25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

VITA BINAFSI IMETUTOA KWENYE MSTARI

NA INNOCENT NGANYAGWA,

KWA kuwa Mungu ndiye aliyeumba vyote vionekanavyo duniani, ndivyo  alivyo na majibu ya kila jambo linalotokea. Ndiyo maana hakuna jipya chini ya jua.

Yanayogusa hisia za watu katika nyakati hizi yalishawahi kutokea na hata katika historia yapo.

Huu ni wakati tunaoishi sisi, kabla yetu kuna walioishi, baada yetu watakuwapo wengine nao watakaoishi.

Muktadha huo wa nyakati, ndiyo Tafakuri Yangu inashughulishwa na matukio yanayojiri hivi sasa nchini mwetu.

Kabla sijajinukuu na kumnukuu Nabii wetu wa kisiasa, Hayati Baba wa Taifa nianze kwa kunukuu maandiko ya Biblia kutoka katika Agano la Kale, kitabu cha ‘Mambo ya Nyakati’ cha pili kumhusu Mfalme Uzziah katika aya ya 26, inayosimulia jinsi watu wa Yudea walivyomsimika ufalme akiwa na umri wa miaka 16 tu ili azibe pengo la baba yake, Amaziah.

Sifa kubwa za Mfalme Uzziah ni jinsi alivyowashinda maadui zake, umaarufu wake ukasambaa katika Falme nyingine zenye nguvu, akaimarisha utawala wake kwa ulinzi na tija ya kiuchumi kutokana na mipango aliyoiandaa kwa baraka za mwenyezi Mungu.

Hakika alikuwa Mfalme mkuu aliyeinukia, msingi wa uimara wake ni jeshi lake la ulinzi lililokuwa na weledi lililoogopwa hata kusababisha nguvu zake kusifika mno.

Kwa mujibu wa maandiko hayo kuanzia mstari wa 16, nguvu zake ziliinua kiburi ndani yake, kilichosababisha anguko lake, kwani aliamua kuingia katika hekalu kutekeleza ambacho kwa kawaida hufanywa na Makuhani.

Akapingwa na makuhani wakiongozwa na Azariah: (2 Mambo Ya Nyakati 17-18): Lakini kuhani Azaria pamoja na makuhani wengine mashujaa themanini wakamfuata Mfalme na kumzuia, wakamwambia: “Si wajibu wako hata kidogo Uzziah, kumfukizia Mwenyezi Mungu ubani ni makuhani tu wa uzao wa Aroni ambao wamewekwa wakfu kufukiza ubani, ondoka mahali hapa patakatifu umemkosea Mwenyezi Mungu na hutapata heshima yoyote kutoka kwake!”

Kwa mujibu wa simulizi hiyo, Mfalme Uzziah, aliyekuwa amesimama karibu na madhabahu na chetezo cha kufukizia ubani, aliwakasirikia makuhani ghafla akashikwa na ukoma katika paji la uso kwa kuadhibiwa na Mungu, naye alijitenga nyumbani kwake na mwanawe Yothamu akachukua nafasi yake kutawala.

Kuna mafundisho makubwa katika simulizi hiyo ya Mfalme Uzziah, lakini ili unielewe vyema, nimnukuu Nabii wetu wa kisiasa hapa nchini, Hayati Mwalimu Nyerere.

Katika hotuba zake mbili aliwahi kusema: “Mungu alituumba na kutuweka katika nchi zilizopo duniani ili tuzitawale sisi wenyewe, hivyo tusitarajie malaika waje kututawalia, bali ni sisi wenyewe kwa misingi tuliyojiwekea” na katika hotuba yake nyingine alisema: “Tusifikiri kwamba sisi tunatofautiana na wengine wenye matatizo ya uhasama kwenye nchi, kwani nao walianza taratibu hadi kufikia walipo sasa!” Simulizi zote mbili zina muktadha wa matukio ya hivi karibuni yaliyoanzia kwenye jambo lililokuwa na nia njema kabisa ya kusafisha nchi yetu dhidi ya mihadarati.

Niliwahi kuandika katika ‘Tafakuri Yangu’ kwamba tusipokuwa waangalifu tukipoteza mwelekeo hatutashinda na malengo yatabadilika, maadui halisi wanaopaswa kupigwa vita watafurahia ‘vita vya panzi’ kama kunguru. Imetokea kama nilivyotahadharisha na sasa mwelekeo ni vita binafsi na hulka mpya ya ubabe ambao haujawahi kuonekana katika taifa hili.

Kama ilishangaza mitutu kuingizwa katika kituo cha utangazaji pengine kina cha uhalisia kilikuwa hakijafahamika sasa inaeleweka, ikiwa hata aliyekasimiwa usimamizi wa sekta ya habari baada ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo anaonyeshwa mtutu waziwazi bila tahayari, tena mbele ya kamera za vyombo vya habari na taifa zima limeona kilichotokea.

‘Tafakuri Yangu’ haitaki kujishughulisha kuhusu nani yuko sahihi na nani amekosea, lakini nafsi zitatusuta na historia itatuhukumu kama haya yataachiwa yaendelee.

Maana tunawaonyesha watoto na vijana wetu kwamba kutafuta ‘kiki’ kwa njia tenge ni sahihi na mitutu kutolewa ovyo hadharani ni sahihi.

Nikikurejesha katika nukuu zangu za awali, kumbukeni alichosema Mwalimu Nyerere, kuwa hatutofautiani na wengine walioanza kama tunavyoanza sasa, kwamba kama ndiyo sisi wenyewe tunaopaswa kujitawala kwa misingi tuliyojiwekea basi si katika namna tunayofanya sasa.

Bila kujali nani yuko kwenye nafasi gani, simulizi ya Mfalme Uzziah inahusika pasina shaka yoyote, turudi kwenye malengo husika tuliyoanzia, kwani figisu zote zinazotokea sasa kwa taarifa rasmi tunazozifahamu zimetokana na kupoteza malengo katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Pengine ni ‘mkakati’ uliotengenezwa kuhakikisha tunashindwa vita hiyo, kwani kwa hali ilivyo sasa kwa mfululizo wa matukio yanayojiri, tumetoka kwenye mstari na tuko katika mstari mwingine wa vita binafsi na kutunishiana misuli, huku waliolengwa awali wakiendelea kufanya yao.

Mungu atusaidie kwa kuibariki nchi yetu iondokane na mtiririko tenge wa hulka zinazotukengeusha, badala ya kuzingatia maendeleo yetu tunashabikia ubabe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles