31.1 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

PORI LA LOLIONDO YATENGANISHWA

 

Na Masyaga Matinyi, Loliondo

HATIMAYE Serikali imeridhia kutenganishwa kwa Pori Tengefu la Loliondo (LGCA), ambalo sasa kilometa za mraba 1,500 zitatumika kwa shughuli za uhifadhi na 2,500 zitabaki kwa matumizi ya wananchi.

Hatua hiyo ya Serikali inahitimisha moja ya migogoro mikubwa ya ardhi kuwahi kutokea nchini, ambao umedumu kwa zaidi ya muongo mmoja ukihusisha Serikali, wadau wa uhifadhi, wananchi, wanasiasa, wawekezaji, asasi za kiraia na baadhi ya balozi za kigeni zilizopo nchini.

Akiwa katika ziara ya ghafla katika eneo hilo juzi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema uamuzi huo unalenga kuilinda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ambayo uhai wake unategemea kwa kiasi kikubwa uhai wa pori hilo.  

Eneo hilo ni muhimu kwa sababu ni sehemu ya mazalia na mapito (ushoroba) ya wanyamapori na ndipo vyanzo vikuu vya maji kwenda Serengeti vinapatikana.

Profesa Maghembe alifanya ziara hiyo kwa lengo la kujionea kazi inayoendelea ya uwekaji alama za mipaka (beacons), inayofanywa na maofisa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, lililoelekeza kutambuliwa na kuwekwa alama kwa maeneo yote ya uhifadhi.

Pia alitumia fursa hiyo kushuhudia uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji unaofanywa na wafugaji, wakiwamo kutoka nchi jirani ya Kenya wanaoingiza maelfu ya mifugo kinyume cha sheria, ambao alikutana nao.

 “Kwanza niwapongeze wote mnaofanya kazi ya uwekaji wa alama za mipaka kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu, utambuzi wa maeneo haya ni jambo la lazima na muhimu sana.

 “Uhakiki wa mipaka ya hifadhi zetu, mapori tengefu na mapori ya akiba unafanyika kama sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu alilolitoa hivi karibuni, kwa hiyo wote tunapaswa kushiriki na kutoa ushirikiano, asitokee mtu wa kupinga hili.

 “Kuna watu kutokana na masilahi binafsi, wanapingana na maelekezo halali ya Serikali, nasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni moja tu, hakuna Jamhuri ya Ololosokwan ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Profesa Maghembe.

 Ololosokwan ni kijiji maarufu ndani ya Pori Tengefu la Loliondo kutokana na kuingia mikataba na wawekezaji wa nje kinyume cha sheria, pia wakazi wake wamekuwa mstari wa mbele kupinga kutenganishwa kwa eneo hilo, harakati ambazo zimekuwa zikiungwa mkono na asasi za kiraia (NGOs) zilizopo Loliondo.

TAMKO LA KUIGAWA LGCA

Akiwa katika eneo lijulikanalo kama Kleins Gate, ambako unapita Mto Grumeti kuelekea Serengeti, Waziri Maghembe alishuhudia makundi makubwa ya mifugo, ambayo nyakati za usiku huingizwa ndani ya hifadhi ya Serengeti kwa malisho.

Pia alijionea jinsi mto huo muhimu ulivyokauka kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji, unaotokana na wingi wa mifugo katika eneo hilo, pamoja na hali ya ukame iliyopo sasa.

“Hii hali inatisha na kuhuzunisha, haiwezekani kuacha iendelee, ni lazima mimi kama waziri mwenye dhamana ya uhifadhi na maliasili kufanya maamuzi magumu, vinginevyo miaka ijayo hakutakuwa na Serengeti.

 “Hakuna asiyefahamu umuhimu wa Serengeti, hifadhi hii ni kivutio cha aina yake Afrika na duniani kote, sasa tutakuwa watu wa ajabu sana kama tutaruhusu haya yanayotokea yaendelee.

“Kwa mujibu wa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009, sehemu ya 16 vifungu Na. 4, 5 na 6, nikiwa waziri mwenye dhamana, natamka kwamba LGCA itenganishwe mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles