26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WAKUCHUNGWA MICHUANO YA AFCON 2017

NA BADI MCHOMOLO


riyad-mahrezMICHUANO ya 31 ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON), inatarajia kuanza kutimua vumbi wiki hii nchini Gabon huku miamba 16 ikitarajia kuoneshana uwezo kisoka.

Michuano hiyo inatarajia kuanza Januari 14 na kumalizika Februari 5 mwezi ujao. Gabon wao wamefanikiwa kufuzu kama waandaji wa michuano hiyo.

Leo hii Mtanzania Spotikiki, imekufanyia uchambuzi wa baadhi ya wachezaji wa kuchungwa katika michuano hiyo kutokana na uwezo wao ule ambao wameuonesha katika Ligi mbalimbali ambazo wanashiriki barani Ulaya kati ya wachezaji 26 ambao wameitwa katika vikosi vyao.

Riyad Mahrez

Huyu ni nyota wa soka kutoka nchini Algeria, mwenye umri wa miaka 25, mshambuliaji huyo anakipiga katika klabu ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini England, Leicester City.

Mbali na kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa msimu uliopita, lakini mchezaji huyo aliweza kutwaa uchezaji bora wa Ligi hiyo.

Kutokana na mchango mkubwa kwa klabu yake na timu ya taifa, aliweza kutwaa tuzo ya mwanasoka bora barani Afrika kwa wale ambao wanacheza soka la kulipwa Ulaya, tuzo hiyo ilitolewa na Shirika la utangazaji nchini Uingereza BBC.

Hata hivyo wiki iliopita ameweza kutwaa taji lingine la mchezaji bora wa mwaka barani Afrika kwa wale ambao wanacheza Ulaya.

Huyu ni miongoni mwa wachezaji wa kuchungwa katika michuano hii msimu huu akiwa na timu yake ya Algeria akiongoza safu ya ushambuliaji.

Pierre Aubameyang

Nyota huyo atakuwa kwenye viwanja vya nyumbani huku idadi kubwa ya mashabiki nchini Gabon wakimuangalia yeye kutokana na uwezo wake. Mshambuliaji huyo anakipiga katika klabu ya Borussia Dortmund ya nchini Ujerumani ambaye amekuwa ni hatari katika safu ya ushambuliaji.

Kutokana na uwezo wake kuwa mkubwa, mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid wameonesha nia ya kuitaka saini ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27. Nyota huyo alikuwa katika orodha ya wachezaji tano bora wanaowania tuzo ya BBC ambayo ilichukuliwa na Mahrez.

Hata hivyo msimu uliopita alichukua tuzo ya mchezaji bora barani Afrika kwa wale ambao wanacheza soka la kulipwa barani Ulaya

Sadio Mane

Katika wachezaji hatari kwa sasa ndani ya klabu ya Liverpool ya nchini England hauwezi kuliacha jina la mshambuliaji huyo raia wa nchini Senegal. Mchezaji huyo alijiunga na klabu ya Liverpool mwaka jana akitokea klabu ya Southampton kwa kitita cha pauni milioni 34, sawa na zaidi ya bilioni 89 na kumfanya kuwa miongoni mwa wachezaji kutoka Afrika ambao wamesajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, akiwa na urefu wa futi 5 na inchi 9, alikuwa tishio katika orodha ya wachezaji watano ambao walikuwa wanawania mchezaji bora wa Afrika ambaye anakipiga soka barani Ulaya, ambapo alikuwa anashindana na Yaya Toure, Pierre Aubaneyang na Riyad Mahrez.

Mashabiki wengi wa Afrika ambao wanashabikia klabu ya Liverpool ya nchini England ni wazi watakuwa wanamtolea macho mchezaji huyo katika michuano hii Afcon.

Eric Bailly

Baada ya mchezaji huyo kuitwa katika kikosi chake cha timu ya taifa ya nchini Ivory Coast, kocha wa klabu ya Manchester United, Jose Mourinho aliweka wazi kwamba, amechukia na maamuzi ya mchezaji huyo kuitwa ndani ya kikosi cha taifa.

Mourinho anaamini kuwa ubora wa klabu yake hasa katika safu ya ulinzi, inachangiwa na uwezo wa beki huyo mwenye umri wa miaka 22, hivyo anatarajia kutoa mchango mkubwa katika michuano hii ya Afcon huku timu yake ikitarajia kutetea ubingwa.

Mohamed Elneny

Huyu ni nyota wa soka wa klabu ya Arsenal, ambaye anashiriki michuano hii akiwa na kikosi chake cha timu ya taifa ya Algeria, huku mchezaji huyo akiwa na umri wa miaka 24.

Mchezaji huyo alijiunga na klabu ya Arsenal akitokea FC Basel mwaka jana, amekuwa na mchango mkubwa katika safu ya kiungo ya klabu yake ya Arsenal, hivyo anatakiwa kuchungwa ndani ya kikosi cha Algeria.

Wilfried Zaha

Huyu ni nyota wa klabu ya Crystal Palace ya jijini London, amekuwa na mchango mkubwa sana katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24, akiwa na urefu wa futi 5 na inchi 11, itakuwa ni mara yake ya kwanza kuitumikia timu ya taifa ya Ivory Coast lakini awali alikuwa anaitumikia timu ya taifa ya England ya vijana miaka 19 na 21.

Lakini mchezaji huyo alizaliwa mjini Abidjan, nchini Ivory Coast, lakini aliamia nchini England akiwa na umri mdogo, ila mwaka jana alionesha uzalendo na kuomba kulitumikia taifa lake.

Uzoefu wake wa kucheza soka nchini England, unaweza kuleta makubwa ndani ya kikosi cha Ivory Coast, hivyo ni miongoni mwa wachezaji wa kuchungwa kwenye michuano hiyo.

Kutokana na hali hiyo wengi wanawapa nafasi Ivory Coast kutokana na kuwa na wachezaji wenye uzoefu wa michuano mikubwa, lakini hadi kufikia Februari 5 kila kitu kitakuwa wazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles