NA ZAINAB IDDY
JUMANNE iliyopita uongozi wa timu ya Azam FC, ulimtambulisha kocha wao mpya, Mromania Aristica Cioaba, akirithi mikoba ya Mhispania, Zeben Hernandez, aliyesitishiwa mkataba pamoja na benchi lake zima la ufundi.
Mromania huyo atasaidiana na makocha wazawa, Idd Nassor ‘Cheche’ na kocha wa makipa, Idd Abubakar ambao wameingiza timu hiyo katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi yaliyomalizika Ijumaa iliyopita na timu hiyo kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, baada ya kufungashiwa virago kwa Hernandez.
Ujio wa kocha huyo unaweza kufufua matumaini mapya kwa mashabiki na wapenzi wa Azam FC, kutokana na kikosi chao kuandamwa na matokeo yasiyoridhisha msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Itakumbukwa kwa takribani miaka nane Azam imebadili benchi lake la ufundi zaidi ya mara tisa, ikiwa ni wastani wa kufukuza kocha kila mwaka.
Tabia ya kutimua timua makocha kila mwaka inaendana na utamaduni wa kocha wao mpya ambaye tangu mwaka 2005, amefundisha katika timu 10 tofauti.
Msimu uliopita, Cioaba aliiongoza Aduana Stars ya Ghana kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Ghana, lakini mbali na timu hiyo ameshakuwa katika benchi la ufundi la miamba ya Morocco, Raja Casablanca mwaka 2005 kocha msaidizi kabla ya kutua Al Masry ya Misri katika nafasi hiyo mwaka uliofuata.
Kocha huyo pia ameshazifundisha timu za Bals inayoshiriki ligi ya Romania (2007/9) akiwa kocha mkuu, kabla ya kutua Al-Tadamun inayoshiriki Ligi Kuu ya Kuwait akiwa kocha msaidizi (2009/10) kisha kwenda Jordan kuinoa Shabab Al-Ordon, akiwa mkuu wa benchi la ufundi la timu hiyo (2010).
Cioaba hakuishia hapo, baada ya kutimkia Ghana kukinoa kikosi cha Aduana Stars (2011/12), msimu uliofuata alikabidhiwa jukumu la ukocha katika kikosi cha Saham ya nchini Oman, lakini hakuweza kudumu na hivyo kuamua kuachia ngazi na kwenda kutua mikononi mwa Al-Oruba SC ya nchini humo (2013/14).
Julai 2014, kocha huyo aliamua kuachana na timu ya Al-Oruba SC na kwenda nchini Kuwait kujiunga katika kikosi cha Al-Shabab SC, lakini nako alikaa msimu mmoja na kurejea kwenye timu yake ya zamani ya Saham nchini Oman, kabla ya kutua tena Aduana Stars walikomwona Azam.
Kutokana na mfumo wa soka la kisiasa la Tanzania, unaoendeshwa na viongozi wa timu zetu ni vigumu kocha huyo kuwa na maisha marefu, lakini pia hata kama uongozi wa wanalambalamba ukiamua kuvuta subira kwake bado yeye mwenyewe hataweza kusalia kwakuwa ameshazoea kubadili timu kila mara.
Ukiangalia safari ya Cioaba haina tofauti yoyote na tabia ya uongozi wa Azam, kwani kila mwaka wamekuwa watu wa kufanyia mabadiliko benchi lake la ufundi na hapo ndipo linapokuja swali, iwapo kama ndoa ya pande hizo mbili itaweza kudumu.