BADI MCHOMOLO NA MITANDAO
MSIMU wa mwaka 2015, nyota wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, alifanikiwa kuchukua tuzo ya mchezaji bora wa dunia ‘Ballon d’Or’ dhidi ya mpinzani wake Cristiano Ronaldo ambaye anakipiga katika klabu ya Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno.
Kulikuwa hakuna sababu mchezaji huyo ya kushindwa kuchukua tuzo hiyo kutokana na mchango wake ambao aliutoa ndani ya timu hizo. Ronaldo ambaye alishindwa tuzo hiyo alijua mapema kwamba hawezi kuchukua msimu huo kutokana na kushindwa kufanya makubwa kwa timu zake.
Baada ya kugundua hilo Ronaldo alisema ‘Mwache Lionel Messi achukue tuzo hiyo ya Ballon d’Or, ana kila sababu ya kuchukua kutokana na kuifikisha timu yake ya taifa fainali za Copa America, pamoja na kutoa mchango mkubwa katika klabu yake na kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini chochote kinaweza kutokea kwa kuwa watu wanapiga kura,” alisema Ronaldo
Hivyo ndivyo anaweza kusema Messi Leo hii kuelekea kwenye tuzo za mchezaji bora wa mwaka wa FIFA 2016, ambapo katika tuzo hiyo wachezaji wanaowania kwa sasa ni Messi, Ronaldo na Antoine Griezmann wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa.
Ni wazi kwamba hakuna sababu ya Ronaldo kushindwa kutwaa tuzo hiyo usiku wa leo, hata Messi analijua hilo, ila ni vizuri kumsikia mwenyewe akitoa kauli yake kwamba ‘Mwacheni Ronaldo achukue tuzo ya mchezaji bora wa mwaka.”
Ronaldo anavigezo vyote dhidi ya wapinzani wake ambao ni Messi na Griezmann, kwa kuwa Ronaldo alitoa mchango wake ndani ya klabu huku akiisaidia kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika fainali dhidi ya Atletico Madrid, pia alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Euro 2016 baada ya kuwachapa Ufaransa kwenye viwanja vya nyumbani.
Hata kama Ronaldo hasingekuwa kwenye kinyang’anyiro hiki bado Messi hasingeweza kutamba mbele ya Griezmann ambaye aliipeleka klabu yake fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, pamoja na timu yake ya Ufaransa katika fainali ya Euro 2016, lakini kwa upande wa Messi hakuwa na msimu nzuri mwaka jana dhidi ya wachezaji hao, kikubwa ni kwamba amekuwa na uwezo binafsi.
Kutokana na sababu hizo ni wazi kwamba Ronaldo anastahili kutwaa taji hilo mwaka msimu huu na hana mpinzani, ugumu ungekuwa ametwaa taji moja na lingine lingechukuliwa kati ya wapinzani wake ndipo kungekuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa wangeangaliwa sehemu zingine ambazo walizisaidia timu zao.
Hata hivyo Ronaldo kwa mwaka 2016 alifanya makubwa kama vile kutwaa taji la Klabu bingwa ya dunia ambapo fainali zake zilifanyika nchini Japan Desemba mwaka jana, hivyo ameweza kutwaa mataji makubwa matatu muhimu, huku akichukua mataji mengine binafsi kama vile Ballon d’Or.
Tuzo ambazo zitatolea usiku wa leo hii ni pamoja na mchezaji bora wa mwaka kwa upande wa wanaume, mchezaji bora kwa upande wa wanawake, huku wachezaji wanaowania tuzo hiyo kwa wanawake ni pamoja na Melane Behringer (Bayern Munich/Ujerumano), Carli Lloyd (Houston Dash/USA) na Marta (FC Rosengard/Brazil).
Kocha bora wa mwaka kwa upande wa wanaume huku nafasi hiyo ikiwaniwa na Claudio Ranieri (Leicester City), Fernando Santos (Ureno) na Zinedine Zidane (Real Madrid). Wakati huo kocha bora kwa upande wa wanawake ni Jill Ellis (Marekani), Silvia Neid (Ujerumani) na Pia Sundhage (Sweden).
Bao bora la mwaka huku wachezaji wanaowania ni Lionel Messi na Neymar kutoka klabu ya Barcelona. Tuzo ya Fair Play kwa klabu huku msimu ulipita ikichukuliwa na Barcelona.