapo ni kazi kubwa mno kutokana na ubovu wa barabara.

Hapo kijijni kuna majengo ya Shirika la Uvuvi yametelekezwa. Na siku vyombo vya habari vikilivalia njuga suala hilo tutavilaumu kweli Rais wangu?

Hakuna mahali popote duniani ambako chombo cha habari kitafanya kazi ya kumpendeza tu mtawala. Hakuna nchi ambayo vyombo vya habari vinaumba matatizo na kuyaongelea kama vile ni ya kufikirika.

Rais wangu Magufuli suala la askari wa Jeshi la Polisi nchini kumtolea bastola Nape Nnauye ni kubwa, ikizingatiwa kuwa wewe ndiye uliyemtoa madarakani, na taasisi ya Serikali ndiyo iliyomzuia asifanye mkutano ule na waandishi wa habari.

Nape hakuwa katika mazingira ya kihalifu wala kukaidi amri. Pamoja na makosa ya kiuongozi ambayo huenda Nape ameyatenda na akiketi chini kuyafanyia kazi atabaini, bado nitamtetea kwa haki yake ya kujieleza kama raia.

Naamini vilevile yapo makosa ya dhahiri kabisa ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambayo yataendelea kututafuna tuendako.

Iweje Rais wangu unalalamikia bastola ya askari ambaye alishindwa kuelewa tofauti au aina ya mtu anayemzuia? Ni vyombo vya habari ambayo havikumpa kitambulisho askari wa Jeshi la Polisi? Hivi kuhoji kuwa kitambulisho cha askari ni kipi kisha akatoa bastola, je, hiyo ni kitambulisho ama ni silaha?

Ndugu Rais, usitarajie kuwa Watanzania wote wanavutiwa na aina ya utendaji kazi wako. Si Watanzania wote wanavutiwa na kauli unazozitoa.  Ukilifahamu hilo, yawezekana kabisa kuepuka magonjwa yasiyotarajiwa kama vidonda vya tumbo na presha.

Kutambua tofauti za mawazo ni jambo la kawaida kwa kiongozi yeyote. Hatukufika duniani ili tukubaliane kwa kila jambo. Katika duniani hii baadhi ya manabii walikataliwa na kukejeliwa.

Ndugu Rais wewe ni muumini wa Kanisa Katoliki na unaifahamu vema habari ya Yuda Iskarioti na Nabii Yesu. Unafahamu kilichotokea kwa Daudi na Goliati pamoja na Samweli aliyeyaona maisha ya wawili hao.

Rais wangu, nina uhakika unafahamu habari ya mwanamke mjane aliyetoa sadaka zote kuliko wengine waliojitokeza siku hiyo. Hii inakupa tafsiri kuwa, kukejeliwa au kupingwa hakukuanza leo wala wewe si wa kwanza. Kukosolewa hakukuanza leo, hata Yesu na Mtume Muhammad walikosolewa.

Mimi ni msomaji mahiri wa vitabu mbalimbali, ninakualika kuvitafuta vitabu vya ‘The Satanic Verses’ cha Rushdie, amekosoa imani ya wenzetu Waislamu. Kitabu hiki kilileta kero kubwa, lakini kinakupa mfano wa watu waliopo duniani na namna yao ya mawazo. Katu hatufanani. Kitabu kingine chenye ukorofi ni ‘The People vs Muhammad’ kimeandikwa na JK Sheindlin. Watu wa namna hii hawakosekani kwenye mataifa.

Mwandishi mwingine ni Brad Meltzer, ambaye aliandika kitabu cha ‘The Book of Lie’, akihoji juu ya silaha iliyotumiwa na Kaini kumuua Abel. Ndugu Rais na mimi ni waumini wa Ukristo tumefunzwa kuyavumilia yasiyotupendeza.

Hiyo ni mifano ya kuwa si tu kwenye vyombo vya habari, bali hata kwenye nyumba za ibada watu hatufanani. Tunayo mawazo, hulka na vitendo tofauti.

Kuyavumilia hayo ni rahisi mno kuliko kuyafanya yakuchochee ghadhabu na hasira ambazo zinasababisha magonjwa. Sitaki kukuona ukiwa mgonjwa Rais wangu sababu ya vyombo vya habari.

Utavikasirikia vyombo vya habari kwa matatizo yanayolelewa na serikali yetu yenyewe miaka nenda rudi, tunalalama mambo yaleyale, shida zilezile, mbinu za kutatua ziwe zilezile kweli Rais wangu?  

Uhuru wa mawazo ni ule ambao mtu anasema kile anachokiamini na kinatoka moja kwa moja akilini na moyoni. Sasa tatizo la uhuru huo ni matamshi au kile kinachoandikwa na mapokeo yake.

Hatuwezi kujidanganya kuwa nchi hii haisumbuliwi na tatizo la ugonjwa wa figo, wakati wataalamu wetu wa figo wanalalamikia uhaba wa bajeti ya kufanyia utafiti juu ya ukubwa wa ugonjwa husika. Hatuwezi kuona vyombo vya habari vikiacha kuandika juu ya uhaba wa fedha katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Taifa (MOI), wakishindwa kukabidhiwa bajeti yao ya Sh bilioni 4.8 tu, wakati tunajua wapo waathirika wa ugonjwa huo.

Mkoa wa Pwani umekuwa kwenye taharuki muda mrefu ambapo kumekuwa na mauaji mara kwa mara. Sitarajii kuona vyombo vya habari vikilaumiwa kwa kuja na ripoti maalumu ya matukio yasiyo ya kawaida. Sababu kubwa serikali yetu ipo na taasisi zake kama watu, majeshi na viongozi wa mkoa, wilaya na mitaa.

Mfano mwingine ni huu wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya uenyekiti wa Shally Raymond, imesikitishwa na vitendo vya kutelekezwa kwa miradi ya nyumba nane za watumishi wa wilaya za Mvomero na Gairo, mkoani Morogoro. Rais wangu ni vyombo vya habari vimeumba tatizo kama hilo?

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles