32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

AFRIKA KUSINI NI ZAIDI YA WAHAMIAJI

Wancnchi wa Afrika kusini wakiandamana

Na MARKUS MPANGALA,

MAMIA ya wananchi wa Afrika Kusini wapo kwenye kampeni kubwa ya kuwafukuza raia wa kigeni katika nchi yao kwa madai mbalimbali. Maandamano makubwa yamekuwa yakifanyika katika Jiji la Pretoria na Mji wa Jeppestown, ambako raia wa kigeni wamekumbana na wakati mgumu.

Taarifa zinasema kuwa, wananchi wa nchi hiyo wamekuwa wakitumia ajenda ya kuilinda nchi yao kama nyenzo ya kuwafukuza wageni kwa sababu wamekuwa chanzo cha matatizo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa pamoja na umasikini unaowakabili.

Aidha, wananchi hao wamedai kuwa, wageni wamekuwa chanzo cha ukosefu wa ajira miongoni mwao, pamoja na ongezeko la uhalifu katika miji mbalimbali ya Afrika Kusini.

Hatua ya kuwafukuza wageni hujulikana kama ubaguzi dhidi ya wageni au ‘Xenophobia’. Kuwafukuza raia wa kigeni nchini Afrika Kusini kumetokea mara nyingi, hali ambayo imewahi kudhoofisha uhusiano kati ya taifa hilo la kusini mwa Afrika na jirani zake kama Zimbabwe, Botswana, Swaziland pamoja na Nigeria, Pakistan, ambapo raia wake wengi wamekuwa wakiishi nchini Afrika Kusini.

Hii ni mara ya tatu kushuhudia mashambulizi dhidi ya wageni. Mwaka 2008 zaidi ya watu 60 walifariki dunia, huku wengine 50,000 wakilazimishwa kuyakimbia makazi yao kutokana na vuguvugu la kuwashambulia wageni (Xenophobia), sababu zikiwa ni zilezile tulizoeleza hapo juu. 

Mara ya pili vuguvugu la kuwafukuza wageni lilitokea mwaka 2015, kabla ya jeshi la polisi kuzima mpango huo. Hii ina maana juhudi za Waafrika Kusini kuwafukuza wageni zinaendelea na huenda zikadumu kwa kizazi kijacho pia.

Kampuni zinazomilikiwa na wageni nchini Afrika Kusini zimejikuta kwenye mashumbulizi ambapo wananchi wanadai wamekuwa chanzo cha wao kukosa kazi.

Inaelezwa kuwa, kampuni mbalimbali kutoka Nigeria zimekuwa zikilengwa na washambuliaji ambao wamekuwa wakihamasisha kuwafukuza wageni kwa madai wanasababisha ukosefu wa kazi kwa wenyeji.

Licha ya ushirikiano wa kibiashara na uchumi baina ya sekta binafsi na umma kati ya Nigeria na Afrika Kusini, bado mamia ya wananchi waliandamana na kushambulia maeneo yote yaliyodaiwa kuwa yanamilikiwa na wageni.

Kwa mujibu wa takwimu za Kamati ya Ushirikiano wa kibiashara kati ya Afrika kusini na Nigeria, SA-NCC (South Africa-Nigeria Chamber of Commerce (SA-NCC: “Jumla ya faida ya kibiashara kati ya Afrika Kusini na Nigeria imekuwa ikikua mwaka hadi mwaka, kutoka randi milioni 174 mwaka 1999 hadi randi bilioni 3 mwaka 2008, na randi bilioni 66 kwa mwaka 2014.

Uwiano huo wa kibiashara umeisaidia Nigeria kama msafirishaji mkuu wa mafuta nje ya nchi, ikiwa na thamani ya randi bilioni 38.5 mwaka 2015. Ndiyo kusema malalamiko ya wananchi wa Afrika Kusini hayaendani na uhalisi wa mambo.

Kutokana na hali hiyo, nao wananchi wa Nigeria walilazimika kuandamana hadi makao makuu ya kampuni ya MTN na kuitaka ifunge ofisi zao kurejea Afrika Kusini, ikiwa ni njia ya kulipa kisasi kwa Afrika Kusini.

IDADI YA WAHAMIAJI IKOJE?

Upo ukweli mwingine ambao wananchi wa Afrika Kusini wanatakiwa kuujua. Takwimu zinaonyesha kuwa, wahamiaji milioni 2.3 wanaishi Afrika Kusini.

Idadi hiyo ni pamoja na watu kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, China, Bangladesh, India, Mashariki ya Kati na Ulaya, ambao hawakuzaliwa nchini Afrika Kusini.  

Watu wengine milioni 1.6 ni Waafrika ambao huendesha shughuli zao za biashara ndogo za maduka, huduma viwandani, uchuuzi na kadhalika.

Pia, hawana uwezo wa kumiliki sehemu ya utajiri uliopo Afrika Kusini. Asilimia 8.7 yao ni watu wa jamii ya Kizungu wenye uraia halali wa Afrika Kusini. Wazungu hao wanamiliki uchumi wa nchi hiyo kwa asilimia 85.

Watu weusi wamekuwa kwenye vyeo mbalimbali, mameneja, wakurugenzi, wafanyakazi na wengineo. Kuna familia 6,000 za watu kutoka Ulaya ambao wanamiliki asilimia 85 ya ardhi ya Afrika Kusini.

Ndiyo kusema wahamiaji hao hawamiliki ardhi yoyote, hawamiliki migodi ya madini, hawamiliki kampuni za uwindaji, hawamiliki kampuni za meli wala mabenki. Ndiyo kusema wananchi hao wanapambana na adui asiye sahihi.

UDHAIFU WA SERIKALI

Awamu ya pili ya Rais Jacob Zuma imekutana matatizo lukuki ambayo hayajatatuliwa hadi leo. Ndani ya chama tawala cha ANC kuna matatizo makubwa ya kiuongozi ambapo mnyukano wa ndani pamoja na kuelemewa kashfa za ubadhirifu kumesababisha chama hicho kushindwa kudhibiti na kufanya uamuzi sahihi ya kiuongozi.

Jacob Zuma amelazimika kubadilisha baraza la mawaziri mara kadhaa. Zuma amenusurika kung’olewa madarakani mara mbili na Bunge, ikiwa ni ishara ya kushindwa kuwatumikia wananchi na badala yake ANC na Rais wanajikuta kwenye mapambano ya kisiasa badala ya kutatua kero za wananchi. Zuma anachuana na makamu wake, Cyril Ramaphosa.

Ramaphosa alitajwa kuhusika katika kashfa ya ubadhirifu kabla ya kukanushwa na makamu huyo wa rais.

Hata hivyo, uchunguzi wa Fica (Financial Intelligence Centre Amendment) unaendelea na kuwaweka katika wakati mgumu wanasiasa wakubwa wawili ndani ya ANC, Zuma na makamu wake, Ramaphosa.

Ikumbukwe mwaka 2016 ilipotolewa ripoti ya kashfa ya Nkandla chini ya uenyekiti wa Thuli Madonsela, ilisababisha kupigwa kura za kuamua kumbakisha madarakani Rais Zuma ama kumng’oa, hali ambayo imejikuta serikali na chama kuyumba.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya mashirika ya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles