24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MAKATIBU 30 CCM WATOSWA NEC

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa mkoani Dodoma jana.

Na Dennis Luambano – Dodoma

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema makatibu wa mikoa wa chama hicho ambao idadi yao inafikia 30, hawana ulazima wa kuwa wajumbe wa Mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa (NEC).

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika Ukumbi wa CCM wa White House wakati akifungua Mkutano wa NEC.

Dk. Magufuli ambaye pia ni rais wa nchi, alisema walikutana jana kwa kazi maalumu waliyoianza Dar es Salaam, ambayo lazima waikamilishe ili leo wawasilishe ripoti katika Mkutano Mkuu Maalumu Taifa wa CCM.

Mkutano huo unakusudia kufanya marekebisho ya katiba ya chama hicho ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2012, kanuni zake na jumuiya zake. Pia utapokea taarifa ya ratiba ya uchaguzi mkuu wa chama hicho na jumuiya zake utakaofanyika mwaka huu nchi nzima.  

“CCM ni chama kikubwa na kikongwe barani Afrika, mara ya mwisho tulikutana Dar es Salaam Desemba 13, mwaka jana, leo (jana) tena tumekutana hapa.

“Tumeshawahi kufanya mabadiliko mengi siku za nyuma, sitarajii kama tutajadili sana, sitarajii kama mkutano huu utakuwa mrefu,” alisema Dk. Magufuli.

 Aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa anaamini yote waliyojadili yatapitishwa kwa sababu mabadiliko ndani ya CCM ni jambo la kawaida.

“Nimeambiwa na katibu mkuu kwamba chama tawala cha China kina wajumbe wa NEC yao 205, licha ya kwamba nchi nzima ina idadi ya watu bilioni moja, ANC cha Afrika Kusini kina wajumbe 110, lakini sisi tupo 163, mabadiliko ni kitu kizuri.

“Wapo wengine walikuwa wanazungumza na nataka niliseme hapa, makatibu wa CCM wa mikoa ni vyema lazima wawepo hapa, nawaambia sio lazima wawepo hapa, hata serikalini huwa kuna mawaziri wana vikao vyao, pia kuna vikao vya makatibu wakuu.

“Kuna wengine walisema wakikosekana hao nitakosa wawakilishi, nikawaambia mbona miaka iliyopita walizomea humu kikaoni, mbona hawakusimama hata kupigana, walipokuwa wakiimba wana imani na mtu fulani mbona walikuwepo, mwenyekiti alikuwa anawalipa mishahara, lakini bado walimwimbia kwamba wana imani na mtu fulani.

“Nataka kulizungumza hili kwa uwazi, kwamba makatibu wa CCM ni waajiriwa, anayetaka lazima awepo humu akagombee uenyekiti, nataka kulizungumza hili kwa uwazi ili kusudi tukubali mabadiliko tunayoyataka,” alisema.

Dk. Magufuli alisema wapo wengine wanazungumza wajumbe wa NEC wa wilaya ni lazima wawepo katika vikao. Vyeo ndani ya CCM vimekuwa vingi mno.

“Kwenye taarifa za awali, waliogombea ubunge, 85 ni wajumbe wa NEC na saa nyingine tunadhoofisha juhudi zinazotakiwa kufanywa kwenye majimbo na wabunge, mbunge yuko huku anatetea, mjumbe wa NEC anazunguka kila mahali, si nafuu ukae usubiri ugombee, ninajua maneno haya saa nyingine yanawagusa, lakini napenda kuzungumza ukweli, kwa hiyo ni lazima tujipange katika kufanya mabadiliko.

“Wajumbe wa NEC vyeo ni vingi, nililizungumza wala wasiwe na wasiwasi, sisi ndio watawala, sisi ndio Serikali na ushahidi unajulikana kwa sababu wengine nishaanza kuwachukua chukua.

“Tukubali mabadiliko kwa ajili ya chama chetu na kwa faida ya chama chetu na hiki chama ndio kila mmoja anakitazama, leo (jana) hapa tuko katika kikao, Chadema wanatuangalia, CUF wanatuangalia hata ambao sio wanachama nina uhakika watakuwa wamejaa katika televisheni wanaangalia CCM wanafanya nini kwa sababu chama hiki ni kikubwa.

“Hivyo ni lazima tufanye mabadiliko makubwa kwa faida ya chama chetu na kwa faida ya taifa letu, nawakaribisha kutoa uamuzi mtakaoona unafaa kwa faida ya chama chetu na mwelekeo mpya wa chama chetu,” alisema.

Dk. Magufuli aliingia katika mkutano huo saa 12:18 mchana na kukuta idadi ndogo ya wajumbe na ilimlazimu awasubiri wengine waingie hadi saa 12:32 mchana.

Awali, baada ya wajumbe wasiokuwapo kuingia ukumbini, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, alisema baada ya wajumbe wengine kuteuliwa katika nafasi mbalimbali serikalini, mkutano huo wa NEC una wajumbe 382 na waliohudhuria jana walikuwa 376, hivyo akidi ilitimia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles