Na DENNIS LUAMBANO, DODOMA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli, amesema pamoja na utajiri wa chama hicho, bado kimeendelea kuwa ombaomba na kupokea fedha kutoka kwa watu wasiostahili.
Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo mjini hapa jana wakati wa mkutano mkuu maalumu wa CCM.
“Watu hao mnawaomba kisha wanatumia hali hiyo kuwadhalilisha. Sasa nataka kusema, chama chetu hakuna tena kuombaomba, wanaotaka kuchangia, wachangie, lakini siyo kwa kuwabembeleza na tumejipanga kutoomba kwa sababu tuna ruzuku ya kutosha ya kuweza kujiendesha,” alisema.
Pia, alisema anataka kukifanya chama hicho kijitegemee kwa kuwa kina rasilimali nyingi ambazo hazikisaidii.
“Nyinyi ni mashahidi, kwenye majengo yetu kuna wanaosema wanapangisha Sh 50,000 kumbe wanapangisha kwa Sh milioni moja. Utajiri upo na lazima uwanufaishe wana CCM wote,” alisema.
Wakati huo huo, chama hicho kimefanya mabadiliko ya 16 ya Katiba yake ya mwaka 1977, toleo la mwaka 2012 na kanuni zake.
Mabadiliko hayo yalipitishwa katika ukumbi mpya wa chama hicho wa CCM Convention Centre ambao Rais Dk. John Magufuli aliubadilisha jina na kusema kuanzia sasa utaitwa Kikwete Hall kumuenzi Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete aliyetoa wazo na kufanikisha ujenzi wake.
“Naomba sasa nitumie utaratibu kama wa Spika wa Bunge wa kuwahoji wajumbe, wanaokubali mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba waseme ndiyo,” alihoji Rais Dk. Magufuli.
Baada ya kuwahoji hivyo, wajumbe wote waliokuwa ukumbini, walijibu kwa pamoja kwa kusema ndiyo.
Awali, wakati akitoa ufafanuzi wa uamuzi wa kufanya mabadiliko madogo ya Katiba ya CCM, Rais Dk. Magufuli, alisema madhumuni ya kufanya hivyo ni kuboresha muundo na mfumo wa chama hicho.
“Wajumbe wa mkutano mkuu, naomba sasa nizungumzie suala lililotuleta hapa. Kama mnavyofahamu, chama chetu kimekuwa na utamaduni wa kujitathmini kila wakati na kufanya mageuzi ambayo yamekuwa chachu ya kukifanya kiendelee kudumu na kuzidi kuimarika na kwenda na wakati.
“Kutokana na utamaduni huo ambao umejengeka ndani ya chama chetu, Halmashauri Kuu yetu ya Taifa ilikutana Desemba, mwaka jana na kupokea tathmini ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kupitisha maazimio yenye lengo la kukiwezesha chama kutekeleza majukumu yake kuendana na mazingira ya sasa ya ushindani.
“Hii ndiyo sababu kubwa ya kuitisha mkutano huu maalumu, tumeuitisha kuwapa fursa nyinyi wajumbe kupitia marekebisho ya Katiba yanayopendekezwa, muyatafakari na ikiwezekana muyapitishe.
“Natambua kuwa Katibu Mkuu wetu, Abdulrahaman Kinana, leo (jana) atawasilisha waraka utakaofafanua kwa kirefu shabaha na maeneo tunayotaka kuyafanyia marekebisho. Kwa sababu hiyo, nitajitahidi kuelezea zaidi malengo na madhumuni tunayoyataka kuyafanya,” alisema.
Licha ya mfumo na muundo wa chama hicho kukipatia mafanikio, alisema kuna upungufu na kasoro zikiwamo mwingiliano wa majukumu baina ya taasisi za chama na jumuiya zake.
Kwa mujibu wa Rais Dk. Magufuli, mwingiliano huo, umechangia chama hicho kuwa na watendaji wengi wanaotekeleza majukumu yanayofanana na kusababisha migongano.
“Sambamba na hilo, hivi sasa ndani ya chama chetu kumeibuka vyeo ambavyo vina nguvu katika uamuzi, lakini haviko katika Katiba.
“Hivyo basi, marekebeisho ya Katiba yanayopendekezwa yanalenga kuondoa upungufu nilioutaja kuboresha mfumo na muundo,” alisema.
Alisema anataka chama kiwe na muundo mdogo wenye kuonyesha mgawanyo wa majukumu na uwajibikaji kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini na ionyeshe uhusiano kati ya chama hicho na jumuiya zake.
Alisema vyeo vyote ambavyo haviko katika Katiba ya chama hicho, vitaondolewa na ndiyo maana NEC imetoa mapendekezo ya kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi.
“Naamini mtakubaliana na mimi kuwa utendaji kazi ndani ya chama chetu ulikuwa umeshuka sana hasa uchaguzi ukimalizika na saa nyingine hata ndani ya uchaguzi kumekuwa na watu wanaokosa heshima mbele ya viongozi wa chama na mbele ya chama chenyewe.
“Mtakumbuka miaka iliyopita, watu walisimama na kuanza kuimba wana imani na mtu fulani, watu wa ovyo kweli, sasa haya nataka niyarekebishe.
“Pia, nataka kukifanya chama kiwe na watumishi wachache, lakini wenye moyo na weledi wa kukitumikia.
“Watumishi mamluki wasiruhusiwe katika chama chetu wakiwamo wale ambao asubuhi wako CCM, usiku wako chama kingine.
“Pia nataka kupunguza idadi ya vikao vya chama na wajumbe wa vikao kwa lengo la kuongeza ushawishi na kutoa fursa kwa watendaji kutumia muda mwingi kufanya shughuli za chama badala ya kushughulikia vikao ili walipane posho.
“Mabadiliko tunayoyafanya, yana lengo ya kukipeleka chama kwa wananchi kwa sababu waasisi wetu walianzisha chama hiki kwa ajili ya kuwatetea wananchi wake hususan wakulima na wafanyakazi, wafugaji na kadhalika,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Kuhusu kupunguza idadi ya vikao vya chama hicho, alisema inafanyika kushughulikia matatizo ya wananchi badala ya viongozi kufanya vikao vinavyotumia fedha nyingi huku vikitumika kupika majungu yanayokiharibu chama.
“Wale wanachama waadilifu, wenye uwezo wa kukiongoza lakini hawana fedha wamekuwa wakisukumwa nje, sasa tunataka kuwa na chama chenye watu wenye uwezo wa kuongoza na siyo wenye uwezo wa fedha.
“Pia, mabadiliko tunayokusudia kuyafanya ni pamoja na kujenga uwezo wetu wa kitaasisi ili kutumia vizuri rasilimali za chama na atakayetaka kujinufaisha, hatua kali zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.
Alisisitiza kuwa mabadiliko ndani ya chama hicho si kitu kigeni kutokana na mazingira na mahitaji.
“Najua kuna wanachama watakaoguswa na mabadiliko hayo na wengine wameguswa jana (juzi),” alisema.
Aliwataka wanachama wenzake kuwachagua viongozi waadilifu na wanaokubalika kwa wananchi katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho unaotarajiwa kuanza kufanyika mwishoni mwa Machi mwaka huu na kumalizika Novemba, mwaka huu.
Alisema wanaokusudia kugombea wasitumie rushwa na wakibainika hawatapitishwa.
Kuhusu mafanikio ya Serikali yake, alisema ametekeleza kwa vitendo nia ya kuhamia Dodoma na kusema hadi kufika mwaka 2020, Serikali yote itakuwa imeshahamia Dodoma.
Katika hatua nyingine, alitangaza mabadiliko mengine katika sekretarieti ya chama hicho kwa kumpendekeza Dk. Juma Abdallah Juma kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Mlela Hamis Silima anakuwa Katibu wa Oganaizesheni huku Dk. Frank Haule akiwa Katibu wa Uchumi na Fedha. Wajumbe wa mkutano huo, waliwapitisha viongozi hao.