25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

NI WAKATI WAKUMKABIDHI SIMBU KIJITI CHA NYAMBUI

NA MARTIN MAZUGWA


NI muda mrefu umepita nchi ya Tanzania imekuwa wasindikizaji katika mchezo wa riadha kutokana na uwekezaji usioridhisha katika mchezo huo ambao umekuwa ukipendwa duniani.

Mara ya mwisho Tanzania kubeba medali ilikuwa mwaka 1980 katika Jiji la Moscow, nchini Urusi ambako mwanariadha mkongwe, Suleiman Nyambui, alibeba medali katika mashindano ya Olimpiki ya mita 5,000 na kuandika historia katika michuano hiyo iliyokuwa inatazamwa na dunia nzima.

Tanzania imekuwa na wanariadha wengi kama vile Juma Ikangaa, Mwinga Mwanjala na Zebedayo ambao ni kati ya wanariadha ambao kwa nyakati tofauti walijaribu kulipigania Taifa kuhakikisha linasonga mbele na kuchukua medali katika mashindano mbalimbali.

Licha ya kupigana kwao ili kuhakikisha taifa linapata sifa kubwa kupitia riadha, lakini suala ambalo lilikuwa kikwazo ni  udhamini ambapo makampuni makubwa yalikuwa yakishindwa kutoa udhamini wao kwa wanariadha wakihofia hasara.

Hivi sasa ni kinyume ambapo mmoja kati ya wanariadha anayeonyesha atawatoa kimasomaso Watanzania ni Felix Simbu, mshindi wa medali katika mashindano ya Standard Chartered Mumbai Marathon yaliyofanyika nchini India mapema mwaka huu.

Simbu ambaye alionyesha uwezo wa hali ya juu, alimaliza mbio hizo kwa muda wa 2:09:32 na kuzawadiwa dola za Kimarekani 42,000 huku akiwaacha midomo wazi, Watanzania ambao walikuwa na shauku ya kuona jambo hilo likitokea kwa kijana wao huyo.

Watanzania wengi wamekuwa mashabiki wakubwa wa mwanariadha mwenye kasi zaidi ulimwenguni raia wa Jamaica, Usain Bolt, ambaye amekuwa akiwagaragaza wenzake kutokana na uwezo wake mkubwa wa kufukuza upepo.

Simbu amefungua njia wengine wamfuate ili turudishe heshima katika mchezo wa riadha ambao tumekuwa wasindikizaji kwa zaidi ya miaka 30 ambayo imekuwa michungu kwa wapenzi wa mchezo wa riadha hapa nchini.

Ni muda mwafaka kwa Simbu kuidhihirishia dunia kuwa kuna kipaji kipya kinachochomoza kwa kasi na huenda katika mashindano yajayo ya Olimpiki yanayotarajia kufanyika mwaka 2020 katika Jiji la Tokyo, Japan akafanya makubwa zaidi.

Wakati anashika nafasi ya tano katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mwaka 2016 nchini Brazil, uwezo aliouonyesha uliwaacha vinywa wazi watu mbalimbali, huku akiweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi tano za juu zaidi ya miaka 30 iliyopita.

Licha ya kufanya hivyo baadhi ya watu walimbeza kuwa hapaswi kusifiwa kwa hatua hiyo kwani kitendo cha kumpa sifa kingefanya abweteke hivyo nchi ingeendelea kuwa na wanariadha wasindikizaji katika mashindano ya Olimpiki.

Mapema mwezi Januari mwaka huu, Simbu amefanikiwa kuwafunga vinywa wale wote waliokuwa wakimbeza kuwa hana uwezo, baada ya kuwabwaga Wakenya ambao mara nyingi wamekuwa  washindani wakubwa katika mashindano mbalimbali ya mbio.

Huu ni muda mwafaka kwa Watanzania kuzidi kumwombea mwanariadha huyu ili aweze kufuta machozi yetu ambayo yametutoka  kwa zaidi ya miaka 30 na mimi rasmi namkabidhi kijiti cha Nyambui, ili amalizie safari aliyoiacha mkongwe huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles