27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

LOWASSA: WAKURUGENZI WALIOKATAA KUBADILI MATOKEO WAMEFUKUZWA KAZI

NA AZIZA MASOUD – DAR ES SALAAM

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amedai ana majina ya wakurugenzi wasiopungua 20, ambao wamefukuzwa kazi kwa kukataa kubadilisha matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka juzi.

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Lowassa amekuwa akidai kwamba, alishinda uchaguzi huo lakini kura zake ziliibwa.

Katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza Rais Dk. John Magufuli kuwa mshindi kwa kupata kura milioni 8.8, sawa na asilimia 58.47, akifuatiwa na Lowassa aliyepata kura milioni 6.07, sawa na asilimia 39.97.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, wakati akifungua  kikao cha ndani cha wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema kutoka kwenye majimbo ya Kibamba na Ubungo, Lowassa, ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu, alisema wakurugenzi hao walifukuzwa kazi baada ya kukataa kubadilisha matokeo ambayo yangepunguza kura alizopata kwenye halmashauri zao.

Alisema uchaguzi huo ulikuwa na ushindani mkubwa, hivyo kukilazimu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwalazimisha wasimamizi wa uchaguzi (wakurugenzi) kubadilisha matokeo ambayo yalikuwa yakiwapa ushindi vyama vya upinzani.

“Uchaguzi tumeshinda na wao wanajua waliiba, lakini tulishinda, wakurugenzi  wanasema walilazimishwa kubadilisha kura za Chadema wakakataa, wapo wakurugenzi wasiopungua 20 ambao majina yao  tunayo wameondolewa katika ukurugenzi baada ya kukataa kubadilisha matokeo,” alisema Lowassa.

Alisema hatua hiyo inaonyesha CCM haikushinda uchaguzi huo kihalali, isipokuwa waliiba kura.

 “Wameiba tukawaachia waendelee kutawala, wapo watu ambao wananilalamikia kwa nini sikutaka waingie barabarani, nikauliza kutatusaidia nini? Hata nikienda mikoani wanasema niliwakataza kuingia barabarani, lakini mimi siamini katika kuingia barabarani,” alisema Lowassa.

Alisema pia anaamini Chadema ina uwezo wa kutawala nchi bila vurugu wala mabavu.

Lowassa alisema ili kuweza kufikia lengo hilo, kuna haja kuhakikisha wanaondoa migogoro iliyopo katika vyama vya upinzani.

“Tumekaa na marafiki wanatuambia  Chadema itashinda, lakini acheni migogoro, katika kipindi cha uchaguzi kulikuwa na migogoro mingi, hasa Ukawa (vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi), hii ni mbaya sana, mshikamano ni muhimu, Ukawa ni muhimu, hatuwezi kuishinda CCM bila kuwa na umoja,” alisema Lowassa.

Alisema nchi zote hadi zilizopo Ulaya Magharibi zinaungana na kuondoa vyama tawala madarakani.

Alisema migogoro iliyopo katika vyama, inachochewa na Serikali, hivyo wanachama wanapaswa kuwa makini kuepuka mitego wanayowekewa.

“Ninawaomba rafiki zetu wa CUF tuelewane,  migogoro hii inachochewa na Serikali, Lipumba (Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa  Ibrahim Lipumba) nina uhakika anachochewa na Serikali atuvuruge,” alisema Lowassa.

Katika hatua nyingine, alisema serikali iliyopo madarakani inaendeleza sera za kimaskini badala ya kuleta maisha bora waliyoyahubiri  kwa wananchi wakati wa kampeni.

“Bidhaa zinapanda juu, unga umepanda, sukari imepanda, Serikali walisema maisha bora, haya ni maisha bora kweli? Watanzania wanapaswa kujua lile neno maisha bora walikuwa wanadanganywa, hii ni shida ya kutupokonya (Chadema) sera, lakini tuseme pale ambapo hawafanyi vizuri,” alisema Lowassa.

Alisema wanachama wa vyama vya upinzani wanapaswa kujipanga na kuondoa hitilafu ndogondogo zilizopo ili waweze kushika dola.

Alisema Chadema kwa sasa ni chama kikubwa, hivyo kinapaswa kuendeshwa kisiasa na si kiharakati.

“Tunapaswa kujirekebisha, watu wakianza kusema afadhali ya CCM, tutakuwa tumekwisha, CCM wajanja,  wanapanga jinsi ya kuchukua maeneo tuliyowapokonya, tunapaswa kuondoa hizi harakati na kuwa chama cha siasa ili tuweze kushika dola,” alisema Lowassa.

Alisema kwa sasa upinzani wametawala katika miji mikubwa, hivyo kuna haja ya kuilinda ili viongozi waliopo waendelee kuongoza na miaka ijayo.

“Katika uchaguzi tumechukua miji mikubwa, tuna haki ya kujivunia, miji hii tumeipata kwa jasho na  tunapaswa kuilinda kwa jasho, nimeanza kusikia maneno, madiwani hamtekelezi wajibu wenu, hamuwatendei haki wananchi kabisa,” alisema Lowassa.

Alisema kwa sasa Chadema ina kazi ya kuhakikisha wanashinda 2020, jambo litakalofanikiwa tu endapo atafanya vizuri kwa sasa.

Mbali na hilo, Lowassa alisema utawala wa sasa umekuwa ukiwatia hofu wananchi na kushindwa kutekeleza haki zao zilizopo katika Katiba, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kutoa maoni.

“Utawala huu umefanikiwa sana kutia wananchi hofu, sasa hata ukipiga simu wananchi wanahisi kama wanasikilizwa, wanaongea kwa woga, Taifa hili siyo la hofu, kila Mtanzania ana haki zake kikatiba, msikubali kutiwa hofu,” alisema Lowassa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles