JUBA, SUDAN KUSINI
JENERALI wa Jeshi la Sudan Kusini, ambaye alijiuzulu mwezi uliopita, ametangaza kuunda kundi jipya la waasi linaloipinga Serikali na hivyo kuzidisha shinikizo kwa utawala wa Rais Salva Kiir.
Luteni Jenerali Thomas Cirillo Swaka, ambaye alikuwa naibu mkuu wa lojistiki, alijiuzulu baada ya kumtuhumu Kiir kuligeuza jeshi la nchi kuwa la kikabila.
Alisema kuwa jeshi, polisi na matawi mengine ya usalama, kwa kiasi kikubwa yamejaa watu kutoka kabila la Dinka analotoka Kiir.
Swaka alikuwa mmoja wa maofisa watatu waandamizi wa jeshi waliojiuzulu Februari mwaka huu wakituhumu ukabila, upendeleo, rushwa na ukiukaji mwingine unaofanywa na Serikali ya Kiir,
Katika taarifa yake mwanzoni mwa wiki, Swaka alisema kundi kubwa la waasi – The National Salvation Front (NSF), limedhamiria kurudisha amani na utulivu Sudan Kusini na kwamba Kiir lazima ang’oke.
Taifa hili tajiri kwa mafuta, ambalo ndilo changa zaidi Afrika, liliingia katika vita yake ya kwanza mwaka 2013 baada ya Kiir kumfukuza kazi naibu wake na hasimu wa kisiasa, Riek Machar.