NA EVANS MAGEGE
WAJUMBE wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), leo wanafanya uchaguzi wa kumchagua rais pamoja na wajumbe wa ngazi mbalimbali za uongozi wa chama chao.
Uchaguzi huo unafanyika mjini Arusha ambako wanachama wote wa TLS wanakutana kutekeleza ratiba hiyo pamoja na kupanga mipango mbalimbali ya utendaji kazi wa chama hicho.
Kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza chama cha TLS ambacho kilianzishwa mwaka 1954, wajumbe watakaochaguliwa leo watakuwa na dhamana ya kukiongoza chama hicho kwa kipindi cha mwaka mmoja kisha wataachia ngazi hizo ili kupisha uchaguzi mwingine.
Pamoja na kwamba uchaguzi huo utagusa nafasi nyingi za uongozi ambazo zinatakiwa kujazwa, nafasi ya rais wa chama hicho ndiyo inaangaliwa na wengi siku ya leo. Kwamba kati ya wagombea watano waliojitokeza kuwania kiti hicho ni nani atakayeibuka mshindi.
Nafasi hiyo inawaniwa na Victoria Mandari, Tundu Lissu, Francis Stolla na Godwin Mwaipongo.
Mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Lawrence Masha, alitangaza kujitoa na kumuunga mkono, Lissu dakika za mwisho jana jioni.
Kutokana na muktadha huo, MTANZANIA Jumamosi limeamua kukuletea wasifu wa wagombea wa nafasi ya urais wa TLS.
Huyu ndiye Tundu Lissu
Tundu Lissu ni wakili ambaye anafanya kazi kama Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Amejipambanua vyema masikioni na machoni mwa watu wengi kupitia siasa za upinzani na taaluma yake ya sheria na hasa umahiri wake wa kupangua hoja za mawakili wa Serikali katika kesi zinazomhusu.
Ndani ya duru za siasa, mbali na jukumu la Mwanasheria Mkuu wa Chadema, pia anatumikia nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.
Kwa nafasi nyingi ya kisiasa katika jamii, anatumikia muhula wa pili wa uwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiye Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Wakili Lissu alizaliwa Januari 20, 1968, amesoma Shule ya Msingi Maambe kati ya mwaka 1976-1982.
Alipata elimu ya sekondari mwaka 1987-1989 katika Shule ya Galanos na mwaka 1983-1986 aliendelea na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Ilboru.
Mwaka 1991-1994 alisoma masomo ya sheria kwa ngazi ya shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baada ya kuhitimu ngazi hiyo mwaka 1995-1996, aliendelea na masomo ya sheria kwa ngazi ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Warwick huko nchini Uingereza.
Victoria Mandari ni nani?
Huyu ni wakili wa Mahakama Kuu, amebobea katika masuala ya sheria ya kodi, katiba na mabenki.
Katika tasnia ya sheria kwa sasa Wakili Mandari ana uzoefu wa shughuli za mahakama kwa muda wa miaka 20.
Pia amewahi kuwa mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wanasheria nchini (TAWLA). Mwenyekiti wa GFC (Gender Forum for Constitution Review Process).
Ni mjumbe wa TLS, Chama cha Wanasheria wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC Law Association), Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki na Umoja wa Wanasheria wa Afrika (PALU).
Ana shahada ya sheria aliyopata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1984.
Pia ana shahada ya uzamili ya sheria aliyoipata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aliandika ‘thesis’ yake katika masuala ya ukwamuaji wa taasisi za kifedha na benki, kumemfanya atunukiwe vyeti vingine kutoka Chuo cha London cha masomo ya Kiafrika, Chuo cha Uongozi na Utawala wa Mahakama (Marekani), Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Wanasheria (Roma, Italia).
Francis Stolla
Francisi Stolla ni miongoni mwa mawakili maarufu nchini. Umaarufu wake umejipambanua zaidi katika utendaji wa masuala ya kisheria na hajapata kujitanabaisha wazi katika masuala ya siasa za nchi hii.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa amewahi kuwa Rais wa TLS mwaka 2012, kwa mantiki hii leo atakuwa anawania nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Hivi karibuni Stolla alikuwa miongoni mwa wanaharakati waliofungua kesi ya kupinga muswada wa sheria ya huduma za habari.
Uwepo wa jina lake katika kundi hilo la wanasheria kuliwafanya wengi wamfuatilie lakini ghafla alijitoa na bado hajawahi kutoa ufafanuzi wa kuchukua hatua hiyo.
Wakati wa uongozi wake TLS, Mei 15, 2012, wanachama wanne wa TLS ambao walikuwa wanaunda baraza la uongozi ndani ya chama chao walitangaza kujiuzulu.
Wajumbe hao ni rais wa zamani ambaye alikuwa ni kiongozi wa baraza hilo, Felix Kibodya, Brooke Montgomery ambaye alikuwa mweka hazina.
Wengine ni Lugano Mwandambo na Fatma Karume ambao walikuwa wajumbe.
Godwin Mwaipongo
Godwin Mwaipongo ni miongoni mwa wanasheria ambao majina yao yalianza kusikika katika miaka ya hivi karibuni.
Kusikika kwake si kwamba kulitokana na taaluma ya sheria tu, bali kujipambanua kwake katika medani za siasa za nchi hii.
Mwaipongo alianza kusikika katika masikioni mwa Watanzania wengi wakati wa mchakato wa kuwania nafasi ya kumpata mgombea urais atakayekiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Wakili huyo ana shahada mbili ambazo moja ni ya masuala ya sayansi ya siasa na uchumi na shahada ya pili ni sheria.
Lawrence Masha
Ingawa ametangaza kujitoa, lakini ni vizuri ikafahamika kuwa Masha ni miongoni mwa wanasheria mashuhuri nchini.
Katika jamii, Masha amejipambanua katika sura mbalimbali lakini kubwa ni sura ya uwakili pamoja na siasa.
Ndani ya sura ya uwakili, Masha amepata kuwa kiongozi wa mwanahisa wa Kampuni ya Uwakili ya IMMMA Advocates ambayo inajihusisha na huduma za kisheria hapa nchini.
Kuhusu sura ya siasa, amepata kukitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo akiwa mwana-CCM kindakindaki mwaka 2005 alifanikiwa kutwaa nafasi ya kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Nyamagana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ametumikia jimbo hilo kwa awamu moja na katika nafasi hiyo ya uwakilishi, Masha aliteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.
Wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliamua kukitosa CCM na kujiunga na Chadema.
Masha ambaye alizaliwa Machi 11, 1970 ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Tanzania Oxygen Limited.
Pia amepata kuwa mjumbe wa bodi za kampuni mbalimbali ambapo mwaka 2013 alikuwa Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni ya Tanga Cement Public Limited.
Mwaka huo huo amekuwa mjumbe wa Bodi wa Kampuni ya Fastjet Airlines Ltd.
Kuhusu elimu, Masha ana shahada ya sheria ambayo aliipata katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na kupata mafunzo ya uwakili katika Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Georgetown, Marekani.