25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

GWAJIMA AZIDI KUMCHIMBA MAKONDA

CHRISTINA GAULUHANGA Na PATRICIA KIMELEMETA- Dar es Salaam


ASKOFU wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amezidi kumchimba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salama, Paul Makonda, huku akijinasibu kuwa yupo tayari kutoa ushahidi dhidi ya kiongozi huyo ambaye anadai anatumia vyeti feki.

Amesema yupo tayari kuutoa ushahidi huo hadharani  pamoja na vielelezo husika.

Hivi karibuni Gwajima alidai mkuu huyo wa mkoa alitumia cheti cha Paul Christian wakati jina lake halali ni Daudi Albert Bashite.

Akizungumza kanisani kwake  Dar es Salaam jana, Askofu Gwajima, alisema kitendo cha kutumia vyeti vya watu ni kosa la jinai.

Gwajima aliwashangaa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,  Simon Sirro   na wakuu wa Idara ya Uhamiaji kwa kushindwa kumkamata Makonda ambaye alidai ametorokea  Afrika Kusini.

Alidai kitendo cha kutoroka nchini kinaonyesha wazi kuwa suala linalojadiliwa na matumizi ya vyeti feki ni kweli na ameshindwa kujitokeza hadharani kukanusha badala yake ameamua kwenda Afrika Kusini.

“Nawashangaa hawa viongozi kwa sababu wana mamlaka ya sheria ya kumkamata Makonda kwa kosa la kughushi vyeti na paspoti kwa sababu ni kosa la jinai.  Badala yake wamemua aende Afrika ya Kusini,” alisema Askofu Gwajima.

Alisema  wakati Makonda alipomtangaza kuwa ni miongoni mwa washukiwa wa dawa za kulevya,   polisi walimkamata na kumuweka mahubusu  yeye  na Mwenyekiti wa Kampuni ya Quality Group, Yusuph Manji lakini cha ajabu mpaka sasa Makonda bado yupo mitaani.

“Kwa nini wameshindwa kumkamata Makonda kwa kosa la kughushi vyeti?”alihoji.

“Mbona  mimi, Manji, Wema Sepetu na wengine tumelala mahabusu, tena kwa kosa la kusingiziwa kuwa tunajihusisha na dawa za kulevya, lakini tulitii sheria na tukaenda polisi wenyewe!” alisema.

Alisema hata maandiko matakatifu yanasema ‘heshimu mamlaka zilizopo’, jambo ambalo limewafanya kwenda polisi kwa ajili ya kuhojiwa.

Gwajima alisema  pia kuwa anaheshimu mamlaka iliyopo akiwamo Rais Dk. John Magufuli, akisema ana nia njema na watanzania.

Alisema  ikumbukwe pia kuwa wakati Magufuli anaingia madarakani, tayari Makonda alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, hivyo  ameshindwa kumtoa kwa sababu anajua ni kijana mchapakazi aliyewekwa na serikali iliyopita.

“Binafsi namkubali Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya, suala la vyeti, la Makonda, hawezi kulijua kwa sababu alimkuta madarakani, hakujua kama ni mzigo… kwa sababu amenipiga nami nampiga mara 100,” alisema.

Alisema kuna watu wanamshangaa kwa nini anazungumzia habari za Makonda ndani ya nyumba ya Mungu bila kujiuliza kauli ya mkuu huyo kumuhusisha yeye na dawa za kulevya imevunja mioyo watu wangapi na  imewakimbiza wangapi kuabudu.

“Nikisema ninyamaze kuongea wapo watu wanaotumika na huyu Bashite kwa kupewa vijipesa na kuongea jambo ambalo linanifanya nizidi kutibuka,”alisema Gwajima.

Alisema matatizo yanayomkuta Makonda katika kipindi hiki ni damu za watu aliowanyanyasa na kuwadhalilisha… inamlilia.

Gwajima alisema  tangu Makonda alipochaguliwa kuwa mkuu wa wilaya hadi mkuu wa mkoa, amekuwa akiwadhalilisha viongozi mbalimbali wa serikali wakiwamo waliomzidi elimu.

Alitoa mfano wa  baadhi ya viongozi waliodhalilishwa na Makonda kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa jiji, Wilson Kabwe.

Gwajima alisema     Makonda aliwahi kuwaweka mahabusu watendaji wa ardhi wa Manispaa ya Kinondoni kwa madai kuwa walichelewa kwenye kikao.

Akizungumzia kuhusu chanzo cha vyeti feki, Gwajima alisema jina halali la Makonda ni Daudi Albert Bashite.

Alidai jina analotumia sasa  alichukua cheti kwa kijana mmoja ambaye binamu yake alikuwa na uhusiano naye wa  mapenzi.

Gwajima alidai  baada ya kushindwa shule ya msingi Kolomije na sekondari ya Pamba, Makonda alimshawishi huyo dada  ampatia cheti cha kaka yake   aweze kujiunga na Chuo cha Uvuvi Nyegezi.

Alisema  baba yake mzazi yupo hai hadi sasa anaitwa na Albert Bashite ambaye aliwahi kuwa mwanajeshi na kupigana vita vya Idd Amin mwaka 1977 hadi 1979.

Alisema wakati huo mzee huyo alikuwa akiishi katika  kijiji cha Kolomije Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza na ni jirani na mzee Gwajima (baba mzazi wa askofu Gwajima).

Alisema Daudi alisoma shule ya msingi Kolomije hadi alipofika darasa la nne ambako alishindwa mtihani na kuchukuliwa na shangazi yake kwenda kuishi mjini Mwanza.  

Gwajima alisema shangazi yake huyo aliolewa na Meya wa jiji hilo,  Suleiman Kamese ambaye alimchukua Daudi na kumpeleka darasa la tano hadi la saba  katika Shule ya Msingi Nyanza ambako nako alishindwa.

Alisema katika kipindi cha kutafuta maisha, Makonda alishawahi kuwa kondakta wa daladala iliyokua inafanya kazi Misungwi  – Sumve.

Alisema gari hiyo ilikua inamilikiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Marehemu Clement Mabina.

Alisema anakumbuka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ilipotangaza majina ya wanafunzi 8,436 wasio na sifa kwa mwaka 2016/2017.

“Najiuliza kama hawa zaidi ya 8,000 waliondolewa katika vyuo 52 na Serikali bila kujali imepoteza fedha kiasi gani ndiyo ije huyo mmoja Makonda?”alisema Gwajima.

Alisema ‘ukitaka taifa lisonge mbele ni lazima ukodoe macho na maskio yote yawe wazi kusikiliza huku na kule’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles