27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SIRRO: KWA SIKU 12 TUMEKAMATA 311

Na Asha Bani – DAR ES SALAAM

KAMANDA  wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, amesema kwa siku 12 kuanzia Februari mosi mpaka juzi, wamekamata watuhumiwa 311 wanaojishusisha na biashara hiyo.

Alisema watu hao wamekamatwa kwa ushirikianao na Kamati ya Uchunguzi iliyo chini ya Mkuu wa Mkoa, ambapo kati ya watuhumiwa waliokamatwa wamegawanyika kwenye  makundi matatu.

Alisema kundi la kwanza ni lililokamatwa na vielelezo ambavyo ni  heroine kilo 544, bangi kilo 438, mirungi kilo 21.

Alisema  kundi la pili lina watu 117  na tayari majalada ya kesi zao 42 yameshafunguliwa.

Kundi la tatu alisema lina watu 77 ambao walitakiwa na Mkuu wa Mkoa kujisalimisha  Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam wakiwemo askari 12, wafanyabiashara, viongozi wa dini, wenye kumbi za starehe  na vituo vya mafuta.

Alisema hadi sasa bado watuhumiwa 45 kati ya waliotakiwa kufika Kituo Kikuu cha Polisi, hawajajitokeza kuhojiwa na kwamba juhudi watasakwa popote walipo.

 “Katika makundi hayo tayari majalada matatu yenye watuhumiwa 16 wako mahakamani, huku mengine 18 yakiwa yanaendelea na uchunguzi,’’alisema Kamanda Sirro.

TID

Kwa upande wake msanii wa muziki wa bongo fleva, Khalid Mohamed, maarufu TID amesema hatotumia tena dawa hizo na kwamba anaunga mkono juhudi zinazoendelea sasa za kutokomeza biashara hiyo haramu.

TID ambaye hivi karibuni alikuwa miongoni mwa wasanii waliotajwa katika sakata la dawa za kulevya alisema anajutia nafsi yake kwa kujiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya.

‘’Hapa najiona kama kijana niliyepotea njia nimerudi, nilikosea sana familia yangu  mama yangu, jamii yangu  kwa ujumla.

“Naomba Mungu  anisimamie,  mnisamehe  kijana  bado nipo shupavu, mpambanaji  na Mnyama  na vita hii lazima uwe Mnyamwa,’’alisema TID.

Alisema hatojali wangapi kusema yeye kuwa msaliti ‘Snitch’ si kweli mtoto wangu Jamal asije kuwa kama Baba yake .

Alisema kuwa ni shetani tu lakini Mungu amesaidia kutokomeza na anaamini kwamba Muziki bila dawa inawezekana.

RAMADHANI MADABIDA

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM ) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida alisema hata ilani ya chama hicho imeelekeza juu ya athari za matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema yanayofanywa na Serikali kwa sasa ni katika kutekeleza ilani ya chama hicho.

“Nipo hapa kuona kwamba  tuliyoyaagiza   wanatekeleza  vinginevyo  tutawaadabisha ,tayari tumeshaanzisha mamlaka kinachohitajika ni usimamizi,’’alisema Madabida.

WAATHIRIKA

Naye Mwathirika wa dawa za kulevya ambaye ni mlezi wa kituo cha Sober Kigamboni, Nuru Suleiman, alisema Mkuu wa Mkoa yupo sawa katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Aliwataka watu wanaomsakama mkuu huyo kupuuzwa kwani endapo watu wakiachwa watumie kuna athari kubwa za maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (HIV) pamoja na kuathirika kiafya pia.

Nao watoto walioathirika na dawa hizo ambao wanalelewa katika kituo hicho mwenye umri wa miaka 11 na 16 wamewatoa watu machozi  kutokana na simulizi zao.

Mtoto wa miaka 16 (Jina limehifadhiwa) amesema alianza kutumia akiwa na miaka 9 na alishawishiwa na mwanamume aliyeeleza kuwa alikuwa akifanya naye mapenzi.

Alisema mwanamume  huyo baada ya kufariki akajiingiza katika biashara ya kuuza mwili maarufu kwa jina la uchangudoa  ili aweze kupata fedha za kujikimu na kununua dawa hizo.

Alisema kwa sasa ameshapata maambukizi ya HIV na anaishi kwa matumaini.

Naye mtoto wa miaka 14 (jina limehifadhiwa),alisema yeye alianza akiwa mdogo hadi kumsababishia kufanya vibaya matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

SHEIKH WA MKOA

Awali Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum alisema akiwa mwenyekiti wa kamati ya amani ya dini mkoani humo alisema jambo hilo ni kubwa na linahitaji mapambano.

Alisema asitarajie mtu kupendwa na watu akiwa kwenye hayo mapambano bali atapendwa na Mungu na kama mtu anataka kupendwa na watu basi atakuwa ni zaidi ya Mtume  Muhammad  na Yesu Kristu ambao hata wao baadaye walichukiwa na kuteswa.

CHID MAPENZI

Mkuu wa Mkoa pia alilitaja Jeshi la Polisi kuwakamata mfanyabiashara wa maduka ya nguo Rashidi Said anayejulikana kama Chid Mapenzi ‘Mapenzi Classic’ ambaye pia ni mume wa msanii wa filamu Shamsa Ford ambaye walifunga ndoa hivi karibuni.

Mwingine ni Mfaume Kiboko ambaye alitakiwa kukamatwa na kupelekwa kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano .

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles