25.4 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

WASANII WANANGUVU KULIKO VYAMA VYA SIASA

Na ALLY KAMWE,

MIONGONI mwa watu wenye ushawishi katika jamii ya Kitanzania pengine na maeneo mengine duniani ni wanamuziki, wasanii, warembo na wanamichezo.

Kwenye chaguzi za vyama vya siasa tumeshuhudia wanasiasa mbalimbali wakiwatumia wasanii, warembo au wanamichezo kuongeza joto la uchaguzi pamoja na ushawishi kwa wapiga kura.

Uchaguzi wa Marekani wa mwaka jana ni miongoni mwa mifano hai. Tuliona wanamuziki kama Beyonce Knowles, Shawn Carter au maarufu kwa jina la Jay Z wakimpigia kampeni aliyekuwa mgombea wa chama cha Democrat, Hillary Clinton, wakati nguli wa hip hop, Kanye West, alimpigia kampeni aliyekuwa mgombea na mshindi wa kiti cha urais wa nchi hiyo, Donald Trump.

Hapa nchini tuliona pia makumi ya wanamuziki, waigizaji wa filamu na warembo walioshiriki mashindano ya Miss Tanzania wakijumuika katika zoezi la uchaguzi mkuu kwa kuvipigia kampeni vyama walivyokabidhiwa jukumu hilo.

Miongoni mwao alikuwamo Wema Sepetu. Hatuwezi kusema yeye ni mwigizaji kama marehemu Mzee Kipara, Bi Kidude. Wema si mwanamuziki kama akina Zay B, Sister, Da Jo au Lady Jay Dee.

Utambulisho wake unatosha kusema yeye ni Miss Tanzania mwaka 2006, japo pia itakupasa kulisema hili huku paji la uso ukilielekeza ardhini, ni aibu.

Ndiyo, ni aibu kumtaja Wema kwenye orodha ambayo ndani yake kuna jina la Nancy Sumari, mshindi wa Miss World Africa, mwaka 2005.

Zaidi ya miaka 10 sasa, Watanzania wameendelea kumpenda, kumjali, kumwamini na kumpigania Wema kwa kila hali, japo hawaelewi anafanya nini kinachowafanya wawe hivyo.

Yatupasa kumpongeza Wema huku tukijiuliza anawezaje kuishinda mioyo migumu ya Watanzania kirahisi namna hii? Lililo gumu kwenye fikra zetu, yeye atalifanya kwa njia nyepesi na kwa urahisi zaidi.

Vanessa Mdee ni mwanamuziki hodari, lakini cha ajabu hafiki hata theluthi ya ukubwa na heshima aliyonayo Wema Sepetu kwa Watanzania.

Nini kipo kwa Wema? Anafanya lipi kubwa linalowashinda wengine? Kuweka picha ‘Instagram’? Shilole anaifanya sana kazi hii, lakini bado atahitaji msaada wa sauti ya Wema pindi atakapohitaji kusikilizwa na wananchi.

Nini kinatembea ndani ya mwili wa Wema Sepetu? Ndoto za wasichana wengi mitaani ni kuwa kama yeye, lakini cha ajabu mpaka leo, zaidi ya miaka 10 tangu abebe taji la Miss Tanzania, hakuna aliyetimiza ndoto hizo, Wema ameendelea kuishi peke yake kwenye dunia yake!

Kitu pekee walichofanikiwa kuiga kwa Wema ni ile sauti na michoro yake mwilini, mengine yote amebaki nayo peke yake.

Nguvu yake, umaarufu wake na ushawishi wake ni mkubwa kuliko hata baadhi ya Vyama vya Siasa nchini. Wema ameingia rasmi kwenye siasa, ametoka Chama Cha Mapinduzi, CCM, amekwenda Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema. Kwa haraka haraka hakuna anayeona athari ya uhamisho huu, tumechukulia poa tu. Hakuna anayezitazama siasa zetu wala anayeyatazama maisha ya Wema, baada ya tukio hili la kukihama CCM na kwenda kujiunga na makamanda wa Chadema.

Kila kitu kimekwenda kama ambavyo mambo ya Wema yamezoeleka! Kuhusu athari ya kwenye siasa, tuwaachie wanasiasa wenyewe, maana hata tukiwaambia watatupa majibu ya kisiasa pia, acha nimshauri Wema kwenye maisha yake.

Mpaka sasa amecheza na siasa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini je, ameshajiandaa na vishindo vikubwa siku siasa itakapoanza kucheza naye?

Je, yuko tayari kukabiliana na vishindo vya kuwa mwanasiasa wa chama cha upinzani nchini kama Godbless Lema, Tundu Lissu, au wengine barani Afrika kama Kizza Besigye wa kule Uganda ambaye amekuwa akisoteshwa gerezani mara kwa mara?

Ni kwa vipi Wema ataweza kumudu vishindo hivyo kama walivyokutana navyo kina Raila Odinga kule Kenya? Ni hayo tu kwa uchache.

Nimemsikia Wema Sepetu amesema ‘Yuko tayari kwa mapambano’, ni kauli njema inayotoa taswira ya kile kilicho ndani ya moyo wake, lakini je, anajua anakwenda kupambana na kina nani? Je, anajua uwezo na mbinu wanazotumia hao anaotaka kupambana nao?

Anajua ukubwa wa pambano lenyewe na aina ya maadui zake? Ameshajua silaha anazotakiwa kuzibeba kwenye mapambano hayo?

Hapa ndipo tunapotakiwa kumkumbusha Wema ukubwa wa hatua aliyoipiga. Mapambano haya si kama yale ya ‘Instagram’ aliyokuwa akipambana na kina Zari The Boss Lady, huu ni uwanja mwingine kabisa. Hii ni vita iliyobeba imani na maisha ya watu, afunge mkanda sawa sawa.

Kwa namna habari yake ilivyopokelewa na wananchi, ni ishara kuwa si mwanachama wa kawaida aliyetoka CCM na kwenda Chadema. Hapa Wema anatakiwa ajifunze kitu.

Umaarufu wake ni silaha ya siri katika mapambano aliyoyaingia, akijitambua na kujielewa kujua anachofanya, ni rahisi kwake kushinda.

Wengi walio kwenye siasa hivi leo wanapenda kuipata nguvu yake ya ushawishi, wanatamani kupendwa na wananchi kama anavyopendwa yeye, ni vyema akaikumbatia vyema silaha yake.

Siasa ndiyo mchezo pekee unaoweza kumshusha na kuipoteza kabisa ngome kubwa iliyosimama nyuma yake, ni mchezo usio na ‘fair’. Anatakiwa awe makini sana kwenye kuzisema na kuzielewa kauli za wanasiasa.

Binafsi nimeshawahi kukutana na kuzungumza na Wema zaidi ya mara mbili, ni mtu mwenye mitazamo ya mbali na maneno yaliyopangiliwa vizuri. Kama akiamua dunia imkumbuke kama nwanasiasa mkubwa aliyewahi kutokea Tanzania, nafasi iko wazi kwake.

Lakini pia, anaweza akakumbukwa kama mwanasiasa mbovu kuwahi kutokea Tanzania, yote yanawezekana. Ni yeye pekee atakayechagua njia ya kupita.

Anahitaji utulivu mkubwa wa mwili na akili, ajue kipi ni sahihi kufanywa na kwa wakati gani? Nani awe rafiki yake kuanzia sasa? Nani msiri wake katika siasa alizoingia kwa sasa? Lakini kubwa zaidi, anatakiwa aachane na Wema huyu tunayemfahamu kila kukicha.

Vijana wanaoota kuwa kama yeye, wajifunze kutoka kwake. Wananchi wanaompenda, wajivunie kulitamka jina lake, popote pale bila chembe ya hofu.  Tanzania inasubiri kumuona Wema mpya kwenye kurasa nyingine ya kitabu cha maisha yake.

MUNGU AMBARIKI SANA

0655 321 415

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles