25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

ZANACO HII, YANGA CHUNGENI SANA

Na ZAINAB IDDY


WAWAKILISHI wa Tanzania katika mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika, Yanga, Machi 11 mwaka huu watawakaribisha mabingwa wa Ligi ya Zambia, Zanaco wanaojulikana zaidi kwa jina la utani ‘Bankers’, katika mchezo wa pili wa michuano hiyo.

Zanaco FC wanakutana na Yanga baada ya kuwaondoa APR ya Rwanda kwa bao 1-0, baada ya sare tasa jijini Lusaka na ushindi huo mwembamba jijini Kigali mechi ya awali.

Hii ni klabu kongwe barani Afrika, ikiwa na umri wa miaka 32 tu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1985, ingawa historia yao inarudi nyuma mpaka mwaka 1978.

Klabu iliyoanzishwa na benki ya biashara nchini Zambia (NBC) mwanzoni mwa 1978, kama timu ya wafanyakazi wa benki hiyo na hapo ndipo lilipozaliwa jina la Bankers ingawa mwaka 1985, ndio ilianzishwa rasmi.

Umri wa Zanaco ni tofauti na wapinzani wao, Yanga ambao Februari 11, mwaka huu walitimiza miaka 82 toka ilipoanzishwa rasmi 1935, ingawa nao historia yao inaanzia mwaka 1926 wakiitwa The Navigators baadaye New Young na 1935 kuchukua rasmi jina la Dar es Salaam Young Africans.

Zanaco ni miongoni mwa timu zenye mafanikio makubwa nchini Zambia kutokana na uongozi wake kuwa imara, hususani masuala ya kiuchumi, ubora katika hilo umewafanya kumiliki uwanja wao ingawa ni mdogo unaoitwa Sunset Stadium ukiwa unabeba watazamaji 20,000.

Timu hiyo imechukua vikombe saba vya Ligi Kuu inayoitwa Super League, Ngao ya Jamii mara nne, Kombe la Cocacola mara moja, kombe la Mei Mosi mara moja na kombe la shirika la mafuta la BP mara moja.

Zanaco licha ya udogo wake kiumri ni timu ya tatu kwenye historia ya Ligi Kuu Zambia, kulichukua kombe hilo mara nyingi, huku kinara akiwa ni Nkana waliolitwaa mara 12 wakifuatiwa na Mufurila Wanderers mara tisa toka ligi ya nchi hiyo ilipoanzishwa mwaka 1962.

Kwa upande wa kimataifa kwa mara ya kwanza Zanaco FC kushiriki michuano ya CAF ni 2003, wakiondolewa hatua ya kwanza. Hii ilikuwa katika michuano ya klabu bingwa na hivyo kujikuta wakitupwa katika Kombe la Shirikisho ambapo waliishia hatua ya makundi.

Kwa sasa Zanaco wananolewa na mchezaji wao wa zamani swahiba mkubwa wa kocha George Lwandamina wa Yanga anaitwa Mumamba Numba ‘The black mamba’, aliyeichezea timu hiyo kipindi cha ujana wake, lakini pia akiwa ameshazitumikia timu nyingine za Kankola Blades, nafasi ya kiungo, mshambuliaji pamoja na timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’ kabla ya kustaafu mwaka 2006 na kugeukia kufundisha soka, akiwa muumini mkubwa wa mpira wa kushambulia, nguvu na umiliki.

Ukiondoa suala la kutumia walimu wazawa pia Zanaco katika wachezaji wao 30 ni wawili tu raia toka nje, lakini waliobaki wote ni wazawa na wanaonekana kuipa mafanikio timu yao wakati Yanga wao wakiwa na wanandinga wakigeni saba pamoja na watu watatu kutoka nje waliopo kwenye benchi la ufundi.

Si timu ya kubeza kwani ina morali ya ushindi muda wote kwa kuzingatia hilo, Yanga inapaswa kucheza kwa tahadhari huku ikitakiwa pia kuhakikisha inapata ushindi mnono nyumbani ili iweze kusonga mbele.

Lakini pia Yanga chini ya Lwandamina na wenzake waliopo benchi la ufundi hawapaswi kuiandaa timu  kucheza soka la mazoea ambalo ndilo lililosababisha kuondolewa kwenye michuano hiyo mapema mwaka jana, ni ukweli uliowazi kwa Zanaco hii, Yanga chungeni sana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles