25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

LISSU GUMZO UCHAGUZI TLS

Na Waandishi Wetu-

Arusha/Dar es Salaam

MGOMBEA wa nafasi ya urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu, amekuwa gumzo baada ya kuwasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) akitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Licha ya kuwa gumzo baada ya kutia nia ya kugombea nafasi hiyo na kusababisha uchaguzi huo kupingwa mara mbili mahakamani huku Serikali ikitoa kauli ya kutishia kuifuta TLS, pia kitendawili cha ama Lissu atashinda nafasi hiyo au atashindwa kitajulikana leo katika uchaguzi utakaoanza saa 12 asubuhi na kumalizika saa tatu asubuhi kwa kuchuana na wagombea wengine ambao ni Victoria Mandari, Francis Stolla, Godwin Mwaipongo na Lawrence Masha.

Aliwasili katika Ukumbi wa Simba uliopo AICC mjini hapa saa 10 jioni na kusababisha shangwe baada ya kukamatwa mjini Dodoma juzi na kupelekwa Dar es Salaam kwa kutotii sheria ya kuripoti polisi kisha akafikishwa mahakamani hapo jana.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alipandishwa mahakamani hapo akikabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kutoa maneno yenye hisia za kidini.

Lissu alifikishwa saa mbili asubuhi na kuwekwa katika chumba cha mahabusu na ilipofika saa 5:15 asubuhi alipelekwa katika chumba cha mahakama hiyo kisha kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Respicius Mwijage, upande wa Jamhuri ulisimamiwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi na Nasorro Katuga, wakati ule wa utetezi ulisimamiwa na Lissu mwenyewe.

Katika shtaka la kwanza la shauri namba 123/2017, Lissu, anakabiliwa na kosa la kutoa maneno yenye hisia za kidini na tukio hilo lilitokea Januari 11, mwaka huu, katika eneo la Kombeni Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi huko Zanzibar.

Nchimbi alidai mtuhumiwa akiwa katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani, kwa nia ya dhati alitoa maneno ambayo yangeweza kuleta uvunjifu wa amani miongoni mwa jamii ya Waislamu huko Zanzibar.

“Inadaiwa ulitamka maneno haya: Kwa hiyo hicho kinachoitwa uchaguzi wa marudio ni uharamia mtupu, haramu, haramu, haramu, kinachoitwa uchaguzi wa marudio ni haramu tupu, nyie ni Waislamu sana naomba niseme uharamu wa uchaguzi wa marudio ya mwaka jana hautofautiani na kula nguruwe kwa wala nguruwe hawa, nilikuwa nazungumzia yaliyokuja baada ya wala nguruwe hawa kufanya uharamia wao, laana tullah,” alidai Nchimbi.

Katika shtaka la pili hadi la mwisho, mtuhumiwa anadaiwa kutoa matamshi yenye nia ya kuleta uhasama.

Nchimbi alidai katika maelezo ya kosa la pili lilitendeka Januari 11, mwaka huu huko Kombeni, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, akiwa raia wa Tanzania Bara katika mkutano wa uchaguzi wa Dimani.

Nchimbi aliendelea kudai kuwa maneno aliyotamka kuwa: “Tangu mwaka 1964 Tanganyika ndiyo inayoamua nani atawale Zanzibar.” Kauli aliyodai kuwa ingeweza kuleta uhasama ndani ya Jamhuri ya Muungano.  

Katika shtaka jingine, Lissu, anadaiwa kutoa matamshi yenye nia ya kuleta uhasama ambapo katika maelezo ya kosa hilo, Nchimbi alitaja maneno yanayodaiwa kuleta uhasama kuwa:

“Tangu mwaka 1964, Zanzibar inakaliwa kijeshi na Tanganyika, nani anayebisha, tangu mwaka 1995 ikifika uchaguzi askari wa Tanganyika wanahamia Zanzibar ili kuja kuhakikisha vibaraka wao wa Zanzibar hawaondolewi madarakani na wananchi wa Zanzibar mnapigwa, mnateswa na mnauawa kwa sababu ya ukoloni wa Tanganyika kwa Zanzibar, marehemu Karume alipoanza kushtuka mwaka 1971/1972 akauawa, itakapofika tarehe 15 mwezi wa kwanza muadhimishe miaka 53 ya kukaliwa kijeshi na Tanganyika,” alidai Nchimbi.

Katika kosa la nne, Lissu, anadaiwa kutamka maneno haya:

“Jumbe aliondolewa Dodoma, Ally Hassani Mwinyi alipewa urais wa Zanzibar Dodoma na aliyempa ni Nyerere si Wazanzibari, marais wa Zanzibar wote ni Made in Tanzania, wanatengenezwa Tanganyika, wanakaa madarakani kwa sababu ya Tanganyika.” Kauli hiyo ilidaiwa ingeweza kuleta uhasama ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la mwisho, Lissu, anadaiwa kutamka kwamba: “Zanzibar inatawaliwa na Tanganyika kwa kivuli cha Tanzania, Tanzania ni Tanganyika, Tanzania ni kivuli cha kuikalia Zanzibar, cha kuigeuza Zanzibar koloni na mkoloni huwa yananyonywa, makoloni yanatawaliwa kisiasa yananyonywa kiuchumi na yanakandamizwa kijeshi, mmetawaliwa kisiasa na Tanganyika miaka yote hii, Dk. Ally Mohamed Shein hatufai tena ataondolewa kama ambavyo Aboud Jumbe alivyoondolewa,” alidai Nchimbi.

Baada ya maelezo hayo, Lissu, alikanusha makosa hayo na upande wa Jamhuri ulidai kwamba upelelezi umekamilika hivyo aliomba kuendelea kusoma maelezo ya awali kwa kuwa yalikamilika.

Alipopewa nafasi ya kwamba akubali kusomewa maelezo hayo, aliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa sababu kuna uchaguzi wa TLS jijini Arusha na angepaswa kuhudhuria.

“Mheshimiwa mashtaka haya yanadhaminika naomba nidhaminiwe, halafu leo ni uchaguzi wa TLS na mimi ni mgombea wa nafasi ya urais hivyo naomba ipangwe tarehe nyingine,” alidai Lissu.

Kwa sababu hiyo, Hakimu Mwijage, aliamua kuahirisha shtaka hilo hadi Aprili 3, mwaka huu baada ya mtuhumiwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na mdhamini mmoja atakayeweka saini ya maandishi ya Sh milioni 10.

Baadhi ya viongozi wa Chadema waliohudhuria mahakamani hapo ni pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, madiwani, mama mzazi wa msanii maarufu nchini, Wema Sepetu, Mariam na wafuasi wa chama hicho.

Baada ya kupata dhamana, alisafiri kwa ndege binafsi kutoka Dar es Salaam na alishukia Uwanja wa Ndege wa Arusha.

Akiwa amefuatana na mkewe, Lissu, aliyesubiriwa na wajumbe wa mkutano huo aliwasili bila ya watu wengi kutarajia na alielekea moja kwa moja ukumbini.

Baada ya kuingia ukumbini huku akizongwa na wajumbe, alisababisha wajumbe kulipuka kwa shangwe kwa kupiga kelele na kumwita jembe.

Kuwasili kwake kulisababisha mkutano usimame kwa dakika kadhaa ili kuruhusu utulivu na usikivu kurejea na Lissu alielekea moja kwa moja katika kiti chake.

Shangwe hizo zilimlazimu Rais wa TLS anayemaliza muda wake, John Seka, kuwatuliza wajumbe wa mkutano huo kwa kusema kuwa kitendo hicho kitawakatisha tamaa wagombea wengine.

Akizungumza ukumbini hapo, Seka, alisema muda wa kufanya kampeni ulikuwa bado hivyo wajumbe walipaswa kutulia.

“Muda wa kampeni bado, wajumbe, kitendo hiki kinawakatisha tamaa wagombea wengine,” alisema Seka.

 

TAARIFA ZA FEDHA ZAZUA TAHARUKI

Katika hatua nyingine, mkutano huo ulijikuta ukikumbwa na taharuki kutoka kwa uongozi unaomaliza muda wake baada ya wajumbe kutaka kupatiwa taarifa ya fedha ya chama hicho.

Hoja ya wajumbe hao kudai kusoma na kukabidhiwa taarifa hiyo ambayo hadi mkutano huo unaendelea ilikuwa haijakabidhiwa iliibua mjadala mrefu.

Baadhi ya wachangiaji katika mjadala huo walidai ipo hofu ya matumizi mabaya ya fedha za wanachama hao yanayodaiwa kuusukuma uongozi kuchelewesha taarifa ya fedha kwa wanachama wake.

Taarifa iliyotolewa ukumbini humo na Seka, ilidai ripoti hiyo ilikuwa haijakamilika na walitarajia ingewasili usiku wa jana.

Kuibuka kwa hoja hiyo kulikuja kabla ya wagombea nafasi mbalimbali za TLS kuanza kujinadi mbele ya wajumbe wanaotarajia kupiga kura leo.

 

Mwakyembe kufukuzwa TLS

Hoja ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, kufukuzwa uanachama wa TLS iliwagawa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho.

Pendekezo la kumfukuza Dk. Mwakyembe lilitolewa na mjumbe wa mkutano huo wa mwaka, Masha, alipochangia mada zilizowasilishwa na Dk. Erick Ng’imaryo na Dk. Hawa Sinare.

Akichangia hoja hizo, Masha, alisema TLS haiwezi kuendelea kuvumilia kuwa na mwanachama anayetishia kuifuta taasisi ambayo yeye ni sehemu ya mwanachama.

“Tangu asubuhi tumesikia kauli nzito kuhusiana na tishio la kuifuta taasisi hii ya kitaaluma. Lakini anayetishia uhai wake ni mwanachama wake. Tunawezaje kuvumilia kuendelea kuwa na mwanachama wa aina hii.

“Kwa kutumia kanuni zetu, ninawasihi wanachama wenzangu wote kwa kauli moja tumfukuze huyu mwenzetu,” alisema huku hoja yake ikipokelewa kwa makofi na mamia ya mawakili waliofurika ukumbini hapo wakiashiria kukubaliana naye.

Naye Wakili maarufu, Albert Msando, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa tishio la kuifuta TLS si la Dk. Mwakyembe peke yake bali ni uamuzi wa muda mrefu wa Serikali kutaka kuwa na taasisi isiyo na meno.

“Haja ya Serikali ni kuwa na taasisi inayojinyenyekesha kwake, taasisi isiyo na meno, ni wajibu wetu kuchagua viongozi watakaopinga haya. Viongozi watakaoboresha na kuihuisha hatuwezi kuendelea kuwa nao hasa wanaojipendekeza serikalini,” alisema Msando. 

Mchangiaji mwingine, Kalolo Bundala, naye aliunga mkono hoja ya kumfukuza Dk. Mwakyembe huku akiishauri TLS kujipanga upya ili kukabiliana na changamoto zilizopo kwa sasa.

Kwa upande wake Jaji mstaafu Tomas Mihayo, ambaye waongozaji wa mkutano huo kila walipomwita walitumia jina lake la pili la Bashite hali iliyozua vicheko na kelele kutoka kwa wajumbe, alitoa tahadhari kwa wanachama wasichukue uamuzi kwa misingi ya hisia na ushabiki na badala yake wajikite katika masuala ya msingi yanayoikabili taasisi.

“Nami nakubali kuwa tishio la kuifuta TLS ni halisi si mzaha, lakini kama mmoja wa wanataaluma hii iliyojaa watu werevu tusifikie uamuzi unaosukumwa na hisia.

“Namna pekee ya kukabiliana na changamoto hizi ni kujielekeza katika vipaumbele vyetu, hili suala la kumfukuza Dk. Mwakyembe halitatusaidia kumaliza changamoto zetu,” alisema Jaji Mihayo.

Kutokana na makofi yaliyoonyesha uelekeo wa kukubaliana na hoja ya Masha, hali ya ukumbi huo ilitaka kuchafuka baada ya mjumbe Loyd Munuo kutaka uchaguzi wa viongozi wa TLS unaotarajiwa kufanyika leo uahirishwe hadi taasisi hiyo itakapofanyiwa mabadiliko ya kimuundo.

Wakati akijaribu kujenga hoja yake, wajumbe wengi wa mkutano walipiga kelele kuashiria kutokukubaliana na maelezo yake jambo lililomlazimu kuondoka kutoka katika eneo la kuzungumzia.

“Jamani ninawasihi tuepuke migongano isiyokuwa na sababu, kama kweli tunakubaliana kufanya marekebisho katika muundo wetu basi mimi naona hakuna haja ya kufanya uchaguzi,” alisema Munuo na kukatishwa na kelele za wajumbe walioashiria kumtaka aondoke eneo hilo.

Awali, akifungua mkutano huo, Seka, alisema chama hicho bado kinaendelea na majadiliano na mamlaka za Serikali ili kutafuta njia mwafaka ya kukabiliana na tishio la kufutwa.

“Hili tishio tulishalipokea na tunaendelea na majadiliano na Serikali, kazi hiyo inafanywa na baraza letu la uongozi ili kuona njia za kuondokana nalo. Rai yangu kwenu wajumbe ni kujitathmini kwanza na kuhakikisha mnachagua viongozi watakaowafaa,” alisema Seka.

Akiwasilisha mada iliyohusu masuala ya uanachama, Dk. Ng’imaryo, alisema kuivunja taasisi hiyo ni dhahama kubwa ambayo haijawahi kutokea ikiwa ni sawa na kuvunja mtumbwi ukiwa katikati ya bahari.

“Kuna nyakati nasikia baadhi ya wanachama wakifikiria hata kuivunja TLS. Yaani tuvunje mtumbwi halafu tugawane mbao. Lakini wakati huo huo sisi tuko katikati ya bahari. Dk. Mwakyembe aliposema anataka kuvunja nilishangaa, hii si mali ya viongozi wa Serikali, ni mali ya wanachama,” alisema.

Naye Dk. Sinare aliyezungumzia masuala ya utawala bora, alitahadharisha wale wanaotishia uhai wa TLS wajiandae kukabiliana na hasira kutoka kwa wanachama ambao hawatakuwa tayari kukaa kimya.

“Ninavyofahamu hakuna aliye juu ya sheria, si waziri wala rais wa nchi, kuna wakati natafakari mtu anakamatwa kwa rushwa kisha anapelekwa mahakamani lakini aliyempa rushwa hafikishwi mahakamni. Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) lazima iangalie hili,” alisema Sinare.

 

MASHA AJITOA

Wakati wagombea wakijinadi, Masha, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya urais alisema kwa muda wa wiki mbili amejiridhisha kuwapo kwa haja ya mabadiliko ndani ya TLS na kwa hiari yake anaamini kuwa Lissu anatosha katika nafasi ya urais.

“Naamini uwezo wa Lissu katika kuiongoza TLS. Nawaomba mawakili kumpigia kura Lissu ikiwamo wale waliopanga kunichagua,” alisema Masha.

Kwa upande wake wakati akijinadi, Lissu, alisema TLS haikuwahi kusikilizwa na sasa itasikilizwa na baada ya kuomba kura baadhi ya mawakili walikuwa wakitoka nje kwa madai rais ameshamaliza kuongea.

Habari hii imeandikwa na Eliya Mbonea, Abrahamu Gwandu na Maneno Selanyika.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles