28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RANIERI ‘FROM ZERO TO HERO’

MARTIN MAZUGWA NA MITANDAO


MSIMU wa 2015/16 utaendelea kukumbukwa na wapenzi wa klabu ya Leicester City pamoja na kocha Mtaliano, Claudio Ranieri, mara baada ya kuwaongoza mbwa mwitu hao kubeba taji kwa mara ya kwanza tangu ilipoanzishwa miaka 133 iliyopita.

Tarehe ambayo haitosahaulika ni Mei 7, ambapo Leicester City walitangazwa kuwa mabingwa wa EPL na kuweka historia ya aina yake katika nchi ya England ambapo timu hiyo haikupewa nafasi ya kubeba taji.

Licha ya kuwa ulikuwa msimu wake wa kwanza, lakini uwezo aliouonyesha Mtaliano huyo ulimfanya kuingizwa katika orodha ya makocha bora watano wa EPL, huku pia akishinda tuzo ya kocha bora wa mwaka.

Ilikuwa safari iliyoanza kwa furaha, lakini imeisha kwa huzuni kubwa kwa upande mmoja wa Ranieri moja kati ya makocha wenye heshima kubwa barani Ulaya, akiwa amezifundisha klabu kama vile Chelsea, Inter Milan, Juventus, Fiorentina pamoja na Valencia ya nchini Hispania.

Leicester walikuwa sahihi kumtimua Ranieri?

Yalikuwa maamuzi magumu yasiyokuwa na utu kwa uongozi wa Leicester City  kumfuta kazi Mtaliano huyo mwenye umri wa miaka 65 ambaye katika umri huo aliweza kutimiza ndoto za mashabiki wengi wa Leicester ambao walikuwa na hamu ya kushuhudia kikosi chao kikibeba taji EPL.

Mmoja wa mashabiki wakubwa wa klabu ya Leicester City, mtangazaji wa Sky sports na mchezaji wa zamani wa Leicester City, Gary Lineker, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa: “Baada ya yote, Claudio Ranieri, aliyoyafanya kwa Leicester City, ni jambo linalohuzunisha kwa kitendo cha kuondolewa kwake,” alisema Lineker.

Leicester City ambao ni mabingwa watetezi wa EPL msimu uliopita walikuwa katika kiwango bora kiasi cha kutetemesha vigogo lakini hali imebadilika na wapo katika nafasi ya 17 wakichungulia shimo la kushuka daraja.

Mara baada ya mechi 26 za msimu uliopita walikuwa katika nafasi ya kwanza wakiwa na pointi 53 mbili zaidi ya aliyekuwa anamfuatia Tottenham Hotspurs waliokuwa wanashika nafasi ya pili.

Msimu huu wapo katika nafasi ya 17 baada ya kushuka uwanjani katika michezo 25 wakiwa na pointi 21 na mwisho wa msimu walikuwa wamepoteza michezo mitatu pekee tofauti na msimu huu, ambapo  tayari wamepoteza michezo 14 ndani ya EPL.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Aiyawatt Srivaddhanaprabha wa Leicester City alisema: “Ulikuwa msimu bora zaidi kwetu msimu wa 2015-16, lakini tumekuwa katika kipindi kigumu msimu huu.”

Ranieri aliichukua Leicester ikiwa nafasi ya 14 aliipandisha klabu hiyo na kuwa bora huku akitengeneza ukuta mgumu pamoja na safu kali ya ushambuliaji iliyokuwa chini ya Jamie Vardy pamoja na Riyad Mahrez ambao walitengeneza pacha hatari.

Vardy alikuwa straika ambaye alikuwa na uwezo wa kawaida ambapo katika mechi 26 alikuwa amepachika mabao matano kabla ya ujio wa Ranieri mara baada ya kutua kwa Mtaliano huyo ndani ya msimu mmoja katika mechi 36 alikuwa ameingia kambani mara 24.

Kocha ajaye ataweza kuvaa viatu vyake?

Ilikuwa Februari 7, mwaka jana ambapo Leicester City walipoweka rekodi ya aina yake mara baada ya kuishushia kichapo klabu yenye historia kubwa duniani ya Manchester United ilipoizamisha kwa mabao 3-0.

Mara baada ya kuondoka kwa Ranieri yameibuka maswali je, kocha ajaye ataweza kuziba nafasi na kuvaa viatu hivi vya Mtaliano huyo ambaye ameandika rekodi ambayo ni vigumu kufutika? Ni jambo la kusubiri na kuona.

Ranieri atakumbukwa kwa lipi Leicester?

Busu lake mara baada ya kubeba taji lake la kwanza la Ligi Kuu ya England akiwa na mbwa mwitu hao ambao kwa zaidi ya miaka 133 hawakuwa na bahati na taji.

Ranieri atakumbukwa kwa mengi katika jiji la Leicester hasa rekodi yake ya kubeba taji, akiwa mbele ya mtu anayemfuata kwa zaidi ya pointi kumi ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tangu timu hiyo ilipoanzishwa.

Nani anapewa nafasi ya kurithi mikoba yake?

Mtu anayepewa nafasi ya kurithi mikoba ya Ranieri ni raia mwenzake wa Italia, Roberto Mancini ambaye ameweka rekodi katika kikosi cha Manchester City kwa kukipatia taji la EPL msimu wa 2011-12 na kuingia katika orodha ya makocha walioipatia taji timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1880 katika jiji la Manchester.

Hii itakuwa mara ya pili kwa kocha huyo kurudi katika timu hiyo tangu alipoondoka mwaka 2001 alipokuwa hapo kama mchezaji ambapo alicheza michezo minne pekee katika kikosi hicho cha mbwa mwitu.

Kocha huyo anaweza kuwa mrithi sahihi wa kocha Ranieri kutokana na uzoefu alionao katika Ligi Kuu ya England pale alipokiongoza kikosi cha Manchester City kuanzia Desemba 2009 hadi Mei 2013, mbali na kuchukua taji la EPL pia alichukua taji la FA mwaka 2011.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles