29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

WAKAZI MABONDENI SASA KUKAMATWA

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM


JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limeanza operesheni ya kuwaondoa wakazi wanaoishi mabondeni ili kuepukana na adha ya mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Hatua hiyo inatokana na kutokea kwa maafa ya vifo yaliyosababishwa na mvua zilizoanza kunyesha tangu mwishoni mwa mwezi uliopita.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema jana kuwa mvua zilizonyesha juzi zimesababisha maafa baada ya mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mongo la Ndege, Imelda Ngonyani (13), kufariki dunia wakati akivuka Mto Msimbazi eneo la Mongo la Ndege.

Alisema mwanafunzi huyo alifariki alipokuwa akijaribu kuvuka Mto Msimbazi kuelekea shuleni akiwa na wanafunzi wenzake watano.

“Tumeanza operesheni ya kuwaondoa watu wanaoishi katika maeneo hatarishi, hasa katika Bonde la Mto Msimbazi, hatuwezi kuacha watu wafe wakati tuna dhamana ya kuwalinda. Wananchi wakubali kuhama kwa hiari la sivyo tutawaondoa kwa nguvu,” alisema Sirro.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo limefanikiwa kuwaua majambazi wawili ambao walikuwa wanajiandaa kufanya uhalifu katika eneo la Kigamboni.

Kwa mujibu wa Sirro, Jumapili iliyopita saa 3:35 usiku walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu kuwapo kwa watu watatu waliopanga kufanya uhalifu katika eneo la Zimbwini Vijibweni ndipo waliweka mtego na kufanikiwa kuwakamata.

Alisema baada ya majibizano ya risasi, majambazi wawili waliuawa na polisi walifanikiwa kukamata bastola moja aina ya bereta ikiwa na risasi sita.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro alisema kuwa jeshi hilo limefanikiwa kukamata watuhumiwa 110 wa makosa mbalimbali ya uhalifu yakiwamo kupatikana na dawa za kulevya, bangi, unyang’anyi wa kutumia silaha, utapeli na kuuza pombe haramu ya gongo.

Kamada Sirro alisema walikamata kete 102 za dawa za kulevya, puli 95, misokoto ya bangi 106 na lita 10 za pombe haramu ya gongo.

Kuhusu msako wa pombe zinazofungashwa katika mifuko ya plastiki maarufu viroba,  alisema Machi 10, mwaka huu walimkamata mmiliki wa duka la kuuza vileo vya jumla na rejareja katika eneo la Banana akiwa na katoni 175 za viroba.

Alisema mfanyabiashara huyo alikutwa na katoni 155 dukani kwake na katoni 20 zilikutwa nyumbani kwake baada ya upekuzi.

Kamanda Sirro pia amepiga marufuku askari wa jeshi hilo kumwaga vyakula katika kumbi za burudani badala yake kama mtu amevunja sheria achukuliwe kwa utaratibu pamoja na vyakula vyake.

“Kila uhuru una mipaka yake, kuna klabu zina leseni na nyingine huwa zinaenda mpaka saa 11 alfajiri na huwa kuna biashara za vyakula zinaendelea. Askari wasiwazuie kwa sababu wako ndani ya utaratibu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles