NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, ameagiza Jeshi la Polisi kumuweka mahabusu Ofisa Mthamini Ardhi wa wilaya hiyo, Einhard Chidaga baada ya kukacha ziara yake kwa siku tano mfululizo.
Hapi alitoa agizo hilo baada ya wananchi wa Kata ya Wazo wilayani humo kulalamikia usumbufu wanaoupata katika Kitengo cha Ardhi wanapoomba kupimiwa na kuthaminishiwa maeneo yao.
“Haiwezekani kila siku hapa mthamini anatafutwa ajibu maswali haonekani, naagiza polisi mtafuteni popote alipo na awekwe mahabusu kwa saa 48,” alisema Hapi.
Katika mkutano huo, wananchi walikuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali wakilalamikia viongozi na watendaji wa Mtaa wa Kilimahewa wakimtaka mkuu huyo wa wilaya kuwaondoa kwa sababu wamekuwa wakikwamisha maendeleo ya mtaa wao.
Wakati huohuo, Hapi amepiga marufuku kuendesha mnada katika uwanja wa kwa Mkanada kwa sababu eneo hilo limepita bomba kubwa la maji.
Vilevile, amepiga marufuku wenyeviti wa mitaa kutoza fedha kwa ajili ya huduma mbalimbali za jamii.