25.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Lowassa, Mbowe wasaidia waathirika Kahama

freeman MboweSitta Tumma na Paul Kayanda, Kahama
MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), ametoa msaada wa Sh milioni 5 kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kahama, Mkoa wa Shinyanga.
Fedha hizo zilikabidhiwa jana na Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga.
Wakati wa makabidhiano hayo, waathirika 250 waliohifadhiwa katika Shule ya Msingi Mwakata, walikuwapo pia.
Akizungumza kwa niaba ya Lowassa, Mgeja alisema mbunge huyo alisema yeye na familia yake walisikitishwa na tukio hilo, na kwamba njia pekee ya kuwatia nguvu waathirika ni Watanzania kuungana pamoja ili kuwasaidia.
“Ni vema Watanzania wakajenga mshikamano wa kweli na umoja wakati wote kwa sababu hata mimi nimeguswa na maafa haya,” alisema Lowassa huku akiahidi kutoa ushirikiano kila atakapotakiwa kufanya hivyo.
Katika mazungumzo yake, Mgeja alisema Lowassa alikuwa amepanga kuwatembelea waathirika hao ili kuwapa pole, lakini kutokana na kubanwa na majukumu mengine, alishindwa kufanya hivyo.
“Mheshimiwa Edward Lowassa ametuma msaada wake wa shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zetu, jamaa zetu na Watanzania wenzetu mliopatwa na maafa haya. Amewaomba Watanzania wengine wote waonyeshe kuguswa na tatizo hili.
“Pamoja na hizi shilingi milioni 5 alizotoa, ndugu yetu Lowassa amesema yuko pamoja nanyi na ataendelea kushirikiana nanyi kwa maombi wakati wote.
“Hii ni Tanzania moja, sote ni wamoja, tushirikiane pamoja, tupendane, tusaidiane na kushikamana pamoja kwa sababu haya yaliyotokea ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu,” alisema Mgeja kwa niaba ya Lowassa.
Pia alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wengine katika kuhakikisha waathirika wote wanaishi maisha ya kawaida ingawa walipata madhara wakati wa mafuriko hayo.
Naye Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, alimpongeza Lowassa kwa msaada wake huo na kusema ni kiongozi anayejali na kuthamini utu wa mtu bila kujali jinsia na umri.
Kutokana na msaada huo, alisema ipo siku Mungu atamlipa mbunge huyo kwa kuwa anaonekana kuwajali watu wanaopatwa na matatizo.

MBOWE AWAFARIJI WAATHIRIKA
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, jana aliwasili wilayani Kahama na kuwatembelea waathirika katika Kijiji cha Mwakata.
Baada ya kufika kijijini hapo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alipokewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, aliyemsindikiza kwenda kuwatembelea waathirika hao.
Wakati wa ziara hiyo, Mbowe aliongozana na viongozi kadhaa wa Chadema, wakiwamo Mbunge wa Viti Maalumu, Rachel Mashishanga, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu, Meya wa Manispaa ya Musoma, Alex Kisurura na Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi.
Akizungumza na waathirika hao, Mbowe aliwaomba Watanzania waungane bila kujali tofauti zao kisiasa katika kuwasaidia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles