LONDON, ENGLAND
KOCHA wa vinara wa Ligi Kuu nchini England, Chelsea, Antonio Conte, amedai kuwa alitoa mchango mkubwa ndani ya kikosi cha Juventus na kutwaa mataji mbalimbali, lakini hakufikia ubora wa nyota wake N’Golo Kante.
Kocha huyo amesema wakati anacheza soka ndani ya wababe wa nchini Italia, Juventus, aliweza kutwaa mataji mbalimbali kama ubingwa wa ligi kuu mara tano pamoja na mara moja Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kustaafu soka na kuwa kocha.
Kante kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji ambao wana mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho cha Chelsea tangu alipotua kwa kitita cha pauni milioni 32, mara baada ya kumalizika kwa msimu uliopita akitokea Leicester City.
Hata hivyo, mchezaji huyo wakati anaitumikia klabu hiyo ya Licester City, aliweza kutoa mchango wake mkubwa na kuhakikisha inachukua ubingwa wa ligi kuu, huku yeye mwenyewe akichukua uchezaji bora na sasa anapigania kutwaa ubingwa akiwa na Chelsea.
Chelsea leo hii wanashuka dimbani dhidi ya Manchester United kwenye mchezo wa Kombe la FA, hivyo Conte anaamini kiungo wake atatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
“Ninaamini Kante ni mchezaji wa aina yake, amekuwa na uwezo mkubwa katika safu ya kiungo, niliwahi kufanya makubwa nikiwa katika kikosi cha Juventus na kuisaidia timu hiyo kutwaa mataji mbalimbali, lakini naamini sijafikia ubora wa Kante kwa sasa.
“Naweza kusema nilikuwa na nguvu dhidi yake, lakini katika kutawala dimba bado sikuweza kufikia alivyo yeye kwa sasa, napenda kuwa na wachezaji wenye aina hii kwa kuwa mimi mwenyewe nilikuwa aina hiyo.
“Ukiwa na wachezaji wanaojituma kama Kante ni kazi rahisi kutwaa ubingwa, hivyo ninaamini tunaweza kuchukua ubingwa endapo wachezaji wengine ndani ya kikosi chetu watashirikiana na kujituma kama Kante, si tu katika kuonesha kiwango kizuri lakini pia kuwa na mchezaji kama huyo ambaye anaweza kukimbia kwa muda mrefu uwanjani,” alisema Conte.
Chelsea kwa sasa inaongoza katika msimamo wa ligi nchini England ikiwa na pointi 66 baada ya kucheza michezo 27, ikifuatiwa na Tottenham yenye pointi 56 sawa na Manchester City.