26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

DAWA ZA KULEVYA AWAMU YA TATU: HAKUNA ATAKAYEPONA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amemkabidhi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, orodha aliyosema ina majina ya watu 97 ambao ni wafanyabiashara ya dawa za kulevya waliojishughulisha na shughuli hiyo tangu wakati wa Serikali ya awamu ya tatu na ndani yake kuna majina ya watoto wa viongozi.

Hata hivyo, Makonda alikabidhi orodha ya majina hayo bila ya kuyataja hadharani kama ambavyo ilizoeleka katika awamu ya kwanza na ya pili, mfumo uliolalamikiwa na watu wa kila kada.

Makonda alisema orodha hiyo ya awamu ya tatu itatikisa kuliko ilivyokuwa ya awamu ya kwanza na awamu ya pili na kwamba wamekubaliana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kwenda hadi awamu ya saba.

 “Katika awamu hii ya tatu joto litapamba moto kidogo, wauza unga kuanzia awamu ya tatu (wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi) na wale wanaotaka kunusa awamu ya tano, hakuna jiwe litakalosalia juu ya jiwe, tutahakikisha tunasaga mawe yote.

“Wengine wao hawafanyi biashara, lakini wanasimama katikati, yaani wanaweza kumpigia simu kiongozi yeyote au wa uwanja wa ndege halafu watu wakaachwa wakapita na dawa za kulevya,” alisema Makonda.

Alisema Jiji la Dar es Salaam limekuwa likitumiwa kama njia ya kupeleka dawa za kulevya Afrika Kusini na China na kwamba kila siku dawa za kulevya aina ya heroin kati ya kilo 10 hadi 15 zinaingizwa katika mkoa huo.

“Mbinu atakayotumia Kamishna (Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya) siijui, lakini yeye mwenyewe ataamua. Lakini sisi kwetu tunashughulika nayo hadharani, namkabidhi orodha hii kupitia vyombo vyake ashughulike nao.

“Bado tuna awamu nne mbele yetu, viongozi wa dini mjue tu mlitajwa, hivyo sitaona haya kuwashughulikia, mtikisiko utakuja kwa makanisa, tunataka mkoa wetu usafishike,” alisema.

ZINAKOPITA DAWA ZA KULEVYA

Pia alisema kuna bandari bubu 50 na kati ya hizo 27 zinatumiwa kuingiza dawa za kulevya.

Alisema ziko hoteli 67 zina wateja wa kudumu wanaofanya biashara ya dawa za kulevya, nyumba 200 zikiwamo za wanasiasa na klabu 20 zinazodaiwa kujihusisha na biashara hiyo.

“Kuna vijiwe 107 na kuna eneo kuna kinamama wanauza vitumbua, lakini wanakuwa pia wanazo kete za dawa za kulevya. Tulikwenda Kitunda uwanjani saa 11 asubuhi tulimkuta mtu ana kete 30.

“Hivi sasa kuna njia mpya inatumika na wanajiona wajanja wakifikiri hatujui, wanatumia mitungi mirefu ya gesi, inatobolewa halafu wanapakia dawa za kulevya kisha wanaifunga na kuitupa baharini,” alisema.

Alisema pia baadhi ya maduka ya kubadilishia fedha yamekuwa yakihusika kutakatisha fedha chafu zinazotokana na biashara ya dawa za kulevya na kuhoji inakuwaje mkoa mmoja uwe na maduka zaidi ya 200.

“Wanatumia maduka haya kama kichaka, hili ni eneo ambalo tukilifanyia kazi tutasaidia kuwapunguza wakubwa wanaosafirisha fedha.

“Yako maduka yanafanya miamala kwa siku yenye thamani ya Dola za Marekani 100,000 wakati sheria ya Benki Kuu (BoT) hairuhusu. Mwingine akifanya mambo yake China anadumbukiza halafu anakuja kuzichukulia huku,” alisema.

AWAVAA WANAOMPINGA

Makonda alichambua watu wanaopinga vita ya dawa za kulevya, akisema wamegawanyika katika makundi manne.

 “Wengine wako katika kundi la wanufaika, kuna waliopata fedha za kampeni kupitia wauzaji, hivyo hawawezi kukaa kimya, kuna ambao wamefikia kiwango kikubwa cha utumiaji na wengine hawataki kuelewa tu, labda kwa sababu wako upinzani.

“Katika kila kona, kwenye mitandao ya kijamii watu wenye heshima zao wanapiga kelele, Rais mstaafu Kikwete (Jakaya) aliwahi kusema anayo majina na kwa hekima zake alikaa kimya, amekuja Makonda wanapiga kelele, wengine wanasema amekurupuka akae kimya… iwe kwa kutaja majina au kwenda kimya, lengo letu hatutaki dawa za kulevya Dar es Salaam,” alisema.

Alisema wengine ni raia wa Nigeria ambao waliamua kutumia hati za kusafiria za Watanzania na kusababisha kuchafua Taifa la Tanzania.

“Heshima yetu imepotea, leo hii ukionyesha hati ya kusafiria ya Tanzania kwa baadhi ya nchi unawekwa pembeni. Na zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wanaokwenda Afrika Kusini wanafanya biashara hiyo,” alisema.

WALIOITWA POLISI

Makonda aliwataka watu wote walioitwa polisi kujisalimisha na kutishia kuwafukuza kwenye mkoa wake wale watakaokaidi.

“Ukiitwa polisi umepewa heshima nenda, ukisubiri tukufuate utakuwa unatafuta matatizo. Tukimuita mtu ujue tunamfahamu kwa miaka 10… wengine wanaumia tunagusa wapenzi wao, wawasaidie waache na si kupiga kelele.

“Usilete mbwembwe kwenye utawala huu au uongozi wangu, na mimi umri wangu bado ni mdogo, unaniruhusu kujaribu kila kitu, bado nina mamlaka ya kukufukuza kwenye mkoa wangu nikijiridhisha wewe ni hatari… unaweza kumfunga mtu kwa saa 48 halafu ushindwe kumuita polisi?” alisema Makonda.

Alisema miongoni mwa watu walioitwa na kuripoti polisi wengi walikiri kujihusisha na dawa za kulevya na kwamba wengine walipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainika kutumia dawa hizo.

“Wako wengine ni wafanyabiashara wakubwa si rahisi kumkuta hata na unga nyumbani kwake, lakini yeye anatumia simu kufanya biashara hii na namba nyingine zimesajiliwa kwa jina la mwanamke wakati yeye ni mwanamume. Akishafanya mambo yake anatupa simu.

“Wengine walipopekuliwa walikutwa na hati mbili za kusafiria za Tanzania na Marekani wakati nchi yetu hairuhusu, halafu anajiita ni kiongozi wa nchi, tena aliomba na kura na kuchaguliwa na wananchi.

Alisema wengine wakiulizwa wana kiburi tu, lakini wakichukuliwa na kwenda kupimwa kwa Mkemia Mkuu, ni watumiaji wakubwa wa dawa za kulevya.

“Wengine mlizoea viongozi au wafanyabiashara wakubwa wakiwa na mambo yao kesho mnamtafuta, awamu hii hakuna kuitana tena, tunakutana ‘central’ (Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam).

APUNGUZA IDADI YA MARAFIKI

Makonda alisema vita aliyoanzisha ya kupambana na dawa za kulevya, imemsababishia kupunguza idadi ya marafiki.

“Vita hii si ya kawaida, inapunguza idadi ya marafiki, inakutengenezea hofu katika kila mlango unaokanyaga na kutokuwa na imani kama ni sehemu salama, inakufanya uhisi unabaki peke yako, muda wowote roho yako inatoka… uwe na hofu hata na familia yako kutokuwa na uhakika wa usalama wa baba na mama yako, lakini kwa mapenzi ya mwenyezi Mungu vita hii inazidi kuwa ndogo.

“Kila kona kwenye mitandao ya kijamii watu wenye heshima wanapiga kelele, watukane tu mimi nasema matusi yote yale naona kama ni hamasa ya kuendelea kushughulika na wauzaji wa dawa za kulevya.

“Mapambano haya si ya mchezo, ni mapambano ya maisha ya watu, lazima uwe na uhakika na Mungu wako, kama huna uhakika na Mungu uliyenaye usiingie. Ukitaka kuwavusha watu ng’ambo ya pili usijadiliane nao njia ya kupita,” alisema Makonda.

WABUNGE WAPIMWE

Makonda pia alimuomba Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuanzisha utaratibu wa kupima wabunge kabla hawajaingia ukumbini ili kujua kama wanajihusisha na dawa za kulevya.

“Wazo hili Spika Ndugai alikuwa nalo siku nyingi, alipitishe. Na hata hivi vipimo vinaweza kutumika tukafanikiwa kulijenga taifa letu,” alisema.

Pia aliwashauri wazazi na walezi kununua vipimo maalumu ili kuwapima watoto wao kama wanatumia dawa za kulevya au la.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles