KITENDO cha Chama tawala cha zamani cha KANU kutangaza kumuunga mkono Uhuru Kenyatta ni ushindi binafsi kwa rais huyo katika azma yake ya kutetea kiti cha urais.
Hata hivyo, kinaweza pia kikawa janga kwake asipozichanga vyema karata kutokana na uwezekano wa mpasuko ndani ya chama tawala cha Jubilee kufuatia ujio huo wa KANU.
KANU inayoongozwa na Seneta wa Boringo Gideon Moi, mtoto wa Rais mstaafu Daniel arap Moi kwa mrefu ilikuwa ikitafakari upande gani iunge mkono baina ya Jubilee na muungano wa vyama vya upinzani wa NASA.
Awali mwezi uliopita Katibu Mkuu wake Nick Salat alionekana akihudhuria uzinduzi wa NASA na kutangaza kuwa KANU inajiunga nao, kauli ambayo ilipingwa na baadhi ya vigogo wa chama hicho waliosema hayo ni matamshi wake binafsi.
Hilo liliifanya KANU kuitisha Mkutano Mkuu, ambao ulimpa muda Moi kutafiti wa upande gani waunge mkono.
Kutokana na ukaribu wa baba yake Moi, na Rais Uhuru pamoja na mama wa rais, mama Ngina Kenyatta, haikushangaza kwa chama hicho kutangaza kuwa nyuma ya Rais Kenyatta.
Licha ya hiyo kuwa ahueni kwa Kenyatta maana alihofia kukosa kura nyingi kutoka jimbo tajiri kwa wapiga kura la Rift Valley, wanakotoka Moi na Naibu Rais William Ruto, changamoto zingalipo bado.
Si tu zinamkabili Rais Kenyatta bali pia naibu wake Ruto na kutishia kuipasua Jubilee, chama kilichoundwa baada ya kuvunjwa vyama vikuu vya wawili hao na vingine vidogo.
Kwa maneno mengine kitendo cha KANU kutangaza kumuunga mkono Kenyatta badala ya NASA ya akina Raila Odinga ni ushindi kwa Rais Kenyatta binafsi si Jubilee. Kwanini?.
Ni kwa sababu Ruto na washirika wake kamwe hawangekuwa tayari kusapoti ushirika huo.
Tatizo ni kwamba Ruto haelewani kabisa kisiasa na Gideon Moi na baba yake Arap Moi kutokana na kuwania ushawishi wa eneo hilo lao la Rift Valley.
Lakini pia Rais Kenyatta anafahamu fika kwa misingi ya ushawishi, ndani na nje ya Rift Valley, Ruto anamzidi Seneta wa Baringo. Kwa hivyo, anafahamu atapoteza nafasi yake ya kushinda katika uchaguzi mkuu ujao endapo wafuasi wa naibu wake watahisi kusalitiwa.
Kwa hivyo, Rais Kenyatta atahitajika kucheza karata zake za kisiasa vizuri ili Ruto na wafuasi wake, ambao tayari wameanza kulalamikia ushirika huo wasione wanatengwa. Kenyatta anahitaji bado kura zao katika jitihada zake za kurejea Ikulu katika muhula wa pili.
Lakini kwa upande mwingine, Rais kajiweka njia panda maana hangependa kwenda kinyume na matakwa ya Mzee Moi ambaye alimlea kisiasa tangu mwaka 1997 na wakati huo huo akijua KANU ina nguvu bado na ushawishi katika jamii ya Kalenjin.
Kwa sababu hiyo hatua ya KANU kutangaza kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa Agosti ni pigo kwa azma ya Ruto kuingia Ikulu mwaka huo 2022.
Aidha mwafaka kati ya Rais na mwenyekiti huyo wa Kanu, unatoa nafasi kwa chama hicho kuwasilisha kivyake wagombea wa nyadhifa nyinginezo katika uchaguzi mkuu ujao, hali inayomjenga seneta huyo wa Baringo kisiasa, hasa katika ngome ya Ruto ya Rift Valley.
Jubilee itatakiwa kutowasilisha mgombea katika kiti cha useneta wa Baringo kinachoshikiliwa na Gideon, kwa mujibu wa mkataba huo.
Katika mkataba huo, kadhalika, KANU itatengewa nafasi kadhaa za uwaziri huku wafuasi wake wakiteuliwa kushikilia nyadhifa za hadhi ya juu za ubalozi na katika mashirika ya serikali, ikiwa Rais atatetea kiti chake.
Wakati hali ikiwa hivyo, washirika wa Ruto ndani ya Jubilee wamepania kuhakikisha useneta wa Baringo unaenda kwa mtu wao, ambaye bila shaka atakuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Kudhibiti Mchezo wa Kamari (BCLB), Simon Chelugui.
Inaelezwa awali, Chelugui alikuwa akimezea mate kiti cha ugavana wa Baringo lakini Ruto akamshauri kubadili nia.
Kwa sababu hiyo huenda makabiliano makali yakashuhudiwa kati ya wafuasi wa Kanu na Jubilee hasa katika Rift Valley wakati wa kampeni “ikiwa makubaliano kati ya Rais Kenyatta na Seneta Moi yatadumishwa.
Taswira ya ushindani kati ya Kanu na Jubilee, iliyoshuhudiwa katika uchaguzi mdogo wa useneta wa Kericho mapema mwaka jana huenda ikarejea hasa katika ngome ya Naibu Rais ya Rift Valley.
Hii ni kwa sababu Ruto na Seneta Moi watakuwa wakiwafanyia kampeni wagombeaji wa vyama vyao katika majukwaa tofauti huku wakijiandaa kwa kinyang’anyiro cha 2022.