Na AGATHA CHARLES,
NYUMBA zaidi ya 250 zilizopo ndani ya mita 30 kutoka ilikopita reli ya kati jijini Dar es Salaam, ukiwamo ukuta wa kiwanda cha mfanyabiashara maarufu Said Salim Bakhresa, zimebomolewa.
Bomoabomoa hiyo ilianza majira ya saa 10 alfajiri chini ya Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco) kupitia kampuni ya udalali ya Heputwa Investment.
MTANZANIA Jumapili ambalo lilikuwa eneo la tukio, lilifanikiwa kuona namna wananchi, hasa maeneo ya Buguruni, walivyokuwa wakihangaika kuokoa baadhi ya mali zao ili kupisha ubomoaji huo ambao walidai hawakuwa na taarifa nao.
Askari polisi waliokuwa na mabomu, silaha na gari la maji ya kuwasha, walitanda katika eneo hilo kuhakikisha kuwa ubomoaji huo unaendeshwa bila kutokea pingamizi au vurugu kutoka kwa wananchi.
Mmoja wa wananchi waliopitiwa na bomoa bomoa hiyo, Ramadhan Mbwana, mkazi wa Buguruni kwa Mnyamani, alisema Februari 5 mwaka jana, Rahco walifika eneo hilo wakiwa na Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa na kuwataka wawepo kuhakikisha futi inavyopimwa hadi mwisho wa nyumba.
Mbwana alisema vipimo hivyo viligusa eneo dogo la banda (nyumba) lake na alipatiwa notisi ya siku 30 ili kuvuja jambo ambalo alilitekeleza.
“Agosti 6 au 7, walifika kuweka alama ya mawe kuonyesha kuwa ile ndio hifadhi ya reli.
“Lakini katika hali ambayo si kawaida, Februari 16, Rahco wakiwa na ulinzi wa polisi walikuja na kupima mita 30. Tukahoji mbona tayari walishawekwa alama? Wakasema tuongee na wakubwa na kupata ufumbuzi wake.
“Sisi tukaunda kamati baada ya siku kadhaa na mimi ni mjumbe, tukaenda Rahco wakatutaka tuandike barua na kuambatanisha vielelezo vya namna tunavyoishi eneo hili,” alisema Mbwana.
Alisema eneo hilo lina leseni za makazi ambazo ziko hai na kuna ambao wana hati kamili walizozitoa ardhi, akiwamo jirani yake ambaye alizimia wakati wa bomoa bomoa hiyo.
Mbwana alisema baada ya kupeleka vielelezo, walitakiwa kusubiri.
Hata hivyo, suala hilo walilifikisha Kitengo cha Haki za Binadamu ambako Rahco walipatiwa siku saba kujieleza.
“Machi 14 tunakutana na mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu ili tukae meza moja na Rahco kama walivyotutaka kupitia barua yao. Lakini wakati tukisubiri hilo, ndipo tulishangaa jana usiku wa saa 10 tunatumiwa ujumbe mfupi wa simu kuwa tutoe vitu kwani wanafika kubomoa,” alisema Mbwana.
Alisema nguvu kubwa imetumika kuwahamisha ingawa rai yao ilikuwa ni kuona wanawezeshwa kwani wamekaa tangu miaka ya 1960 na walirithishwa kutoka kwa wazazi wao.
Naye mkazi wa Buguruni, Anitha Joseph, alisema hawakuwa na taarifa za ubomoaji huo ambao umesababisha nyumba yao ya vyumba vinne kubomolewa pamoja na fremu ambazo walizitumia kwa biashara.
MTANZANIA Jumapili lilipozungumza na Diwani wa Kata ya Mnyamani, Shukuru Dege kuhusu bomoa bomoa hiyo, alisema hakuwa na taarifa rasmi.
“Kama ofisi sina taarifa zozote wala notisi ya lini wanabomoa, ninachofahamu hawa watu walikuja Februari 15, mwaka huu na watu wenye bunduki. Wakati huo nilikuwa halmashauri nikapigiwa simu kuwa kuna watu wanapita relini na askari wanaweka alama ya X.
“Nilimuuliza Mkurugenzi wa Manispaa iwapo analifahamu jambo hilo, akasema hajui na hata Mstahiki Meya akasema hana taarifa,” alisema Dege.
Alisema anachokitambua ni kuwa awali baada ya Rahco kupita walijikusanya na kuunda kamati ili kushughulikia jambo hilo na Jumanne ya wiki hii wanakwenda kuonana na Mkurugenzi wa Rahco na mwanasheria wake kwenye Tume za Haki za Binadamu.
“Lakini ajabu ni kwamba jana (juzi) usiku saa sita nikapokea ujumbe kutoka kwa mtu ambaye yuko kwenye zoezi hilo, aliniambia diwani jiandae na watu wako tunaanza kuvunja kuanzia alfajiri. Kweli wakaanza.
“Zoezi limekiuka haki za binadamu kwa kuwa wananchi hawakuwa na taarifa, maana tuliwaambia Rahco sisi hatugomei maendeleo, lakini kama tuna haki ya kulipwa fidia tulipwe watu wahame,” alisema Dege.
Alisema bomoa bomoa hiyo imehusisha nyumba zaidi ya 80 katika kata yake na hivyo kaya nyingi hazina mahali pa kulala wala kufanyia biashara ili kupata kipato.
MTANZANIA Jumapili lilizungumza na Meneja wa Operesheni hiyo, Idd Kebwe ambaye alisema taratibu zote zilifuatwa.
“Wote walio ndani ya hifadhi ya reli tunawaondoa ili kupisha ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge).
Zoezi hili tumelianzia Station huko mjini na litakwenda hadi mikoa ya mwisho wa reli, ikiwemo Mwanza,” alisema Kebwe.
Alisema walitoa taarifa na siku 30 za watu kujiandaa kabla ya bomoa bomoa na kwamba ndiyo maana hakukuwa na vurugu wakati bomoa
bomoa hiyo ikiendelea jana.