30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

TAHARUKI CCM, YAMTIMUA SOPHIA SIMBA NA WENGINE 11, YAONYA WANNE, BASHE, MSUKUMA, MALIMA WAKAMATWA, WAHOJIWA, WAACHIWA

Dennis Luambano Na RAMADHAN HASSAN-Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimewafukuza wanachama wake 12, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba, ambaye wiki iliyopita alitangaza kutogombea tena nafasi hiyo.

Sophia ambaye kwa sasa atalazimika kupoteza ubunge kutokana na uamuzi huo, amefukuzwa baada ya kupatikana na makosa ya maadili kinyume na Katiba na kanuni za chama hicho.

Mbali na ubunge ambao ameutumikia kwa takribani miaka 22, pia atapoteza nafasi yake ya uenyekiti wa UWT aliyoitumikia kwa muda wa miaka 10.

Akitoa taarifa ya Mkutano wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa (NEC) kwa waandishi wa habari, uliofanyika mjini hapa jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepele, pasipo kufafanua, alisema Sophia alipatikana na hatia ya makosa ya kiuadilifu ya chama hicho.

“Wajumbe wa NEC kwa sauti moja wameridhia kumfukuza uanachama Sophia Simba,” alisema Polepole.

Mbali na Sophia, pia alisema wenyeviti wa CCM wa mikoa minne nao wamefukuzwa kwa makosa kama hayo.

Aliwataja wenyeviti hao na mikoa yao katika mabano kuwa ni Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga), Ramadhan Madabiba (Dar es Salaam) na Christopher Sanya (Mara).

Polepole aliwataja wanachama wengine waliofukuzwa kuwa ni Willfred ole Mollel ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini, mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Babati Mjini, Ally Sumaye na Mathias Manga wa Wilaya ya Arumeru.

Katika orodha hiyo, pia wamo wenyeviti wa wilaya wa chama hicho ambao ni Omari Awadhi (Gairo), Ally Msuya (Babati Mjini), Makolo Laizer (Longido) na Salumu Madenge (Kinondoni-Dar es Salaam).

 “CCM imeanza safari ya mageuzi na kuna watu walikuwa wanasema hatuchukui hatua, sasa tumeanza kuchukua kwa watu waliokihujumu chama na waliokisaliti na kukifanya kinuke mbele ya wananchi.

 “Leo (jana) tumechukua uamuzi kwa baadhi ya wanachama na huu ni mwanzo tu wa kuelekea katika mageuzi, vikao vya chama havitakuwa na hajizi ya kuchukua hatua kwa mwanachama au kiongozi yeyote anayekwenda kinyume,” alisema.

Polepole pia aliwataja wanachama wengine waliochukuliwa hatua baada ya kufanya makosa kama hayo kuwa ni Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye amepewa onyo kali na anatakiwa kuomba radhi.

Wakati Nchimbi akipewa onyo, Adam Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mbunge wa Afrika Mashariki yeye amesamehewa.

“Nchimbi yeye ni balozi nchini Brazil, amepewa onyo kali na anatakiwa kuwaomba radhi wanachama, chama na viongozi na kwa kuwa yuko Brazil tutapokea radhi yake kwa njia ya maandishi kutoka uko aliko na Kimbisa baada ya kuchunguza mwenendo wake amesamehewa, adhabu zote hizi zimeanza kutekelezwa leo (jana),” alisema Polepole.

Ingawa Polepole hakufafanua sababu za kumfukuza uanachama Sophia, kumpa onyo kali Nchimbi na kumsamehe Kimbisa, wanachama hao ndio waliojitokeza hadharani kupinga uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM iliyoketi kupitisha majina ya wagombea urais kupitia chama hicho mwaka 2015.

Itakumbukwa, Nchimbi, Kimbisa na Sophia walipinga kitendo cha kamati ya maadili chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wake Rais Mstaafu Jakaya Kikwete cha kukata majina ya wagombea urais likiwamo la aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na kupeleka majina matano tu yajadiliwe ndani ya kamati hiyo.

Wanasiasa hao walidai kuwa kanuni za chama hicho zilikuwa zimepindishwa. 

Mbali na hilo la akina Nchimbi, wengine waliopewa adhabu jana ni Ali Mchumo ambaye ni mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Kilwa (amepewa onyo kali), Ajili Kalolo ambaye ni mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Tunduru (ameachishwa uongozi).

Yumo pia Hassan Mazala (ameachishwa uongozi), Valerian Buretta ambaye ni mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Kibaha Vijijini (ameachishwa uongozi).

Wenyeviti wa wilaya wa chama hicho waliopewa adhabu ni Abeid Kiponza wa Iringa Mjini (ameachishwa uongozi), Assa Haroun wa Ilala (ameachishwa uongozi), Hamis Nguli wa Singida Mjini (ameachishwa uongozi) na Muhaji Bushako wa Muleba (amepewa onyo kali).

“Utaona wengine wamepewa onyo kali ambalo unakuwa chini ya uangalizi kwa muda wa miezi 12 na unapoteza sifa ya kushiriki shughuli zozote za chama ikiwamo uchaguzi wa ndani.

“Wengine wameachishwa uongozi baada ya kukiuka maadili na kutishia uhai wa chama, kiburi jeuri na hushauriki na hufuati maelekezo ya chama.

“Maana yake ni kwamba watakuwa chini ya uangalizi kwa miezi isiyopungua 30 na wanapoteza sifa ya kugombea katika uchaguzi na kufanya chochote kile ndani ya chama, masuala ya kimaadili ndani ya chama chetu sio ya kuyafanyia mchezo na vikao vilivyotoa uamuzi huu ni vya mwisho na hakuna rufaa,” alisema Polepole.

Aliwataja wengine kuwa ni pamoja na mbunge na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Kigoma, Josephine Genzabuke ambaye amepewa onyo kali.

“Wanatakiwa kukabidhi mali za chama na hata kama wengine wako njiani wanakuja katika mkutano wa kesho (leo) hawataruhusiwa kuingia,” alisema.

Katika hatua nyingine, Polepole, alisema NEC imeridhia ratiba ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho utakaonza kufanyika mwishoni mwa Machi na kumalizika mwanzoni mwa Novemba, mwaka huu.

Pamoja na hilo, alisema pia imeridhia kuundwa kwa kamati ndogo itakayokuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula, kwenda Zanzibar kuangalia hali ya siasa na kufanya tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

 “Baada ya huku Bara kazi hiyo kumalizika kwa mikoa 25, sasa hiyo kazi inahamia Zanzibar,” alisema.

 Aliwataja miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni Pandu Amiri Kificho, Daud Ismail, Shamsa Vuai Nahodha, Dk. Maua Daftari, Steven Wasira na Zakhia Meghji.

BASHE, MSUKUMA WAKAMATWA

Wakati hayo yakitokea, Jeshi la Polisi mkoani Dodoma limewakamata wabunge wawili wa CCM, Hussein Bashe wa Nzega Mjini na Joseph Kasheku ‘Msukuma’ wa Geita kwa kile kinachodaiwa ni njama za kutaka kuvuruga Mkutano Mkuu wa chama hicho unaofanyika leo.

Mbali na wabunge hao, mwingine aliyekamatwa ni Adam Malima ambaye amepata kuwa mbunge wa Mkuranga na Naibu Waziri katika wizara mbili tofauti; Fedha na Nishati na Madini katika Serikali ya awamu ya nne.

Taarifa za kukamatwa kwa viongozi hao zilianza kusambaa jana saa 12:44 jioni kabla ya baadaye kuthibitishwa na Jeshi la Polisi mkoani Dodoma.

Akizungumza kwa simu na MTANZANIA Jumapili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alikiri kuwashikilia viongozi hao.

Kamanda Mambosasa ambaye alizungumza na gazeti hili kwa nyakati mbili tofauti – saa 1:00 na 2:00 usiku, alisema jeshi hilo lilikuwa likiwashikilia viongozi hao kwa mahojiano.

Alisema viongozi hao walikamatwa jana nje ya ukumbi wa mikutano wa CCM, White House wakati mkutano wa Halmashauri Kuu ukiendelea.

Kamanda Mambosasa alisema sababu kubwa ya kukamatwa kwao ni kudaiwa kutengeneza njama za kutaka kuvuruga mkutano huo.

 “Ni kweli tumewakamata leo (jana), sababu kubwa ni njama za kutaka kuvuruga mkutano, tumewakamatia nje ya ukumbi wa CCM,” alisema.

 Alipoulizwa walijuaje wanafanya njama za kuvuruga mkutano huo, Kamanda Mambosasa alisema wamejua kupitia vyanzo vyao.

“Wote hao tunawahoji, taarifa tumepata kupitia vyanzo vyetu,” alisema Kamanda Mambosasa ambaye hakutaka kuelezea kwa undani jambo hilo.

Hata hivyo, wakati gazeti hili likielekea mitamboni saa 3:50 usiku, Bashe na wenzake walikuwa wameachiwa baada ya kuhojiwa kwa saa kadhaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles