MWANDISHI wa habari mkongwe, Ali Saleh Ali, ni miongoni mwa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) waliochukua fomu za kuwania nafasi ya ubunge wa Mji Mkongwe visiwani Zanzibar. Kaimu Katibu wa jimbo hilo wa CUF, Nassor Amin Said, alisema mwandishi huyo anafanya idadi ya wanachama wane waliojitokeza hadi sasa kuchukua fomu za ubunge ambapo wawili ndio waliorejesha. Aliwataja wanachama wengine ni waliochukua fomu kuwa ni Mohamed Noor Mohamed, Badru Adam Ali na mbunge wa sasa anayetetea nafasi yake Mohamed Ibrahim Sanya. Alisema wanachama wengine wa chama hicho visiwani Zanzibar wanaendelea kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa ngazi ya uwakilishi na udiwani. Kujitosa katika kinyang’anyiro hicho kwa mwandishi huyo wa habari, kumetafsiriwa na wachambauzi wa mambo ya siasa kuwa kumeongeza msisimko kwa siasa za Zanzibar, hususani kwa CUF ambapo mbunge wa sasa, Sanya anatajwa kuwa bado ana nguvu za kuweza kunyakua jimbo hilo. Katibu wa Jimbo la Mtoni wa CUF, Kitwana Juma Kombo, alisema hadi sasa wamejitokeza wanachama watatu kuchukua fomu za ubunge, ambao ni Ali Ame Ali, Ame Khamis Ame na Radhid Mohamed Ali. Kwa upande wa udiwani ni Safia Mahamoud Aboud, Salim Mikidadi Hamad, Rished Ali Kassim, Masoud Ali Omar na Shaib Makame Hamad.