25.4 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

WANANCHI KENYA WAGOMEA HOTUBA YA RUTO

BUNGOMA, KENYA


William-RutoNAIBU Rais, William Ruto kwa mara nyingine amekabiliwa na wakazi wenye hasira waliomkataa kuwahutubia na kumlazimu kukatiza ziara yake katika kituo cha magari mjini Bungoma.

Ruto aliyekuwa ametoka Mumias alikokutana na wafuasi wa Chama cha Jubilee (JP), alikuwa amepanga kuhutubia wakazi katika kituo hicho cha mabasi.

Lakini kundi la vijana waliokuwa wakiimba nyimbo za kuunga mkono muungano wa upinzani wa NASA pamoja na chama cha ODM, lilizuia msafara wake kuingia mjini humo na polisi wakawa na wakati mgumu kukabiliana nao.

Vijana hao waliharibu mabango na karatasi zilizokuwa na ujumbe wa Jubilee walizokuwa wamepewa na gavana wa Bungoma, Ken Lusaka.

“Msituletee kampeni zenu wakati huu baada ya kutupuuza kwa miaka yote hii. Sisi vijana hatutaki kuhutubiwa. Tumeteseka vya kutosha,” kijana mmoja alisikika akisema.

Walilalamika wakisema ingawa Naibu Rais amezuru Bungoma mara kadhaa, eneo hilo bado liko nyuma kimaendeleo.

Vijana hao waliokuwa na hasira pia walichoma fulana zenye nembo ya Jubilee wakisema eneo hilo ni ngome ya NASA na Cord.

“Tumechoka na Jubilee, hapa ni ngome ya Nasa. Uzeni Jubilee kwingine si hapa Bungoma. Jubilee imetutesa sana,” akasema mmoja wao.

Msafara wa Naibu Rais ulilazimika kubadilisha mkondo na kupitia katika barabara ya Kanduyi ili kukwepa eneo la katikati mwa mji walimokuwa vijana hao.

Msafara huo ulikuwa ukitoka Kakamega ambako Ruto alikutana na wajumbe wa Jubilee kutoka kaunti za Kakamega na Vihiga.

Tukio hilo lilitokea wakati ambapo kinara wa Cord,  Raila Odinga alikuwa akitarajiwa kupitia mjini Bungoma akielekea Lugari na Turbo.

Hiyo ni mara ya nne kwa Ruto kukutana na upinzani wa aina hiyo.

Desemba 5, 2016 mjini Garissa, naibu wa rais alizomewa na vijana waliokuwa na hasira. Wakazi wa mji huo walikataa miradi ya maendeleo ambayo Bw Ruto alikuwa amewapelekea akiandamana na Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale.

Wakati huo wakazi hao walitaja jina la kinara wa Cord, Raila Odinga na kusikika wakikejeli kauli mbiu ya Jubilee ya ‘Tuko Pamoja’ na kusema “Hatuko Pamoja”.

Aidha Januari 19, 2017, Ruto alipingwa na kundi la vijana mjini Narok.

Vijana hao walifika katika shule ya upili ya Sogoo, eneo Bunge la Narok Kusini, na kumpigia kelele alipokuwa akiwahimiza wachukue kadi za kura.

Walilalamika kuwa serikali imekuwa ikiwatafuta tu inapohitaji kura zao ilhali eneo lao lina barabara mbovu, hali duni ya afya na ukosefu wa kazi kati ya mengine.

Kadhalika Januari 22, wakazi wa Baringo walimkemea naibu wa rais kwa kujaribu kuwalazimisha kiongozi anayewafaa katika kaunti yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles